Siku za nyuma watu walikuwa wanachukulia wazo la biashara kama kitu muhimu sana kwenye mafanikio ya biashara. Watu walifanya mawazo yao ya biashara kuwa siri kali sana ambayo haikupaswa kujulikana na yeyote.
Lakini kwenye zama hizi za taarifa, wazo la biashara limekosa kabisa thamani. Mawazo ya biashara ni mengi sana kiasi kwamba hakuna mtu anayeweza kufanyia kazi mawazo yote.
Pia kuja na wazo la biashara siyo kazi kubwa, kila mtu ana mawazo mengi sana ya biashara. Changamoto inakuwa kuja na wazo sahihi la biashara, ambalo linaweza kukuletea mafanikio unayotaka.
Hapa ndipo wengi wamekuwa wanahangaika, wasijue hatua zipi za kuchukua ili kujua kama wazo lao ni sahihi. Wengi wamekuwa wanachukua maoni ya watu kwamba wangependelea nini. Wanayapata maoni, lakini wanakuja kugundua baadaye kwamba maoni hayo siyo sahihi.
Ni kweli kwamba njia mbovu kabisa ya kupima wazo la biashara ni kukusanya maoni ya watu, hata kama ni wateja. Watu wengi wanapoombwa kutoa maoni, huwa wanatoa maoni ya kile wanachotegemewa kufanya, huwa hawapendi kumwangusha mtu, hivyo wanatoa maoni ya kumpendeza mtu.
Hivyo kutegemea maoni ya watu kama sehemu ya kupima usahihi wa wazo lako la biashara, ni kujiandaa kushindwa, kwa sababu wanachosema watu huwa siyo wanachofanya.
Njia sahihi ya kupima ubora wa wazo la biashara siyo kuwasikiliza watu wanafanya nini, bali kuwaangalia wanafanya nini, tena wanafanya nini na fedha zao.
Njia sahihi ya kupima wazo la biashara yako ni kuanza na bidhaa na kisha kuiuza moja kwa moja kwa mteja. Unapoanza na bidhaa hii unapata mrejesho sahihi kutoka kwa wateja. Kama wateja hawatainunua kabisa utajua kwamba wazo lako siyo sahihi. Kama watainunua lakini wasirudi tena au wakarudi na malalamiko, utajua wazo ni sahihi, ila ulichowapatia wateja siyo sahihi hivyo unapaswa kuboresha zaidi.
Na kama watainunua na kurudi tena kununua, unajua wazo ni sahihi na bidhaa au huduma unayowauzia watu ni sahihi.
Unapoanza na mteja na bidhaa, unajifunza mengi zaidi kuhusu biashara kuliko kukusanya maoni pekee. Unapoenda moja kwa moja kwa mteja na kupima anatumiaje fedha yake, unapata taarifa nyingi kuliko unapomuuliza mteja. Mteja atakuambia mengi kwa kununua au kutokununua kuliko pale unapomtaka akupe maoni yake.
Kwa wazo lolote la biashara ulilonalo, anza na bidhaa au huduma ya msingi kabisa ambayo mteja anaweza kuitumia, kisha uza moja kwa moja kwa wateja. Kazana kuwafikia wateja na kuwaeleza manufaa ya kile unachouza, washawishi wanunue kisha ona kama watarudi tena na kama bidhaa au huduma watakayonunua itakuwa na manufaa kwao.
Na kwa zama tunazoishi sasa, huhitaji makubwa sana ili kuanza, huhitaji hata kuwa na eneo la kufanyia biashara ili kuanza, unaweza kuanzia popote ulipo sasa na ukawatafuta wateja wa kutumia unachotoa. Mawasiliano na mtandao wa intaneti umerahisisha sana mambo, unaweza kufanya mengi ukiwa hapo ulipo kabla hujaanza kufikiria kuwa na eneo maalumu la kufanyia biashara yako.
Unapoanza biashara na wazo ambalo huna uhakika nalo, usipoteze fedha nyingi kabla hujapata mrejesho wa wateja kwenye bidhaa ya msingi kabisa utakayokuwa umeanza kuwauzia. Una nafasi ya kupima mwitikio wa wateja kwa wazo la biashara ulilonalo, tumia nafasi hiyo vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,