#TANO ZA JUMA #16 2019; Usione Aibu Kwenye Utajiri, Siri Za Kufikia Utajiri Kutoka Kwa Mtu Tajiri, Makosa Matano Yanayoua Biashara Nyingi, Misingi Mitano Ya Utajiri Na Kama Unaweza Kuhesabu Fedha Zako Hujawa Tajiri.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye tano za juma la 16 la mwaka huu 2019, naamini limekuwa juma bora sana kwako, juma la kujifunza na kuchukua hatua ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Hongera sana kwa kila ulichojifunza na kufanyia kazi juma hili.

Kwenye tano za juma hili, tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa How to Get Rich: One of the World’s Greatest Entrepreneurs Shares His Secrets ambacho kimeandikwa na Felix Dennis. Felix Dennis alikuwa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa sana katika sekta ya uchapishaji wa majarida.

libro-how-to-get-rich-de-felix-dennis

Felix alianzia chini kabisa, bila ya elimu kubwa wala mtaji, lakini aliweza kuingia kwenye biashara ya uchapishaji wa majarida na kuweza kuwa tajiri mkubwa sana nchini Uingereza. Katika kitabu hiki, Felix anatushirikisha safari ya mafanikio yake, makosa aliyofanya, bahati alizopata na ushauri muhimu kwa wote ambao wanataka kupata utajiri kwenye maisha yao, ambapo najua wewe ni mmoja wao.

Felix anasema vitabu hivi vya jinsi ya kuwa tajiri vimekuwa vinadharaulika na wengi kwa sababu wanaoviandika huwa siyo watu matajiri. Lakini yeye aliandika kitabu hiki kama tajiri, akishirikisha yale aliyofanya mpaka kufikia utajiri huo. Hivyo kinakuwa ni kitabu cha tofauti sana na vitabu vingine vinavyohusu utajiri. Kwenye kitabu hiki Felix hajaficha chochote, ametueleza mpaka uvunjaji wa sheria ambao amewahi kufanya ili kupata fedha, kadhalika ametuonesha jinsi kupata fedha nyingi kulivyoharibu maisha yake, akageuka kuwa mtu wa pombe na wanawake wengi kiasi cha kuhatarisha afya yake. Ni vitabu vichache sana vinavyohusu utajiri vitakavyokufunulia mambo kama haya, na ndiyo maana nimeona ni kitabu muhimu mno kwetu kujifunza, siyo tu kwa jinsi ya kupata utajiri, lakini pia makosa ya kuepuka pale tunapokuwa tumeupata utajiri.

Baada ya utangulizi huu, sasa tuzame kwenye tano za juma, tujifunze kwa kina jinsi ya kupata utajiri na makosa ya kuepuka kwenye safari hii.

#1 NENO LA JUMA; USIONE AIBU KWENYE UTAJIRI.

Kumekuwa na unafiki mkubwa kwenye jamii zetu inapokuja kwenye utajiri, wengi hawapendi kuona wengine wakizungumzia utajiri waziwazi, au kusema hadharani wanataka kuwa matajiri. Wanaosema hivyo wanaonekana ni watu wenye tamaa na wasiojali wengine.

Felix anatupa kisa kimoja, ambapo akiwa mtu mzima alishiriki msiba wa rafiki yake, na katika msiba huo alikutana na mama wa aliyekuwa rafiki yake wa kike enzi za ujana. Walitaka kuwa wachumba lakini wazazi wa binti wakamkataza binti yao asichumbiwe na Felix. Basi katika msiba huo mama yule akamwambia hatimaye umepata ulichokuwa unataka siyo? Akamuuliza nini? Mama akamjibu, akamjibu utajiri, ulikuwa unanitisha sana ulipokuwa kijana, hukuwa kama vijana wengine. Wakati tunakuuliza unataka kuwa nani kwenye maisha, hukujibu kama vijana wengine kwamba unataka kuwa daktari, mhasibu, mwanasheria na kadhalika, wewe ulijibu unataka kuwa tajiri, tena ukiwa unajiamini sana, kwa kweli hilo lilitutisha.

Felix anasema tukio hilo lilimkumbusha mbali sana kuhusu kiu yake ya kupata utajiri tangu akiwa kijana mdogo, ambayo haikukauka mpaka alipopata utajiri.

Hivi ndivyo tunavyopaswa kuwa kwenye maisha yetu, tusiuonee aibu utajiri, tusijionee aibu wenyewe na wala tusimwonee aibu mtu yeyote yule. Kama tunataka utajiri tujiambie wenyewe na tuseme wazi kabisa kwamba tunataka utajiri. Wengi hawatapendezwa na maamuzi yetu, lakini kumbuka, huishi kwa ajili ya yeyote yule, bali unaishi kwa ajili yako mwenyewe.

Jiambie leo unataka kuwa tajiri, jikumbushe kila siku unataka kuwa tajiri, na hata kama umeshapiga hatua kifedha, bado kuna hatua zaidi unazoweza kupiga. Kama ambavyo utajifunza kwenye tafakari ya kufikirisha, kama unasoma hapa, bado una hatua kubwa sana hujapiga kwenye utajiri. Hivyo endelea kujikumbusha kila siku na endelea kujifunza na kuchukua hatua ili kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Kwenye maisha yangu nina malengo makubwa mawili ambayo nayafanyia kazi kila siku bila ya kukata tamaa, lengo la kwanza ni kuwa bilionea kufikia mwaka 2028 na lengo la pili ni kuwa raisi wa Tanzania mwaka 2040. Malengo haya mawili nitayapigania kila siku ya maisha yangu, na hakuna kitakachonirudisha nyuma, kama nipo hai ni siku nyingine ya mapambano.

Nakusihi na wewe rafiki yangu uwe na malengo makubwa ya aina hii, hasa kwa upande wa fedha, na usiache kujikumbusha kila siku malengo hayo, tena kwa kuyaandika, na kuyafanyia tahajudi, kujiona tayari umeshayafikia, na uwezo mkubwa wa akili yako utahakikisha unayafikia malengo hayo.

Usione aibu kwenye utajiri, sema wazi unataka kuwa tajiri na wapuuze wale wanaokuona una tamaa. Kumbuka, watu ambao hawataki kutajirika au hawajiamini kwamba wanaweza kutajirika ndiyo watu wa kwanza kuwakatisha tamaa wale ambao wanataka kutajirika. Hivyo njia ya kuwajua haraka ni kutangaza nia yako ya kutaka utajiri na ukiona yeyote anakukatisha tamaa kwenye hilo mwondoe kabisa kwenye maisha yako.

#2 KITABU CHA JUMA; SIRI ZA KUFIKIA UTAJIRI KUTOKA KWA MTU TAJIRI.

Rafiki, kama nilivyokueleza kwenye utangulizi, kitabu chetu cha juma ni HOW TO GET RICH, kitabu ambacho kiliandikwa na Felix Dennis akitushirikisha safari yake ya kutoka sifuri mpaka utajiri mkubwa.

Yafuatayo ni mambo muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi kutoka kwenye kitabu hiki, ili kila anayetaka kuwa tajiri, aweze kuwa tajiri bila ya kizuizi chochote.

MAKUNDI MATATU YA WATU WALIOKWAMA KATIKA SAFARI YA UTAJIRI NA JINSI YA KUJIKWAMUA.

Felix anatuambia katika safari ya kuelekea kwenye utajiri kuna makundi matatu ya watu waliokwama, na pia ametushirikisha njia za kila kundi kujikwamua.

Kundi la kwanza ni la vijana ambao hawana pa kuanzia, hivyo hawana uzoefu na wala hawana mtaji. Hawa husingizia ukosefu wa mtaji na uzoefu kama kikwazo kwao. Lakini Felix anasema hakuna kundi lenye faida ya kufikia utajiri kama hili. Kwa sababu kundi hili halina cha kupoteza, kama huna chochote, maana huwezi kupoteza chochote na hivyo unaweza kujaribu chochote. Kama upo kwenye kundi hili, Felix anakuambia ni wakati wa kuanza kujishughulisha na chochote unachochagua, kujifunza sana, kuweka juhudi kubwa na utafanikiwa. Kundi hili lina faida ya kuwa na muda na nguvu ya kufanya kazi kwa muda mrefu, hivyo linapaswa kutumia faida hiyo ambayo wengine hawana, kujituma sana kwenye chochote wanachofanya, usiku na mchana ili kujijengea msingi wa utajiri.

Kundi la pili ni wale ambao wapo vizuri kidogo, hawa ni wale ambao wana ajira ambayo inawapa kipato cha kutosha kuendesha maisha yao, lakini haiwapi utajiri. Kundi hili huwa wanakuwa na hofu ya kuondoka kwenye ajira na kupoteza kipato cha uhakika. Pia ukosefu wa mtaji ni sababu inayotumiwa zaidi na kundi hili. Felix anashauri waliopo kwenye kundi hili kuanza kuchukua hatua za kujijengea utajiri, kuchukulia ajira waliyonayo kama ngazi ya kufika kule wanakotaka kufika na siyo kuiona kama ndiyo mwisho wa safari.

Kundi la tatu ni wale ambao wameshapanda vyeo kwenye ajira zao, wameshafikia ngazi za umeneja au ubosi kupitia kazi zao. Hivyo kipato kinakuwa kikubwa pamoja na marupurupu mbalimbali. Hawa ndiyo wanakuwa wameingia kwenye shimo refu zaidi, maisha yanakuwa mazuri kwa kuweza kupata kila wanachotaka, lakini utajiri hauwezekani kwa njia hiyo. Hawa wanakuwa wamekwama zaidi kwa sababu kazi zinakuwa zinawachukulia muda wao mwingi, na wakisema waondoke siyo tu watajiumiza wao wenyewe, bali pia watawaumiza watu wa karibu yao, ambao wameshazoea maisha mazuri yanayoletwa na kazi ambayo mtu anayo. Kwa kundi hili, Felix anashauri mtu aliye kwenye kundi hili kujijengea ujasiri wa kuchukua hatua ya kuelekea kwenye utajiri. Kwa sababu wengi kwenye kundi hili kinachowarudisha nyuma ni hofu ya kupoteza vile ambavyo wanavyo kwa sasa. Lakini kama ni uwezo na uzoefu wanao mkubwa, kama wakiwa na ujasiri na wakiacha kuwasikiliza wale wanaowataka wabaki pale walipo basi wanaweza kupiga hatua zaidi.

SABABU MBILI KUBWA ZINAZOWEZA KUKUZUIA USIFIKIE UTAJIRI MKUBWA.

Felix anatuambia ukichukua idadi ya matajiri na kulinganisha na idadi ya watu, inakuja wastani wa tajiri mmoja kwa kila watu milioni moja. Hii ina maana nafasi ya wewe kuwa tajiri mkubwa ni moja kati ya milioni moja, hii ni nafasi ndogo sana kuliko hata ya ushindi kwenye kamari.

Lakini anasema ukiondoa watoto sana na wazee sana, kisha ukaondoa wafanyakazi wa umma ambao wameshachagua hayo ndiyo maisha yao, kisha ukaondoa wavivu ambao hawataki kujituma, unakuta nafasi yako inapanda zaidi, inakuwa moja kati ya elfu moja. Hivyo kama utajituma, kama utachagua kuwa tofauti na watu wengine walivyo, nafasi yako ya kufikia utajiri inaongezeka zaidi.

Kuna sababu mbili kubwa zinazoweza kumzuia mtu asifikie utajiri ambazo Felix ameziainisha kwenye kitabu;

Sababu ya kwanza ni afya, kama afya yako ni mbovu hutaweza kuhimili mikiki mikiki ya kuelekea kwenye utajiri. Unapokuwa na afya mbovu, kipaumbele chako cha kwanza ni afya, mengine hayapati nafasi. Na pia matatizo ya afya yana gharama kubwa sana. Hivyo linda sana afya yako.

Sababu ya pili ni umri, kwa wale ambao umri umeenda sana, kuianza safari ya utajiri na uhitaji wake wa kuweka juhudi kubwa, hawataweza. Hivyo unapaswa kuianza safari hii mapema uwezavyo, ili uweze kuijenga misingi ukiwa bado una nguvu za kupambana.

Ukiondoa sababu hizo mbili, hakuna kingine kinachoweza kumzuia mtu, siyo rangi, dini, kabisa, jinsia, malezi au chochote kile kinaweza kukuzuia. Hivyo kama kuna sababu unaitumia kwa nini huwezi kuwa tajiri, ambayo haihusishi afya au umri mkubwa sana, basi jua unajidanganya.

ISHINDE HOFU YA KUSHINDWA.

Kazi kubwa uliyonayo kwenye safari yako ya kuelekea kwenye utajiri ni kuishinda hofu ya kushindwa. Hiki ndiyo kikwazo kikubwa cha ndani yako, ambacho kama hutakivua, hutaweza kujaribu mambo makubwa.

Hakuna mtu ambaye hana hofu kabisa, kila mtu anakutana na hofu mbalimbali, lakini kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni jinsi wanavyozikabili hofu zao.

Wanaoshindwa wanachukua hofu kama kikwazo, na kwa kuwa hawataki kuonekana wakishindwa au hawataki lawama, basi hawachukui hatua.

Wanaoshinda wanaiona hofu kama mrejesho kwamba wanajaribu kitu kikubwa, hivyo wanachukua hatua na hofu hiyo inapotea.

UFANYE NINI?

Kutaka utajiri ni ndoto ya kila mtu, lakini njia ya kufika kwenye utajiri ndiyo inakuwa kikwazo kwa wengi. Wengi wanakwama kwenye kujiuliza ni kazi au biashara gani wafanye ambayo itawafikisha kwenye utajiri.

Kabla ya kupata jibu ni nini ufanye, Felix anasema ajira ya aina yoyote ile haiwezi kukuletea utajiri, na hata utaalamu uliosomea, hautakuletea utajiri. Hivyo anasema kama kusudi lako kwenye maisha ni kuwahudumia watu, kupitia taaluma uliyonayo basi pokea njia hiyo na kubali kwamba hutakuwa tajiri. Kwa kuwa mwalimu, daktari, mhasibu, mwanasheria na taaluma nyingine, utatoa msaada mkubwa kwa watu kupitia taaluma yako, lakini hutakuwa tajiri.

Hivyo basi, kwa wale ambao wanautaka utajiri, lazima waingie kwenye biashara. Na hapa ndipo linakuja swali la biashara gani mtu afanye.

Felix anasema katika kutafuta ufanye biashara ya aina gani ili kufanikiwa, unapaswa kuangalia vigezo hivi vitatu;

Moja; mapenzi. Ni kitu gani unachopenda kufanya au kufuatilia, hapo ndipo penye hazina yako kubwa. Utafanikiwa zaidi utakapojihusisha na biashara inayoendana na vile vitu unavyovipenda, kwa sababu utajituma zaidi kuliko anayefanya kwa kupata fedha pekee. Angalia ni vitu gani unavyopenda sana kufanya, ambavyo utakuwa tayari kufanya hata kama hakuna anayekulipa, kisha ona ni namna gani watu wanaweza kukulipa ka kufanya vitu hivyo.

Mbili; kipaji. Kila mmoja wetu ana kipaji na uwezo wa tofauti na wa kipekee uliopo ndani yake. Ukijua kipaji ulichonacho, ukaweza kujihusisha na biashara inayoendana na kipaji hicho, utaweza kupiga hatua sana. Kazi kwako itakuwa rahisi kuliko kwa wale ambao hawana kipaji kama chako. Angalia vipaji ulivyonavyo na jinsi unavyoweza kuvitumia kibiashara kufanikiwa zaidi. Hata kuona vipaji vya wengine inaweza kuwa ndiyo kipaji chako, na ukawatumia hao kupiga hatua zaidi.

Tatu; hatima. Kuna imani ambazo watu tunazo kwamba kila mtu ana hatima yake, kwamba kila mtu kuna kitu ameletwa hapa duniani kukifanya. Mtu anapojua kitu hiki na kuanza kukifanya, anakuwa kwenye nafasi ya kufanikiwa kuliko akifanya kitu kingine. Wapo watu waliofanikiwa sana, ambao awali walijaribu vitu vingi, ila hawakufanikiwa, lakini baada ya kujua hatima yao na kuifuata, mambo yakabadilika sana. Jua hatima ya maisha yako, kulingana na imani yako na chukua hatua kuelekea kwenye utajiri.

KOSA LA WAZO BORA.

Wapo watu ambao wamekwama kufikia utajiri kwa sababu wanasubiri mpaka wapate wazo bora, wazo la kipekee ambalo hakuna mwingine analo. Hili ni kosa kubwa ambalo hupaswi kuruhusu litokee kwako.

Wazo ni sehemu ndogo sana ya mafanikio, kama ni kwa asilimia basi tunaweza kusema ni asilimia moja, asilimia 99 ipo kwenye juhudi ambazo mtu anaweka ili kufanikiwa.

Usisubiri mpaka upate wazo bora, anza na wazo lolote ulilonalo kisha nenda ukiliboresha kadiri unavyokwenda. Utafanikiwa zaidi kwa njia hiyo.

KAMWE USIKATE TAMAA.

Kwa kujifunza na kuwaangalia wengine waliofanikiwa, utapata hamasa sana ya kuchukua hatua. Utakwenda kuchukua hatua, na hapo utakutana na vikwazo ambavyo hukutegemea kabisa kukutana navyo. Na hapa ndipo unapoanza kujishawishi kwamba haiwezekani. Na kuona wale ambao wamefanikiwa mambo yalikuwa rahisi kwao.

Rafiki, iko hivi, yeyote unayemwona amefanikiwa, jua amepitia magumu mengi mno. Jua kuna wakati amekutana na changamoto kubwa zinazokatisha tamaa. Lakini amefika pale alipo sasa kwa sababu alikataa kukata tamaa.

Hivyo jiwekee agano leo, kwamba kamwe kamwe hutakata tamaa kwenye safari yako ya kuelekea kwenye utajiri. Hata ukutane na ugumu kiasi gani, utaendelea na safari mpaka ufanikiwe. Jiwekee agano kwamba utafikia utajiri au utakufa ukiwa unautafuta, hakuna njia nyingine tofauti na hiyo.

Kadiri unavyojitoa kufikia utajiri, na kama hutakata tamaa, dunia itakuachia upate kile unachotaka.

MANENO MACHACHE KUHUSU BAHATI.

Felix anatuambia ni kweli kwamba watu waliofanikiwa wana bahati kuliko wale ambao hawajafanikiwa. Lakini kitu tunachopaswa kujua ni hiki, bahati hazikuwafuata vitandani kwao wakiwa wamelala. Bali walikutana na bahati katika mapambano yao.

Hivyo ili ufanikiwe unahitaji kupata bahati, lakini bahati hiyo haitakutafuta wewe, itabidi uitafute wewe. Lazima uweke kazi, lazima ujitume sana, na katika kujituma kwako ndiyo utakutana na fursa ambazo wengine hawawezi kuzitumia kwa sababu hawana maandalizi kama uliyonayo wewe.

Hivyo tunajumuisha kwa kusema, bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fikra. Kama unataka bahati zaidi, hakikisha unakuwa na maandalizi bora zaidi.

UMILIKI, UMILIKI, UMILIKI.

Felix anasema huwezi kuwa tajiri kama huna umiliki mkubwa wa kile anachofanya. Na anasisitiza, biashara yako kuu unapaswa kuwa na umiliki wa silimia 100. Anasema usitoe hisa zako kwa mtu yeyote yule, kwa sababu kadiri unavyoweka kazi na biashara yako kukua, utaishia kuwanufaisha wengine, ambao hawajaweka kazi kama uliyoweka wewe awali.

Felix anasisitiza kwamba kama unataka kuwa tajiri mkubwa, umiliki siyo tu ni muhimu, bali ndiyo kitu pekee unachohitaji. Usidanganyike na ukagawa hisa za biashara yako kuu kwa watu wengine.

Felix anasema unapomiliki biashara yako kwa asilimia 100 unakuwa huru kufanya maamuzi yoyote unayotaka wewe bila ya kusubiri ruhusa ya wengine. Unakuwa na udhibiti mkubwa ambao unakuwezesha kufanya makubwa na kuondoa mlolongo mrefu kwenye kufikia maamuzi.

Lakini pia anatuambia tunapopata fursa za kushirikiana na wengine, kwa biashara nyingine basi tufanye hivyo. Lakini kwa ile biashara yako kuu, ile ambayo umeweka maisha yako yote pale, imiliki kwa asilimia 100. Unapoanza kuongeza vyanzo vyako vya kipato, hasa kwenye maeneo ambayo wewe huna uzoefu mkubwa, shirikiana na wenye uzoefu maeneo hayo na kazana upate umiliki mkubwa kwenye ushirikiano huo.

KUGATUA MAJUKUMU YAKO.

Kikwazo kingine kwa wengi kwenye safari ya kuelekea utajiri mkubwa ni kutaka kufanya kila kitu mwenyewe. Wengi kwa kuwa wanakuwa vizuri kwenye ile biashara wanayofanya, basi biashara inawategemea wao kwa kila kitu. Wasipokuwepo basi biashara haiwezi kwenda vizuri. Felix anasema huko ni kujijengea umasikini.

Kama unataka utajiri wa kweli, lazima ufike mahali ambapo unaweza kuondoka kwenye biashara yako kwa miezi mingi, na ukarudi ukakuta biashara inaenda vizuri. Utaweza kufikia hatua hii kwa kugatua majukumu yako, kwa kutengeneza mifumo mizuri kwenye biashara yako, kisha kuajiri watu wenye vipaji na kuwaamini katika utekelezaji wa majukumu yao. Unachofanya wewe ni kuwapima kwa utekelezaji wa majukumu yao, na unapogundua mtu ni mzigo basi unamwondoa mara moja kwenye biashara yako.

Kama biashara inakutegemea wewe kwa kila kitu huna biashara bali una ajira yako mwenyewe, ambayo inakuwa ngumu kuliko ajira ya wengine. Jifunze kugatua majukumu yako, weka mifumo kwenye biashara yako, na ajiri watu wenye uwezo wakusaidie kukuza biashara yako.

NGUVU YA UMAKINI.

Felix anasema umechagua kupata utajiri kwenye maisha yako, basi achana na vitu vingine vyote na peleka umakini wako kwenye lengo lako kuu ambalo ni kufikia utajiri. Hivyo usifanye chochote kile ambacho hakikufikishi kwenye utajiri.

