Rafiki, bila ya kupitia changamoto mbalimbali kwenye maisha yetu, hatuwezi kujua uwezo mkubwa ambao upo ndani yetu. Mambo yanapokwenda vizuri huwa tunajisahau na kufanya kwa ukawaida. Hivyo changamoto huwa zinakuja kama kitu cha kutustua na kutukumbusha kwamba mambo siyo rahisi kama tunavyofikiri.
Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio tunayotaka kwenye maisha yetu.
Kukusanya mtaji kwa ajili ya kuanza biashara ni changamoto kubwa sana kwa wengi, hasa pale ambapo mtu unakuwa na kipato kidogo. Kuna wakati mtu unajibana na kupata kiasi kidogo cha fedha, lakini mara yanatokea matatizo yanayopelekea wewe kutumia fedha uliyoweka akina na hivyo unarudi tena kuanza upya.
Unahitaji kuwa na njia bora zaidi ya kukuwezesha kukusanya mtaji wa biashara pale ambapo una kipato kidogo. Hili ndiyo tutakwenda kujifunza kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto.
Msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye hili, alikuwa na haya ya kusema;
“Mimi ni mwanafunzi wa chuo najitahidi kuwa na nidhamu binafsi ya fedha na matumizi ili nijiwekee kipato ila mambo ya chuo yananiingilia najikuta ile hela imetumika kwa mambo hayo sasa nifanyeje kujiwekea fedha kwa ajili ya mtaji.” – Isack A. W.
Unapopanga kukusanya mtaji wa kuanza biashara ukiwa na kipato kidogo, unapaswa kuzingatia yafuatayo;
- Jiandae kuwa na maisha ya mateso kwa kipindi fulani.
Kwa kuwa kipato chako ni kidogo na kupitia kipato hicho pia unataka kuweka akiba kwa ajili ya mtaji, lazima ujiandae kwa mateso. Mateso yatatokana na kujinyima baadhi ya vitu unavyopendelea kuwa navyo, lakini kwa sasa huwezi kwa kuwa unakusanya mtaji. Kipindi hiki cha mateso hakitakuwa kirefu sana, hivyo uvumilivu ni muhimu sana.
- Yajua matumizi yako ya msingi kabisa, kisha mengine achana nayo.
Kama hutakufa au maisha yako kuwa hovyo usiponunua kitu fulani, basi kitu hicho siyo muhimu na kinaweza kusubiri. Kitu chochote unachotamani sana kununua, lakini kinaweza kusubiri, basi kinapaswa kusubiri. Hudumia yale mahitaji ya msingi pekee, na kiasi cha fedha kinachobaki weka akiba kwa ajili ya biashara.
- Weka akina eneo ambalo huwezi kuitoa hata iweje.
Tatizo kubwa kwenye kuweka akiba ni kwamba pale unapokutana na tatizo kubwa kwenye maisha yako, linalohitaji fedha kutatua, unajikuta unarudi kwenye akiba zako, unazitumia na inakubidi uanzie tena chini. Unapaswa kuiweka akiba yako eneo ambalo huwezi kuipata hata iweje, inakuwa huna tofauti na kwamba umeitumia, hivyo unapokutana na tatizo, inakubidi utafute njia nyingine ya kulitatua na siyo kutumia akiba zako. Kuweka akiba eneo ambalo huwezi kuitoa unaweza kuwa na akaunti maalumu ya benki ambayo unaweza kuweka fedha lakini siyo rahisi kutoa.
- Fanya kazi zaidi.
Kujibana na kupunguza matumizi kuna ukomo, kuna hatua utafika huwezi tena kupunguza matumizi zaidi. Hivyo wakati unapunguza matumizi, pia unahitaji kuwa unaongeza kipato chako. Na hapa unahitaji kufanya kazi zaidi, iwe ni kazi za vibarua, za kusaidia au vyovyote vile, angalia kipi unachoweza kufanya na ukalipwa. Kama umeajiriwa omba majukumu ya ziada ambayo yatapelekea ulipwe zaidi, au unaweza kufanya kazi nyingine nje ya ile unayofanya sasa. Na fedha yote unayoongeza kwenye kazi ya ziada unayofanya, ipeleke yote kwenye akiba yako ya kuanza biashara.
- Usitafute kuonekana, bali tafuta kufikia ndoto zako.
Kosa ambalo wengi wamekuwa wanafanya wanapoanzia chini ni kutaka kuonekana au kujilinganisha na wengine, hili linawafanya waingie kwenye ushindani wa kijinga, waache kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwao na kufanya yale yatakayowafanya waonekane kwa wengine. Hakikisha unayaishi maisha yako, kulingana na vipaumbele vyako na ndoto unazofanyia kazi. Wengine wanaishije maisha yako hiyo siyo biashara yako. Na hata kuanza kufuatilia wengine wanasemaje kuhusu wewe ni upotevu wa muda wako pia. Peleka nguvu zako na muda wako wote kwenye kufikia ndoto zako na utaweza kupiga hatua zaidi.
Rafiki, fanyia kazi mambo haya matano ili uweze kukusanya mtaji wa kukuwezesha kuingia kwenye biashara hata kama kipato chako ni kidogo sana. Unahitaji kuwa na maamuzi kamili kwamba unakwenda kuwa na biashara na usiruhusu lolote likuzuie wewe kufikia maamuzi hayo.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog