Rafiki yangu mpendwa,

Kwa zama tunazoishi sasa, ajira haiwezi tena kutosheleza mtu kuweza kuendesha maisha yake ya kawaida. Hii ni kwa sababu kipato cha ajira ni kidogo na mahitaji ya maisha ni mengi.

Hivyo kila aliyepo kwenye ajira anapaswa kuwa na njia mbadala ya kuingiza kipato ili aweze kuwa na maisha bora. Pia njia hiyo mbadala ya kuingiza kipato itamwezesha mtu kununua uhuru wake baadaye, kwa kuwa ajira zimewanyima wengi uhuru wa kuwa na maisha wanayoyataka.

Lakini changamoto kwa wengi imekuwa kwamba hawana fedha za kuweza kuanza biashara, kwa sababu kipato chao ni kidogo mno. Lakini hii siyo sababu halisi, bali ni kitu cha kujificha, kwa sababu wengi hawapendi na pia hawapo tayari kuumia mwanzoni ili kupata wanachotaka.

Katika makala ya leo ya ushauri, tutakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kuanzisha biashara hata kama kipato chako ni kidogo sana. Na msomaji mwenzetu aliyekwama kwenye hili ametuandikia hapa kuomba ushauri kama ifuatavyo;

“Napata pesa lakini nashindwa nini nifanyie au biashara gani nitumie ili kuizalisha pesa hiyo kwakua nalipwa elfu 60 kwa mwezi naombeni ushauri wenu nami niwe tajiri.” – Anold C. J.

Rafiki, kipato kidogo au kukosa kipato kabisa hakujawahi kuwa kizuizi cha mtu kuingia kwenye biashara. Wapo watu wengi ambao wameweza kuingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo na wakati mwingine bila ya mtaji kabisa na wakaweza kupiga hatua kubwa sana.

Unapoanza biashara kwa mtaji kidogo au hata bila ya mtaji kabisa, kuna kitu muhimu sana unapaswa kujua, kwamba mtaji pekee unaokuwa nao ni nguvu zako mwenyewe. Jasho lako linafidia ile sehemu ya mtaji ambayo hukuwa nayo.

Hivyo hitaji la kwanza na muhimu kabisa kwenye kuanza biashara ukiwa na mtaji kidogo au bila ya mtaji kabisa ni kuwa tayari kuweka nguvu zaidi ya wengine wanavyoweka.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Baada ya utangulizi huu wa nguvu kama mtaji, sasa tuingie kwenye ushauri unawezaje kuanza biashara kwa kipato kidogo.

Hatua muhimu za kuchukua ili kuanza biashara kama kipato chako ni kidogo.

  1. Jua ni biashara gani unayotaka kufanya na ipi unaweza kuanza nayo.

Hatua ya kwanza na muhimu kabisa ni kujua aina ya biashara unayotaka kufanya, hata kama ni kubwa, wewe jua. Kujua wapi unataka kwenda ndiyo hitaji muhimu kabisa la kuanza safari ya mafanikio.

Ukishajua biashara unayotaka kufanya, kama ni kubwa na huwezi kuanzia juu, angalia ni chini kiasi gani unaweza kuanzia. Na kama hata kwa kuanzia chini bado huwezi kupata fedha hizo, basi anza na biashara nyingine ambayo utaifanya kwa muda, lakini lengo lako ni kwenda kwenye biashara ile uliyochagua.

  1. Jua kiasi cha mtaji unachohitaji ili kuweza kuanza.

Ukishachagua biashara unayoweza kuanza nayo, jua kiasi cha chini cha mtaji unachoweza kuanza nacho. Watu wengi wanaosema hawana mitaji, huwa hata hawajui ni kiasi gani cha chini wanachoweza kuanza nacho.

Wewe jua kiasi cha chini kabisa ambacho ukiwa nacho unaweza kuanza biashara, na usitake kuanza na vitu vingi, bali kuanza kwa namna ambayo unaweza kumpa mteja kile anachotaka.

  1. Weka mpango wa kukusanya kiasi hicho cha mtaji.

Ukishajua kiwango cha mtaji unachohitaji, weka mpango wa kukusanya kiasi hicho cha mtaji. Na hapa nashauri utumie njia mbili;

Njia ya kwanza ni kujiwekea akiba kwenye kipato chako mwenyewe. Kwa kila fedha unayoingiza, sehemu ya kumi iweke pembeni kama akiba ambayo baadaye utaitumia kuanzisha biashara. Hata kama kipato chako ni kidogo kiasi gani, hakikisha sehemu ya kumi unaweka pembeni. Kwa kipati cha elfu 60, weka angalau elfu sita pembeni. Jipe muda wa kukusanya mtaji huu na uweke sehemu ambayo hutaweza kutumia fedha hiyo hata kama utapata shida.