Felix anatuasa tusije kuingia kwenye mashindano na wengine, kutaka kuwa namba moja kwenye kile tunachofanya au kuwazidi wengine. Ukianza kuhangaika na hayo unakuwa umepoteza lengo na hutalifikia. Lengo lako kuu ni moja, kufikia utajiri ambao umejiwekea (zaidi ya dola bilioni 2) mengine yote hayana nafasi kwako, wengine wanafanya nini au wamepata nini hayakuhusu.

Katika kufikia lengo lako la utajiri, Felix anasema uzingatie sana kutengeneza vitu hivi viwili;

Cha kwanza ni mazingira mazuri kwenye biashara yako, iwe sehemu ambayo watu wanaweza kufanya kazi vizuri na kushirikiana.

Cha pili ni kufanya kazi ambayo ni bora sana, kazi ambayo ni ya viango vya juu sana, usijihusishe na chochote ambacho siyo bora.

Mara zote kumbuka lengo lako kuu ni kufikia utajiri, hivyo usijihusishe na chochote ambacho hakikufikishi kwenye lengo.

UKWELI KUHUSU UTAJIRI.

Wengi wanapoingia kwenye safari hii ya utajiri, huwa wanaona mambo mazuri tu mbele, kwamba wakishapata utajiri maisha yatakuwa mazuri na watakuwa na furaha.

Felix anatupa ukweli kuhusu utajiri, kupitia maisha yake binafsi, ili tuelewe ni kitu gani tunakwenda kukutana nacho mbele, na tujiandae vizuri.

Kwanza kabisa anasema utajiri haujawahi kumletea yeye furaha, zaidi umemletea matatizo makubwa ya kiafya baada ya kujihusisha na ulevi, madawa ya kulevya na uzinzi.

Pili anasema utajiri unakufanya uwe chambo ambapo kila mtu atatumia kila njia kupata fedha zako. Wapo watakaotumia njia za kuomba, wengine kuiba na hata wengine kukushitaki kwa kitu ambacho hujafanya.

Tatu utajiri utaharibu mahusiano mengi uliyonayo. Mahusiano ya ndoa, kwa wengi yanaathirika sana. mahusiano ya kifamilia na kindugu nayo yanaathiriwa sana na safari yako ya utajiri na hata baada ya kufikia utajiri.

Kwa kifupi kadiri unavyokuwa tajiri siyo kwamba matatizo uliyonayo yanaondoka, bali yanakuwa makubwa zaidi. Hivyo jiandae kukabiliana nayo, na kazana kujijengea busara zaidi kadiri unavyoendelea kutajirika. Kwa sababu utajiri bila busara utakuwa ni kujichimbia kaburi lako mapema.

KUNA FEDHA ZINA JINA LAKO.

Felix anatupa kauli moja tunayopaswa kujiambia kila wakati na kuifanyia kazi. Kauli yenyewe ni hii ‘DUNIA IMEJAA FEDHA NYINGI SANA, BAADHI YA FEDHA HIZO ZINA JINA LANGU. KAZI YANGU NI KUKUSANYA FEDHA HIZO’

Hii ni kauli fupi sana, lakini iliyobeba ujumbe mkubwa sana na una nguvu ndani yake. Kwanza dunia haina uhaba, fedha ni nyingi mno. Hivyo unavikiri kwa utele. Pili, baadhi ya fedha hizo zina jina lako, ni zako, hivyo kumbe kuna fedha zimetengwa kwa ajili yako, lakini hazitakufuata hapo ulipo wewe, badala yake lazima utoke ukazikusanye. Jiambie kauli hiyo kila unapoamka na iendee dunia kwa mtazamo huo wa utele na fedha zilizotengwa kwa ajili yako na hakuna kitakachoweza kukukwamisha.

UTAJIRI UNAODUMU NI ULE UNAOTOA KWA WENGINE.

Ipo kauli kwamba hujaishi kama hujawahi kufanya kitu kwa mtu ambaye hawezi kukulipa. Utajiri wa kweli siyo ule unaobaki nao wewe, bali ule unaotoa kwa wengine.

Utakapokufa, hakuna atakayesimulia ulikuwa na majumba mangapi, magari mangapi au mali nyingine ulizomiliki. Bali watu watasimulia ni kwa jinsi gani ulivyogusa maisha yao.

Hivyo baada ya kuwa tajiri, jukumu lako kubwa ni kugawa utajiri wako kwa wengine, na siyo kugawa fedha bure, badala yake kutoa misaada ambayo inafanya maisha ya watu kuwa bora zaidi. Kusaidia kwenye huduma kama za elimu na afya. Kusaidia yatima na wasiojiweza.

Matajiri wote wakubwa wana mifuko yao kwa ajili ya kusaidia jamii, hiki ni kitu ambacho unapaswa kukifanya kama tajiri. Kwa sababu utajiri wako unatokana na jamii na hivyo kuurudisha kwenye jamii hiyo ndiyo njia pekee ya utajiri wako kudumu hata baada ya wewe kuondoka hapa duniani.

MUDA WA KUCHUKUA HATUA NI SASA.

Umejifunza mengi sana kupitia kitabu hiki, umejifunza kuanzia umuhimu wa kuwa tajiri, umuhimu wa kuwa na biashara, aina gani ya biashara ufanye na yale ya kuzingatia ili kufanikiwa kwenye biashara.

Lakini kuna kosa moja utakalolifanya hapa, kosa ambalo litakugharimu sana kwenye maisha yako, kosa ambalo miaka mitano ijayo utakumbuka na litakuumiza sana.

Kosa hilo ni kusema nitaanza kesho, au nitaanza nikiwa tayari. Jua hili rafiki, ni utaanza sasa au hutaanza kabisa, kesho au kuwa tayari ni njia ya kujidanganya tu, hutaki kufanya lakini pia hutaki kukubali kwamba hutaki kufanya.

Chukua hatua sasa, hapo ulipo sasa, unaposoma hapa sasa, au hutachukua hatua kabisa, na utakuja kujilaumu sana baadaye.

HITIMISHO; SIRI NANE ZA KUWA TAJIRI.

Kwa kuhitimisha, Felix ametuorodheshea siri hizi nane za kuwa tajiri.

  1. Jua nini hasa unataka. Tamaa haitoshi. Lazima uwe na msukumo mkubwa kutoka ndani yako.
  2. Achana na watu ambao ni hasi. Kamwe usikate tamaa. Baki kwenye njia yako na usiyumbeyumbe.
  3. Achana na mawazo bora. Kazana na kuchukua hatua kubwa.
  4. Weka jicho lako kwenye mpira ulioandikwa FEDHA ZIKO HAPA, na usihangaike na kitu kingine.
  5. Ajiri watu ambao wana vipaji na uwezo mkubwa kuliko wewe. Gatua majukumu yako. Walipe vizuri uliowaajiri.
  6. Umiliki ndiyo siri kuu ya utajiri. Shikilia kila hisa ya kampuni yako mama.
  7. Uza biashara yako kabla hujafikia kuuza, au pale ambapo umeshaichoka biashara yako. Kuwa na mbinu bora za mapatano katika uuzaji wa biashara.
  8. Usiogope chochote na usimwogope yeyote. Kuwa tajiri. Na kumbuka kugawa utajiri wako kwa wengine.

Rafiki, ni imani yangu kwamba umejifunza kila unachopaswa kujua kuhusu utajiri, kazi ni kwako kuchukua hatua SASA HIVI na siyo kesho au ukiwa tayari. Fanya SASA au hutafanya kabisa.

#3 MAKALA YA JUMA; MAKOSA MATANO YANAYOUA BIASHARA NYINGI.

Rafiki, kama ambavyo nimekuwa nakushirikisha mara kwa mara, huwezi kutajirika kupitia ajira pekee. Ndiyo maana nimekuwa nakusisitiza sana uwe na biashara, hata kama upo kwenye ajira, basi kuwa na biashara ya pembeni, ambayo utaweka juhudi ili kununua uhuru wako.

Kwenye kitabu hiki cha HOW TO GET RICH, Felix anasema mshahara ni kikwazo cha kwanza kuelekea kwenye utajiri. Mshahara una tabia ya kulevya na kuleta uraibu kama ilivyo kwenye madawa ya kulevya. Hivyo kama unapokea mshahara, unapaswa kutengeneza njia mbadala ya kukuingizia kipato ambayo itakupa uhuru mkubwa baadaye. Na hakikisha hukai kwenye mshahara kwa muda mrefu, kwa sababu kadiri unavyozoea mshahara, ndivyo unavyojijengea hofu kubwa ya kuingia kwenye biashara.

Nimekushirikisha mengi sana kuhusu kuanza biashara ukiwa kwenye ajira katika kitabu nilichoandika, BIASHARA NDANI YA AJIRA. Na kitabu hiki kimewasaidia wengi sana kuanzisha biashara zao wakiwa bado wameajiriwa.

Lakini ugumu mkubwa kabisa kwenye biashara haupo kwenye kuanzisha biashara, bali kwenye kuikuza na kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara hiyo. Wengi wamekuwa wanaanza biashara lakini hazidumu, ndani ya muda mfupi biashara zao zinakufa.

Kwenye kitabu cha juma hili, Felix ametushirikisha makosa matano yanayoua biashara nyingi. Yaani kila biashara inayokufa, ukiangalia kwa undani, utakuta moja au zaidi ya makosa haya matano. Hivyo kama unataka kuanzisha biashara yenye mafanikio, na kuizuia isife, basi unapaswa kuyajua makosa hayo matano yanayoua biashara nyingi na kuyaepuka.

Kwenye makala ya juma hili la 16 nilikushirikisha makosa hayo matano yanayoua biashara nyingi. Kama bado hujaisoma makala hiyo, nashauri uache kila unachofanya, isome na chukua hatua mara moja ili kunusuru biashara yako. Isome makala hiyo sasa kwa kufungua hapa; Makosa Haya Matano (05) Pekee Ndiyo Yanayoua Kila Aina Ya Biashara, Yajue Na Yaepuke Ili Biashara Yako Isife. (https://amkamtanzania.com/2019/04/19/makosa-haya-matano-05-pekee-ndiyo-yanayoua-kila-aina-ya-biashara-yajue-na-yaepuke-ili-biashara-yako-isife/)

Pia endelea kutembelea www.amkamtanzania.com na www.kisimachamaarifa.co.tz kila siku ujifunze kupitia makala nzuri zinazowekwa kila siku.

#4 TUONGEE PESA; MISINGI MITANO YA UTAJIRI.

Kila kitu kwenye maisha kina misingi yake, na ukitaka kujua kitu bila kujua misingi yake ni kujidanganya. Nyumba imara inakuwa na msingi imara. Msingi wa nyumba ya kawaida haufanani na msingi wa nyumba ya ghorofa.

Kwenye utajiri pia kuna misingi, misingi ambayo ukiijua na kuiishi kila siku, usipokuwa tajiri basi utakuwa na tatizo kubwa. Yaani ukishaijua misingi hii na kuiishi, usipokuwa tajiri basi kuna namna unajizuia wewe mwenyewe. Ukiishi misingi hii kila siku lazima utafikia utajiri mkubwa, maana misingi hiyo imekuwepo tangu enzi na enzi, na kinachobadilika ni mazingira na teknolojia tu, misingi hii haibadiliki.

Kwa kuwa wewe umeshajitoa kuwa tajiri, kwa kuwa umeshaamua kwamba hakuna cha kukuzuia kufikia utajiri, basi ijue misingi hii na iishi kila siku ya maisha yako.

MSINGI WA KWANZA; UNG’ANG’ANIZI SAHIHI.

Kila kitabu kinachohusu mafanikio kinasisitiza sana ung’ang’anizi na uvumilivu ili kuweza kufanikiwa. Lakini siyo kila ung’ang’anizi na uvumilivu utakufikisha kwenye mafanikio. Bali unahitaji ung’ang’anizi sahihi, na kukubali pale ambapo umekosea ili kuboresha zaidi.

Tunapaswa kuwa ving’ang’anizi ili kupata utajiri na mafanikio, tunapaswa kujaribu tena na tena na tena kila tunaposhindwa. Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba kufanya jambo lile lile kwa njia ile ile halafu kutegemea kupata matokeo tofauti ni maana sahihi ya ujinga.

Tunapaswa kung’ang’ana kwa njia sahihi, tunapaswa kubadili njia tunazotumia, ambacho hatupaswi kubadili ni lengo ambalo tumejiweka. Tunapaswa kuendelea na mapambano mpaka pale tutakapopata tunachotaka.

Wote tunajua jinsi ambavyo dunia ina uangalifu, haikubali kutoa kitu kwa mtu ambaye hajaonesha kweli anakitaka na yupo tayari kulipa gharama kukipata. Jioneshe kwamba wewe unautaka utajiri kweli, kuwa tayari kulipa gharama na ng’ang’ana kwa njia sahihi na utapata unachotaka.

MSINGI WA PILI; KUJIAMINI WEWE MWENYEWE.

Kama hujiamini wewe mwenyewe, hakuna yeyote anayeweza kukuamini na hutaweza kufanikiwa kwenye jambo lolote maishani mwako.

Unapaswa kujiamini wewe mwenyewe, unapaswa kuamini kwamba una uwezo mkubwa ndani yako wa kukuwezesha kupata chochote unachotaka, unapaswa kuamini hakuna kinachoweza kukuzuia kupata kile unachotaka. Tunaambiwa imani inaweza kuihamisha milima, na hii ndiyo imani unayopaswa kuwa nayo ili kufanikiwa na kufikia utajiri.

Katika safari yako ya kusaka utajiri utakutana na vikwazo vya kila aina, utapatwa na hofu nyingi, wapo watakaokukatisha tamaa kwa kukupa mifano ya wengi walioshindwa. Kitu pekee kinachoweza kukuvusha kwenye hali hizo ni kujiamini wewe mwenyewe.

Pia hakuna utakachopanga na kikaenda kama ulivyopanga, utashindwa kwenye mambo mengi licha ya kufanya kila unachopaswa kufanya. Kujiamini ndiyo kutakupa nguvu ya kuamka kila unapoanguka ili uweze kuendelea na safari ya mafanikio.

Jiamini wewe mwenyewe na hakuna kitakachoweza kukuzuia kufanikiwa.

MSINGI WA TATU; AMINI SAUTI YAKO YA NDANI.

Kila mmoja wetu ana sauti iliyopo ndani yake, hisia fulani unazozipata ambazo huwezi kuzielezea, ambazo zinakuashiria kama kitu ni kibaya au kizuri, kama ni sahihi au siyo sahihi. Mara nyingi huwa tunapuuza sauti hii na matokeo yake tunafanya makosa makubwa. Kuna wakati ndani yako unapata msukumo wa kufanya au kutokufanya kitu, lakini ushawishi wa nje unakufanya uende kinyume na sauti hiyo na unakuja kugundua ungejisikiliza ungekuwa sahihi zaidi.

Jifunze kuamini sauti yako ya ndani, hata kama inaendana na uhalisia wa nje. Kuna kitu kwa nje kinaweza kuonekana ni sahihi, lakini sauti yako ya ndani ikakuambia siyo sahihi, au kitu kwa nje kikaonekana siyo sahihi, lakini sauti yako ya ndani ikakuambia ni sahihi. Jifunze kusikiliza sauti yako ya ndani, inajua zaidi kuliko wewe na itakuongoza kwa usahihi mara zote.

Watu wote ambao wamefikia utajiri na mafanikio makubwa, kuna hatua ambazo wamewahi kuzichukua, ambazo watu wa nje waliwaambia wanakosea, lakini wao walifanya, kwa sababu sauti ya ndani iliwaambia ndiyo kitu sahihi kufanya.

Unapojikuta njia panda na hujui hatua ipi sahihi kuchukua, isikilize sauti yako ya ndani, inajua njia sahihi na utaweza kufanya kilicho sahihi.

MSINGI WA NNE; KUWA NA VYANZO VINGI VYA KIPATO.

Chanzo kimoja cha kipato ni utumwa, iwe ni kazi au biashara, huwezi kutajirika kwa kutegemea chanzo kimoja pekee. Angalia matajiri wote wakubwa, hakuna hata mmoja ambaye anategemea chanzo kimoja pekee cha kipato.

Kila biashara huwa ina changamoto zake, hakuna biashara ambayo inafanya vizuri wakati wote, kila biashara kuna kipindi inafanya vizuri na kipindi kingine inafanya vibaya. Unapotegemea biashara moja pekee, kila wakati utakuwa kwenye kupanda au kushuka.

Dawa ya kuondoa hali hiyo ya kupanda na kushuka ni kuwa na vyanzo vingi vya kipato, na ambavyo havitegemeani. Hivyo unapokuwa na changamoto eneo moja, eneo jingine linakuwa linaenda vizuri.

