Ukweli kuhusu mafanikio, na ambao nimekuwa natumia muda mwingi kukueleza ni kwamba unaweza kufanikiwa kwenye kitu chochote ambacho umechagua kufanya. Haijalishi ni kitu gani, kama utakifanya kwa misingi ya mafanikio basi utafanikiwa.
Japokuwa kila kitu kinaweza kukupatia mafanikio, bado hutaweza kufanikiwa kama utafanya kila kitu kama ambavyo kila mtu anafanya. Bali kuna namna ya tofauti ya kufanya chochote kile ambacho unataka kufanikiwa.
Zipo sifa kuu mbili za namna ya kufanya kile unachotaka kufanikiwa kwa kukifanya.
Sifa ya kwanza ni uadimu, chochote unachofanya, lazima kiwe adimu sana kupatikana, lazima kiwe nadra kupatikana. Kadiri kitu kinavyokuwa kigumu kupatikana, ndivyo uhitaji wake unakuwa mkubwa na wengi kuwa tayari kulipa gharama ili kukipata. Kama kitu kinapatikana kwa wingi na kwa urahisi, hakuna anayekuwa tayari kulipa gharama kubwa kukipata. Angalia thamani ya dhahabu na chuma, yote ni madini, lakini kinachotofautisha thamani zake kifedha ni ugumu wa kupatikana. Ni vigumu zaidi kupata dhahabu kuliko kupata chuma.
Sifa ya pili ni thamani ya kile unachofanya kwa wanaokitumia, kile unachofanya, kinapaswa kuongeza thamani kwenye maisha ya wengine, kinapaswa kuwa kitu ambacho kinayafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Kadiri unavyotoa thamani zaidi, ndivyo unavyowavutia wengi zaidi na ndivyo unavyofanikiwa zaidi.
Sasa rafiki, sifa hizi mbili zinafanya kazi pamoja, na kadiri zinavyotumiwa kwa pamoja, ndiyo zinavyoleta matokeo makubwa sana. Kama kitu unachofanya kinaongeza thamani kwenye maisha ya wengine, na wakati huo huo siyo rahisi kupatikana kwingine ila kwako tu, kila mtu atahitaji kile ulichonacho, na hapo hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa.
Kama unafanya kile ambacho ni cha thamani na adimu, mambo mazuri sana yatakuja kwako; fursa zitakuwa nyingi na nzuri, utakuwa na uhuru zaidi wa kuchagua nini ufanye na watu watakutegemea na kukutangaza kwa wengine zaidi.
Usipoteze muda wako kuhangaika kufanya kitu kama hakuna sifa hizo mbili, usikimbilie kufanya vitu rahisi na vinavyoonekana kwa nje. Kufanya vitu ambavyo ni adimu na vya thamani, utakutana na ugumu, na wengi huwa hawawezi ugumu huu hivyo hukimbia. Weka nguvu zako kufanya hayo magumu ili uweze kutoa kazi ambayo ni adimu na ya thamani. Mafanikio yako na uhuru wako uko kwenye sifa hizo mbili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,