Njia ya pili ni kukusanya fedha kutoka kwa watu wako wa karibu kama mchango. Hili ni gumu kwa wengi lakini linawezekana sana. Unachofanya ni kuwachagua watu 100 ambao unawafahamu na wanakufahamu. Kisha chagua kiasi cha mtaji ambacho ungependa kupata kutoka kwa watu hao, kisha gawa kwa watu hao 100. Kama unataka kupata laki moja, ukigawa kwa 100 utapata elfu moja. Ukishapata kiasi ambacho unahitaji kila mtu akuchangie, kizidishe mara mbili, kisha wasiliana na kila mtu kumwomba akuchangie kiasi hicho ili uanze biashara. Kama nusu tu watakubali, basi utakuwa umetimiza lengo lako. Na kama utakuwa mfuatiliaji mzuri, zaidi ya nusu watakubali.

Jipe muda wa kukusanya mtaji na tumia njia zote mbili kwa pamoja. Ukiwa na nia ya kweli na kutoruhusu chochote kikukwamishe basi utaweza kukusanya mtaji wa kukuwezesha kuanza.

SOMA; USHAURI; Njia Bora Ya Kukuwezesha Kuweka Mtaji Wa Biashara Pale Unapokuwa Na Kipato Kidogo.

  1. Tumia mtaji nguvu katika kukuza mtaji wako wa kuanza.

Wakati unakusanya mtaji wa kuingia kwenye biashara uliyochagua, endelea kutumia nguvu zako kupata kipato cha ziada. Hapo ulipo una muda mwingi na nguvu ambazo unaweza kuwapa wengine na wao wakakulipa. Hivyo angalia mazingira yanayokuzunguka, ni kazi zipi unazoweza kuwasaidia wengine na wakakulipa.

Usione aibu kufanya kazi za chini, kama unalipwa na ni kazi halali fanya. Unapokuwa mtafutaji ambaye una hasira za mafanikio huwezi kuchagua aina gani ya kazi unaweza kufanya na ipi huwezi kufanya.

Fanya vibarua, wasaidie wengine kuuza bidhaa zao na wakulipe kwa kamisheni, saidia kwenye kazi mbalimbali ili tu uweze kuingiza kipato.

Fedha yote unayoingiza kupitia kazi za ziada unazofanya inapaswa kuingia moja kwa moja kwenye mtaji, usiiweke kwenye matumizi.

  1. Endelea kujifunza na kujipanga vizuri.

Wakati unaendelea na zoezi la kukusanya mtaji, endelea kujifunza kuhusiana na biashara unayotaka kuingia na pia kujipanga vizuri ili kufanikiwa kwenye biashara hiyo.

Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara ambazo hawazijui vizuri, na hivyo wanakutaka na changamoto kubwa zinazowarudisha nyuma. Wakati unakusanya mtaji, endelea kujifunza kuhusu biashara unayotaka kufanya, ifuatilie kwa karibu, wafuatilie wale wanaoifanya pia ili kujifunza.

Pia soma vitabu vitakavyokujengea misingi ya mafanikio kwenye biashara ili unapoingia unajua nini cha kufanya na nini cha kuepuka.

Pia kumbuka kama unafanya au unataka kufanya biashara ukiwa ndani ya ajira, hakikisha unasoma kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA. Ni kitabu kizuri kitakachokupa mwongozo wa kuweza kuanza na kuendesha biashara yenye mafanikio wakati bado umeajiriwa. Kukipata tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye maneno BIASHARA NDANI YA AJIRA na nitakupa maelekezo ya kupata kitabu.

Usikubali kipato kidogo kuwa kikwazo kwako kuingia kwenye biashara, kuwa na nia ya kweli na kuwa tayari kujitoa na utaweza kuingia kwenye biashara. Jipe muda na usichague nini unafanya au hufanyi kwa kuwa unajipa hadhi fulani. Unapoanzia chini kuwa tayari kufanya vitu vya chini na hivyo ndivyo vitakusukuma kufanikiwa zaidi.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog