Hivi ni vitu ambavyo wengi hufikiri ni kitu kimoja hasa kwenye matumizi. Lakini siyo sahihi, ni kweli vinahusiana kwa karibu lakini siyo kitu kimoja.
Data siyo taarifa, taarifa siyo maarifa na maarifa siyo hekima. Wengi hufikiri kwamba ukishajua kitu basi tayari umekuwa na hekima, lakini huo siyo ukweli.
Tunaweza kuangalia kimoja kimoja kabla ya kuja kwenye hitimisho la hekima.
Data ni kipande cha taarifa, kitu ambacho kinaeleza kuhusu jambo fulani. Lakini ukipewa data zenyewe, bila ya maelezo zaidi, hakuna taarifa hapo. Ukiambiwa watu 10 wamekufa kwa ajali ya pikipiki, hata kama unawaona watu hao kumi, bado hiyo siyo taarifa ya kutosha. Unahitaji maelezo zaidi kuelewa data hiyo. Hivyo ili data iwe taarifa, lazima iwe na maelezo ya kuifanya ieleweke.
Taarifa ni maelezo yanayotufanya tuelewe kuhusu data fulani, lakini kwa sababu tumeelewa kitu hicho, haimaanishi kwamba kuna kitu kipya tumejifunza ambacho tunaweza kutumia kwenye maisha yetu. Ndiyo maana taarifa siyo maarifa. Taarifa nyingi tunazopata huwa zinaishia juu juu wala hatujisumbui nazo, hatuzitumii ili kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi. Taarifa nyingi ni za kusisimua na zinapita, hazina muda mrefu kwetu.
Maarifa ni pale unapojifunza kitu ambacho unaweza kukitumia kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Lakini kwa kujifunza tu kitu hicho maisha yako hayabadiliki na kuwa bora, ni mpaka pale utakapofanyia kazi kile ambacho umejifunza. Maarifa yana nguvu ndani yake, lakini ni mpaka nguvu hiyo ifanyiwe kazi ndiyo mtu anaweza kuifaidi.
Hekima ni pale unapotumia maarifa uliyopata na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Pale unapojifunza kitu na kukifanyia kazi kwenye maisha yako, hiyo ndiyo hekima. Kujua tu haitoshi, bali unapaswa kufanyia kazi kile unachojua, na hapa ndipo maisha yako yanaendana na kile unachojua.
Hivyo ili kufika hatua ya juu kabisa, hatua ya hekima, lazima uwe na data ambazo zinakupa taarifa muhimu, yenye maarifa ndani yake na unatumia maarifa hayo kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Siyo kitu kigumu kuwa na hekima, bali inahitaji uvumilivu wa kujifunza na kufanyia kazi yale unayojifunza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,