Kanuni hii haiwahusu wale wanaoanza, unapokuwa unaanza, anza na kitu kimoja na kiwekee msingi imara wa kuweza kujiendesha chenyewe. Baada ya kuhakikisha kitu cha kwanza kimekuwa imara, hapo sasa unaweza kuanzisha kitu kingine. Kuanza vitu vingi kwa wakati mmoja ni njia ya uhakika ya kushindwa.

MSINGI WA TANO; SIKILIZA NA JIFUNZE.

Kusikiliza ndiyo silaha yenye nguvu sana katika safari ya mafanikio. Ukiwa msikilizaji mzuri, utajifunza mambo mengi sana kwa watu wengine. Kuanzia wale unaofanya nao kazi na hata wale ambao inabidi upatane nao kwenye makubaliano mbalimbali.

Kusikiliza ni kugumu sana, na wengi hawawezi kusikiliza kwa umakini ndiyo maana hawajifunzi, hawajui watu wanataka nini na kuweza kuwapatia. Ukiwa mtu wa kusikiliza kwa umakini, kwa lengo la kuelewa na kujifunza, utajua mengi na pia utazijua tabia za watu, ambazo utaweza kuzitumia kwa mafanikio zaidi.

Ukiwasikiliza wateja wako utayajua mahitaji yao hata kama hawajakuambia wazi na kuweza kuwatimizia. Ukiwasikiliza wafanyakazi wako utajua kinachowahamasisha na ukiwapatia watajituma zaidi. Ukiwasikiliza unaotaka kufikia nao makubaliano, utajia udhaifu wao uko wapi na kuweza kuutumia.

Katika safari ya mafanikio na utajiri, kusikiliza na kujifunza ni hitaji muhimu sana. Hata watu wanawaheshimu sana wale ambao wanachukua muda na kusikiliza. Tumia nguvu hii kwa manufaa yako na ya wengine pia.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KAMA UNAWEZA KUHESABU FEDHA ZAKO HUJAWA TAJIRI.

“If you can actually count your money, then you’re not a rich man.” – J. Paul Getty

Felix ametumia kauli hii ya aliyekuwa bilionea kupitia uchimbaji wa mafuta, Jean Paul Getty ambaye anasema kama unaweza kuzihesabu fedha zako, basi hujawa tajiri. Na hili lina ukweli mkubwa sana ndani yake.

Felix anasema orodha zinazotolewa na majarida mbalimbali kuhusu utajiri wa watu siyo utajiri halisi, kwa sababu kwa matajiri wa kweli, hawawezi kuwa na uhakika wa kiwango cha utajiri wao. Utajua kiwango chako cha utajiri kwa uhakika kama utauza kila ulichonacho na uwe na fedha zako keshi. Lakini nje ya hapo, yanabaki kuwa makadirio na siyo utajiri halisia.

Na ndiyo maana Felix anamuunga Getty mkono kwamba kama unaweza kuhesabu fedha zako, au kukadiria kwa uhakika utajiri wako, basi bado hujawa tajiri vya kutosha.

Felix ana viwango vyake vya utajiri ambavyo vimekuwa vinawashangaza wengi. Mfano kwenye kitabu hiki cha how to get rich, ametoa madaraja yafuatayo kwenye utajiri;

Wenye utajiri kuanzia dola milioni 2 mpaka dola milioni 4 amewaweka kwenye kundi la masikini ambao wapo vizuri.

Dola milioni 4 mpaka dola milioni 10 ni wapo vizuri, hawapo kwenye umasikini.

Dola milioni 10 mpaka milioni 30 wana uhuru wa kifedha.

Matajiri wa kweli ni kuanzia dola milioni 150 na kuendelea.

Na wenye utajiri wa zaidi ya dola bilioni mbili ndiyo anawaita matajiri wa juu kabisa (super rich).

Hivyo ndivyo viwango vya Felix katika utajiri. Kwa fedha za Tanzania, kwa wakati huu dola milioni moja ni zaidi ya bilioni 2 za kitanzania.

Hivyo pale unapopata fedha zaidi ya wengine na kuanza kujiona umeshamaliza, pale wengine wanapokuambia wewe ni tajiri na hupaswi kujisumbua tena, jikumbushe kauli hii, kama unaweza kuzihesabu fedha zako, hujawa tajiri bado. Na kama utajiri wako uko chini ya dola milioni 4 (au shilingi bilioni 10) basi bado hujatoka kwenye umasikini.

Rafiki, hivi ndizo tano za juma kutoka kwenye kitabu HOW TO GET RICH, naamini umepeta hamasa zaidi na maarifa ya kukufikisha kwenye utajiri. Muhimu ni kuyaweka kwenye matendo, kuchukua hatua ili uyafanye maisha yako kuwa bora zaidi. Na kumbuka, hakuna atakayekupa utajiri, wala hakuna anayeweza kukunyima utajiri ila wewe. Na pia kumbuka anachotuambia Felix, usitafute sababu, kama umechagua kutokuwa tajiri basi endelea na maisha uliyochagua, lakini usilete visingizio. Imani yangu ni umechagua kuwa tajiri na unajituma kila siku kufikia utajiri. Kama ndivyo basi tutakutana kwenye kilele cha utajiri wa hali ya juu sana.

Kwenye #MAKINIKIA, mafunzo ya ziada kutoka kwenye kitabu hiki, tutakwenda kujifunza njia sita za kupata mtaji na moja unayopaswa kuitumia, njia za kuongeza umakini wako kwenye kazi zako, njia bora za kuongeza mapato kwenye biashara na kuwalipa vizuri wafanyakazi wako, pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia ili utajiri unaoupata usipotee.

Mafunzo haya yatapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA, kama bado hujajiunga na channel hii fuata maelekezo yaliyopo hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu