Rafiki yangu mpendwa,

Ulimwengu wa biashara siyo lele mama. Biashara zimekuwa na changamoto nyingi mno, hasa katika zama hizia ambazo kila mtu anaweza kufanya kila aina ya biashara anayotaka kufanya.

Sasa hivi kuingia kwenye biashara imekuwa rahisi sana, huhitaji hata kuwa na eneo, mtandao wa intaneti umerahisisha sana ufanyaji wa biashara. Unaweza kuwa na huduma au bidhaa nyumbani kwako, ukatangaza kupitia mtandao wa intaneti na kisha kuwapelekea wateja wape wanapohitaji.

Urahisi huu wa kuingia kwenye biashara, umefanya ushindani uwe mkali sana. Na hili limepelekea wengi wanaoingia kwenye biashara kushindwa kuendelea kwa sababu biashara zao zimekufa.

inline-4-common-mistakes

Tafiti ambazo zimekuwa zinafanywa, zinaonesha kwamba asilimia 80 ya biashara mpya zinazoanzishwa, zinakufa ndani ya mwaka mmoja. Na zile zinazoendelea, ndani ya miaka mitano nusu unakuta zimekufa. Hii ina maana kwamba, kama mwaka huu zitaanzishwa biashara 10, basi baada ya mwaka mmoja nane zitakuwa zimekufa, na baada ya miaka mitano itakuwa umebaki biashara moja pekee.

Kama upo kwenye biashara au unapanga kuingia kwenye biashara, najua hupendi kuwa kwenye kundi ambalo biashara zao zinakufa. Unapenda biashara unayoianzisha ikue zaidi na kukuletea faida kubwa.

Kama hicho ndiyo unachotaka, basi kuna makosa matano unayopaswa kuyaepuka sana, ambayo ndiyo chanzo cha kufa kwa kila aina ya biashara ambayo imewahi kuanzisha na kufa.

SOMA; Sababu Tano (05) Kwa Nini Biashara Nyingi Ndogo Zinakufa Na Jinsi Ya Kuiokoa Biashara Yako Isife.

Makosa haya matano tumeshirikishwa kwenye kitabu kinachoitwa How to Get Rich: One of the World’s Greatest Entrepreneurs Shares His Secrets ambacho kimeandikwa na Felix Dennis. Felix Dennis alikuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa sana katika sekta ya uchapishaji wa majarida. Katika kitabu hiki ametushirikisha mambo aliyojifunza katika kujijengea utajiri, makosa aliyofanya na mambo mazuri aliyoweza kufanya kwenye safari yake.

Katika moja ya sura za kitabu chake, Felix ametushirikisha makosa haya matano yanayoua biashara nyingi, yasome hapa, chukua hatua ili kuweza kuikuza biashara yako na kuweza kufika kwenye utajiri mkubwa.

KOSA LA KWANZA; KUCHANGANYA TAMAA NA MSUKOMO WA NDANI.

Kila mtu anatamani kuwa tajiri, kila mtu anatamani kuwa na biashara hasa pale anapoona wengine wameingia kwenye biashara na kufanikiwa. Kama utachukua hatua kwa sababu umetamani, utashindwa vibaya sana kwenye biashara.

Katika kuanzisha na kufanikiwa kwenye biashara, tamaa peke yake haitoshi, unahitaji kuwa na msukumo mkubwa sana ndani yako. Tamaa huwa zinapita, unaweza kutamani kitu kimoja sasa, baada ya muda ukatamani kitu kingine. Kama utakuwa unasukumwa kwa tamaa, hutaweza kuweka juhudi kwenye biashara na kufanikiwa.

Unahitaji kuwa na msukumo mkubwa sana ndani yako, msukumo ambao hauchoki na wala haukubali kukosa kile ambacho unataka. Msukumo huu utakuwezesha kujituma zaidi, kufanya kazi zaidi na hata kuteseka pale inapobidi ili uweze kupata kile unachotaka.

Safari ya mafanikio kwenye biashara na hata kuelekea kwenye utajiri ni safari ngumu sana, ni safari ambayo itayabadili kabisa maisha yako, ni safari ambayo itavuruga sana mambo ambayo umeyazoa, kuanzia kukunyima muda wa kustarehe mpaka kukukosesha muda wa kukaa na watu wa karibu kwako. Kama huna msukumo mkubwa kutoka ndani yako, safari hii hutaiweza.

Felix anasema hajawahi kukutana na mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa ambaye familia yake na mahusiano yake hayajaharibiwa na mafanikio yake kwa namna moja au nyingine. Changamoto za mahusiano, kukosa muda wa kukaa na familia na kukosekana nyumbani ni matokeo ya kutafuta mafanikio na utajiri.

Felix anasisitiza kama haupo tayari kuona baadhi ya maeneo ya maisha yako yakitetereka wakati unafanyia kazi ukuaji wa biashara yako na utajiri, basi usijaribu kuanza safari hii, maana utaishia njiani na bado itaathiri maeneo mengi ya maisha yako.

Ingia kwenye safari hii ukijua kuna maeneo mengi ya maisha yako ambayo yatavurugwa, lakini kama msukumo ni mkubwa na unatoka kweli ndani yako, utaweza kwenda na maeneo hayo yaliyovunjika kwenye maisha yako.

KOSA LA PILI; KUWA NA MATUMAINI YALIYOPITILIZA KWENYE MZUNGUKO WA FEDHA.

Fedha ndiyo uhai wa biashara, mzunguko wa fedha kwenye biashara ni sawa na mzunguko wa damu kwenye miili yetu, ukisimama hakuna maisha. Mzunguko wa fedha ni eneo muhimu sana kwenye biashara, ambalo kila mfanyabiashara anapaswa kuweka jicho lake. Sahau mambo mengine yote kwenye biashara, lakini siyo mzunguko wa fedha. Toa majukumu mengine yote kwa wasaidizi wako, lakini siyo jukumu la kusimamia mzunguko wa fedha.

Mzunguko wa fedha kwenye biashara unahusisha mapato na matumizi. Mapato yanatokana na mauzo yanayofanyika na matumizi ni gharama zote za mauzo na uendeshaji wa biashara. Kama biashara ina mzunguko wa fedha chanya, yaani mapato na faida ni kubwa kuliko matumizi, biashara hiyo itafanikiwa, hata kama haiendeshwi vizuri. Lakini kama mzunguko wa fedha ni hasi, yaani mapato na faida ni ndogo kuliko matumizi, biashara hiyo itakufa, hata kama inaendeshwa vizuri kiasi gani.

Biashara inayopoteza fedha inakufa, na kila biashara inayokufa, tatizo huanzia kwenye mzunguko wa fedha, unakuta biashara inapoteza fedha lakini mwenye biashara hajui, kwa sababu hasimamii vizuri mzunguko wa fedha. Wengi wanakuwa na matumaini kwamba mambo yanaenda vizuri, hasa pale wanapoona mauzo ni makubwa. Lakini hawapigi hesabu na kuona kama mauzo hayo makubwa yanaleta faida ya kutosha kujiendesha kwa biashara.

Felix anasema unapaswa kuweka jicho lako kwenye mzunguko wa fedha wa biashara yako, ujue kila senti ya biashara yako iko wapi, ujue kila wakati kama biashara inaingiza fedha au kupoteza fedha na pia uweze kuchukua hatua haraka pale unapogundua biashara inapoteza fedha. Biashara nyingi huwa zinaanza kupoteza fedha kidogo kidogo, wafanyabiashara wanakuwa hawajui au wanapuuza, inafika hatua fedha zinazopotea ni nyingi na biashara haiwezi kupona tena.

Usikubali biashara yako ifike huko, kama unataka biashara yako ikue na upate mafanikio, mzunguko wa fedha ndiyo eneo ambalo jicho lako linapaswa kuwepo muda wote. Usimwamini mtu mwingine yeyote kwenye eneo hilo.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuzuia Upotevu Wa Fedha Kwenye Biashara Yako Na Kuweza Kuiona Faida.

KOSA LA TATU; KUNG’ANG’ANA KWENYE KUSHINDWA.

Wote tumekuwa tunajifunza kauli muhimu sana kwenye mafanikio, kuwa ving’ang’anizi na wavumilivu, kutokukubali kushindwa na kujaribu tena na tena na tena. Na wengi tunafanyia kazi kauli hizi bila ya kujitafakari kwa kina na badala ya kupiga hatua, tunajichimbia shimo zaidi.

Felix anasema biashara zote ambazo zimeshindwa, ukiangalia kwa ndani utaona kuna makosa ambayo yamekuwa yanarudiwa kwa muda mrefu ambayo yanakuwa yameifikisha biashara eneo ambalo haiwezi kurudi tena kwenye ukawaida.

Mfanyabiashara anakuwa na wazo fulani la kuboresha au kukuza biashara yake, analipenda sana wazo hilo na kuliamini, na hivyo analifanyia kazi. Lakini anapochukua hatua, wazo hilo linaleta hasara badala ya faida. Sasa kwa sababu mfanyabiashara anapenda sana wazo lake, anaona hasara ni mwanzo tu, hivyo anaendelea tena kujaribu. Wengi hujaribu hivi na kuendelea kupata hasara kwa muda mrefu mpaka wanapokuja kustuka biashara imekufa.

Felix anatuambia tunapaswa kuepuka sana kuweka hisia kwenye mawazo au mikakati ya biashara tunayoifanyia kazi, kwa sababu tukishaweka hisia, tunashindwa kufikiri kwa usahihi na kuona uhalisia na hivyo kurudia makosa ambayo yanatugharimu.

Hakuna ubaya wowote kwenye kuacha kitu ambacho hakileti faida, hivyo tunapaswa kuwa tayari kuacha mawazo au mikakati ambayo inaleta hasara kwenye biashara yako.

Unapokuwa na wazo jipya au mkakati mpya unaotaka kufanyia kazi kwenye biashara yako, jiwekee ukomo kabla hujaanza kufanyia kazi. Jiwekee ukomo wa muda na fedha ambazo upo tayari kupoteza katika kujaribu wazo au mkakati huo. Kiasi hicho ulichotenga kinapoisha, usiweke tena kiasi kingine, kubali hasara hiyo ndogo na songa mbele. Hapo kwenye kukubali hasara ndiyo pagumu, wengi huona kwa kuwa wameshaweka fedha, basi waendelee kuweka ili waokoe zile walizoweka awali. Na hapo ndipo hasara inapokuwa kubwa zaidi na zaidi.

Kubali hasara ndogo na songa mbele, kushindwa kukubali hasara ndogo itakuwa ni kuchimbia biashara yako kaburi.

KOSA LA NNE; KUFIKIRI KIDOGO NA KUCHUKUA HATUA KUBWA.

Tumekuwa tunaona biashara nyingi zinaanza zikiwa ndogo, na zinafanya vizuri sana wakati zikiwa ndogo. Kwa kuwa zinafanya vizuri kwenye udogo wake, mfanyabiashara, labda kwa kujishauri mwenyewe au kushauriwa na wengine anaona anaweza kukuza zaidi biashara hiyo. Na hapo ndipo matatizo ya kila aina yanapoibuka kwenye biashara hiyo.

Biashara nyingi zimekuwa zinakufa pale wamiliki wanapoanza kuzikuza zaidi. Na tatizo ni moja, wanakuwa wanataka kufanya makubwa na biashara zao, huku wakiwa wanafikiri kidogo. Kwa mafanikio madogo waliyopata, wanaona wanaweza kufanya chochote wanachotaka kufanya, na hapo wanaanza kufanya mambo makubwa kuliko uwezo wa biashara zao na biashara zinakufa.

Biashara nyingi kubwa pia zimekuwa zinaingia kwenye makosa haya, biashara inapokuwa inaanza watu wanajituma sana, wanajifunza na kujaribu mambo mapya kila wakati. Wanadhibiti sana matumizi ya biashara na kila senti inafuatiliwa kwa umakini mkubwa. Nguvu hiyo kubwa inawawezesha kukua sana. Lakini biashara inapopata mafanikio, watu wanazoea, wanaanza kuendesha biashara zao kwa mazoea, wanaanza kuingia gharama kubwa kwenye vitu ambavyo siyo vya msingi, na wafanyabiashara wanawaachia watu wengine jukumu la kudhibiti mzunguko wa fedha. Na hapo majanga ya kila aina huanza kuitembelea biashara hiyo.

Felix anatushirikisha makosa ambayo amewahi kuyafanya kwenye biashara, kwa kujiona ameshafanikiwa sana na kuanza kuendekeza starehe na kusahau biashara, kitu ambacho siyo tu kiliathiri biashara zake, bali pia kiliathiri afya yake.

Unapaswa kufikiri makubwa na kuchukua hatua kidogo. Kuwa na maono makubwa sana ya biashara yako, ione biashara yako ikiwa kubwa na kuwafikia wengi, ikikuingizia faida kubwa na kukufanya wewe kuwa tajiri mkubwa sana. Lakini kila wakati chukua hatua kama vile ndiyo unaanza biashara, weka umakini wako kwenye kila kitu, dhibiti sana matumizi na gharama za kuendesha biashara, jua kila senti ya biashara yako ilipo.

Kwenye biashara usijikweze kuliko uwezo wako, na pia itakusaidia sana kama utabaki na maisha yako ya kawaida hata kama umefanikiwa sana kwenye biashara, hilo litakupunguzia matatizo na changamoto ambazo wengi wanakaribisha kwenye biashara zao pale wanapobadili maisha yao ghafla baada ya kufanikiwa kwenye biashara.

Kila siku endesha biashara yako kama ndiyo siku ya kwanza kwako, na kila siku utaweza kuikuza biashara yako na kufanikiwa zaidi.

KOSA LA TANO; KUPUUZA VIPAJI.

Felix anasema kama unataka biashara yako ifanikiwe na uwe tajiri mkubwa, kuna kipaji kimoja muhimu unapaswa kuwa nacho. Kipaji hicho ni uwezo wa kutambua, kuajiri na kuwakuza watu wenye vipaji. Kwa kifupi unahitaji watu wenye vipaji katika kukuza biashara yako.

Biashara yako haiwezi kukua kuzidi wale ambao wanafanya kazi kwenye biashara hiyo. Hivyo kama unaajiri watu wa kawaida, ambao hawajui wanaenda wapi na maisha yao, jua biashara yako itakuwa ya kawaida na haitakuwa na mwelekeo. Unapaswa kuweka juhudi kubwa katika kuajiri watu wenye vipaji, ambao wataiwezesha biashara yako kukua zaidi.

Kuajiri watu wenye vipaji na uwezo mkubwa kutakugharimu lakini ni uwekezaji muhimu kufanya kwenye biashara yako. Kama unaepuka kuwalipa watu vizuri na hivyo kuajiri watu wa kawaida, jua pia kipato cha biashara yako kitakuwa cha kawaida. Lakini kama utaajiri watu wenye uwezo na vipaji, na ukawalipa zaidi, jua biashara yako itakuwa na kipato kikubwa.

Felix anahitimisha kwa kusema, mtu yeyote anayetaka kuwa tajiri, hawezi kufanya hivyo bila ya vipaji, iwe kipaji chake mwenyewe au cha wengine. Kipaji ni lazima na hakikwepeki katika kukuza biashara.

Kanuni ambayo Felix anatupa kwenye upande wa kipaji ni kutambua watu wenye vipaji, kuwaajiri, kuwakuza, kuwatuza vizuri na kuwalinda wasichukuliwe na wengine. Anatuambia washindani wako wakijua una watu wenye vipaji, watajaribu kuwalaghai na kuwachukua, hivyo unapaswa kuwa makini na kuhakikisha huibiwi vipaji vyako, hata kama itabidi kuwalipa zaidi au kuwapa nafasi zaidi.

Felix anatupa mfano huu, mapiramidi ya Misri, moja ya maajabu saba ya dunia, ni kitu ambacho Mafarao wa Misri wanasifiwa nacho sana. lakini hakuna Farao aliyejenga piramidi kwa mikono yake, badala yake walitambua vipaji vya wengine na kuvitumia kujenga mapiramidi hayo. Kadhalika kwenye ukuaji wa biashara yako, unahitaji zaidi vipaji vya wengine kuliko kipaji chako. Kazana kupata watu wenye vipaji ambao utawaweka kwenye uendeshaji wa biashara yako na utabaki kusimamia yale muhimu kama mzunguko wa fedha na maono makubwa ya ukuaji zaidi wa biashara yako.

Rafiki, hayo ndiyo makosa matano ambayo yanaua kila aina ya biashara, nina imani umeyaelewa kwa kina na unakwenda kuyaepuka kwenye biashara yako ili iweze kukua na uweze kufikia utajiri mkubwa kama ambavyo Felix Dennis ametushirikisha.

Katika juma hilila 16 la mwaka huu 2019 tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu hiki cha HOW TO GET RICH, ni kitabu ambacho mtu mwenye uzoefu wa kuanzia chini mpaka kufika utajiri anaushirikisha yale aliyojifunza kwenye safari yake. Kwenye kitabu hiki anatushirikisha kila kitu kuanzia wazo, kupata mtaji, mchango wa bahati, misingi ya utajiri na mengine mengi.

Kuhakikisha hukosi uchambuzi wa kina wa kitabu hiki, pamoja na mafunzo ya ziada (#MAKINIKIA) jiunge na CHANNEL YA TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram. Kama bado hujajiunga, tuma ujumbe sasa kwa app ya telegram kwenda namba 0717396253 ujumbe uwe na maneno TANO ZA JUMA na utaunganishwa kwenye channel hii. Karibu sana tujifunze kwa kina kupitia usomaji wa vitabu.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT