Rafiki yangu mpendwa,

Ni siku nyingine ya juma ambapo tunakutana hapa kwa ajili ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa ambayo tunayatamani sana.

Changamoto hazimaanishi kwamba safari haiwezekani, bali ni mtihani wa kutupima utayari wetu wa mafanikio tunayoyataka. Kwa sababu mafanikio ni dhamana kubwa, hivyo inabidi yaende kwenye mikono salama.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya fedha kupotea kwenye biashara. Pale ambapo mtu unauza sana kwenye biashara, lakini mwisho wa siku huoni faida na biashara inazidi kuanguka.

Wale wasiopenda kujifunza kuhusu biashara na mzunguko wa fedha kwenye biashara, huwa wanasema kuna chuma ulete, kwamba kuna watu wenye nguvu fulani, ambao wanaweza kuondoa fedha kwenye biashara zao bila ya wao kujua.

Hiki ni kitu ambacho watu wanaamini sana, na ni moja ya vitu vya uongo sana ambavyo watu wanaviamini mno.

Nimekuwa nasema kila siku kwamba hakuna namna yoyote mtu anaweza kuondoa fedha kwenye biashara yako kwa muujiza, lazima umruhusu wewe mwenyewe kwa kumpa au kuwa mzembe na ukaibiwa.

Narudia kusema tena ya kwamba kile watu wanaita chuma ulete, ni uzembe wao binafsi na hakuna mtu mwenye nguvu ya kuvuta fedha kwenye biashara yoyote ile, hayupo, kabisa. Na kama yupo namkaribisha aje avute fedha kwangu.

Na kwa wale ambao bado wanasisitiza kuhusu chuma ulete, nimekuwa nawaambia kitu kimoja, kama kuna chuma ulete kwenye biashara, basi ni wao wenyewe. Ndiyo, kama umewahi kulalamika kwamba kuna chuma ulete kwenye biashara yako, basi chuma ulete huyo ni wewe mwenyewe. Uzembe wako mwenyewe na kukosa nidhamu ya fedha ndiye chuma ulete mkubwa anayeua biashara zako.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Sasa leo tutakwenda kushauriana jinsi ya kuzuia upotevu wa fedha kwenye biashara yako na kuweza kuiona faida unayotengenea. Lakini kabla hatujaingia kwenye ushauri huo, tuyapate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

“Nauza bidhaa lakini faida hamna najikuta duka linakufa tu nifanyeje?” – Maly C. P.

Rafiki, kama unafanya mauzo kwenye biashara yako, lakini huoni faida, na biashara inakufa, hatuhitaji shahada ya biashara kukuambia kwamba tatizo la biashara hiyo ni moja; INAPOTEZA FEDHA.

Biashara hiyo inaweza kuwa inapoteza fedha kwa kujiendesha kwa hasara, kwamba ukichukua mauzo na kutoa manunuzi na gharama za kuendesha biashara unabaki na deni, yaani manunuzi na gharama za kuendesha biashara ni kubwa kuliko mauzo. Hivyo mtaji unakuwa unapungua kwa sababu unaingia kwenye gharama za kuendesha biashara.

Pia biashara inaweza kuwa inapoteza fedha kwa uzembe wa usimamizi wa mzunguko wa fedha. Na kwa biashara nyingi ndogo, tatizo huanza pale mmiliki anaposhindwa kutofautisha matumizi ya fedha zake binafsi na fedha za biashara. Mtu anapokuwa na fedha kwenye biashara, anafikiri ni zake na hivyo kutumia atakavyo, kinachotokea ni biashara kukosa mtaji wa kujiendesha na kufa.

Kuzuia upotevu wa fedha kwenye biashara yako na kuzuia biashara yako kufa, zingatia mambo yafuatayo;

  1. Itenge biashara yako na wewe binafsi.

Biashara yako siyo wewe, biashara yako ni kitu tofauti kabisa na wewe, hivyo unapaswa kutengeneza mipaka kati yako na biashara yako.

Fedha za biashara zikae kwenye biashara na fedha zako binafsi ndiyo zinae kwako. Usichukue fedha kwenye biashara na kuziweka kwenye matumizi binafsi. Usichukue vitu kwenye biashara kwa kuwa ni yako na kutokuvilipia.

Pia usitumie fedha za biashara kwa mambo yako binafsi, badala yake kuwa na kiasi cha fedha unachojilipa kutoka kwenye biashara yako, na kiasi hicho kitokane na faida inayopatikana, hicho tu ndiyo unaweza kutumia.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuepuka CHUMA ULETE Kwenye Biashara Yako.

  1. Zijue namba zako za kibiashara.

Wahenga walisema mali bila ya daftari hutumika bila ya habari. Kujua namba zako za kibiashara ni muhimu sana, tena zijue wakati wote. Jua manunuzi uliyofanya kwenye biashara, jua mauzo unayofanya, jua gharama zote za kuendesha biashara yako na pia jua faida halisi unayoipata.

Usifurahie tu kuona mauzo makubwa, jua faida halisi, unaweza kuwa na mauzo makubwa, lakini ukawa hauingizi faida, kitu ambacho kitaifanya biashara yako ife.

  1. Jua kila fedha ya biashara yako ilipo.

Kwa wakati wowote kwenye biashara yako, unapaswa kujua kila fedha ilipo, unapaswa kudhibiti mzunguko wa fedha kwenye biashara yako kwa kujua fedha zipo wapi na kwa wakati gani. Jua kama fedha ipo kwenye mzunguko au kwenye mali.

Pia kuwa na akaunti maalumu ya biashara yako, ambapo unatunza fedha zako za biashara, hii itakusaidia kuweza kuona fedha zipo wapi na hata kukokotoa namba zako za kibiashara. Kuwa na fedha nyingi kwenye biashara kunaweza kukufanya ujisahau na pia kiusalama siyo jambo zuri.

  1. Usishindane kwenye bei, shindana kwenye thamani.

Kitu kinachoua biashara nyingi, licha ya kuonekana kuuza sana ni kushindana kwenye bei. Pale ambapo panakuwa na ushindani, na washindani wako wakapunguza bei, usikimbilie kupunguza bei zaidi yao. Unaweza ukauza sana kwa bei rahisi, lakini faida unayotengeneza ikawa kidogo sana au isiwepo kabisa, hasa kama gharama zako za kuendesha biashara zipo juu.

Wenzako wanapopunguza bei, wewe ongeza thamani zaidi. Na usiogope kwamba biashara yako itakufa kama hutapunguza bei kuliko wengine, wewe lenga wateja wanaojua thamani unayotoa na utaweza kusimama vizuri kibiashara. Lakini kama utakimbilia kupunguza bei, utakuwa umekimbilia kifo cha kibiashara wewe mwenyewe.

  1. Usikopeshe

Kitu kingine kinachoua biashara nyingi ni kukopesha, wafanyabiashara wengi huwa wanajikuta wamekopesha sana kiasi kwamba mtaji mwingi upo nje ya biashara. Na wateja wakishakopa wanaacha kuja kwenye biashara kama hawawezi kulipa.

Kama biashara yako siyo ya ukopeshaji, basi epuka sana kukopesha wateja wako, ni njia rahisi na yenye maumivu kwako ya kuwafukuza kwenye biashara yako.

Watake wateja wako walipe fedha taslimu kabla ya kupata kile unachowauzia, usiogope kuwapoteza kwa sababu hujawakopesha, bali ogopa kuwapoteza baada ya kuwakopesha, maana hicho ndiyo huwa kinatokea pale unapowakopesha watu, wanakukimbia.

Rafiki, zingatia mambo hayo matano kwenye biashara yako, na muhimu zaidi kazana kutoa thamani kubwa na kwa bei ambayo wewe unabaki na faida, kisha kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana kwenye fedha za biashara yako. Kwa kufanyia kazi haya, utaweza kuanzisha na kukuza biashara yako mpaka kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji