Watu wanapoleta malalamiko kwetu, au kutokuridhika na namna ambavyo tumewatendea, hatua ya kwanza huwa tunakimbilia kujitetea.
Na katika kujitetea huko, huwa hatukosi kitu cha kuelezea au kulaumu kama sababu ya malalamiko yaliyoletwa kwetu.
Lakini kukimbilia kujitetea hakuna manufaa kwa yeyote, hakumsaidii yule anayelalamika na wala hakukusaidii wewe unayelalamikiwa. Kukimbilia kujitetea ni kujaribu kuyakwepa majukumu yako kwenye kile unachofanya.
Ndiyo maana leo nakukumbusha hili muhimu sana, usikimbilie kujitetea.
Pale mtu unayemhudumia, iwe ni kwenye kazi au bishara, au watu wengine unaohusiana nao kwa namna yoyote ile, wanapokuja kwako na malalamiko, unachopaswa kufanya ni kusikiliza kwa kina.
Usisikilize huku unatengeneza utetezi, badala yake sikiliza akili yako ikiwa wazi, sikiliza kwa lengo la kuelewa na pia jiweke kwenye viatu vya yule anayelalamika.
Sikiliza kwa lengo la kujifunza na sikiliza ukijua kwamba mtu yule kuna kitu anataka kukifikisha kwako, hata kama ni kitu kidogo au hajui akifikisheje.
Unaposikiliza kwa namna hii unajifunza, unaelewa wapi penye mapungufu, unaelewa ni nini wale wanaolalamika wanategemea kupata.
Kwa kuyaelewa hayo na kuyafanyia kazi, utaweza kuwa bora zaidi kwenye chochote unachofanya. Unakuwa bora zaidi kwa kufanyia kazi malalamiko ambayo watu wanayaleta kwako, unayapokea na kuyaelewa.
Lakini kama utakuwa mtu wa kujitetea, wa kujitoa kwenye majukumu na kuwasukumia wengine, hutajifunza na hutaweza kuboresha kile unachofanya.
Kwenye biashara, wateja ambao hawajaridhishwa, wateja ambao wana malalamiko ni fursa kubwa sana kwako kibiashara. Kwa sababu hawa ni wateja ambao kama utawaelewa na kutatua malalamiko yao, watakuamini zaidi na watakuwa mabalozi wako wazuri.
Kosa wanalofanya wafanyabiashara wengi ni kuwakwepa wateja ambao wana malalamiko, kuwaona kama ni wateja wasumbufu na wasioelewa. Kama mteja yupo tayari kulipia kile unachomuuzia, huyo ni mteja mzuri wa biashara yako, sasa jukumu lako kubwa ni kumridhisha ili aendekee kununua zaidi na zaidi na hata kuwaleta wengine pia.
Kila kinacholalamikiwa kwenye kazi au biashara yako, kichukue na kifanyie marekebisho, watu hawalalamiki bure, hata kama wanacholalamikia siyo sahihi, bado kuna kitu unaweza kuboresha zaidi na watu wakapata huduma bora zaidi.
Usikimbilie kujitetea, jipe muda wa kusikiliza, kuelewa na kisha kuchukua hatua sahihi kulingana na malalamiko unayopewa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha kwa maoni haya bora Sana, nikweli kusikiliza ni njia nzuri Sana ya kujifunza, uwe na siku njema.
LikeLike
Asante na karibu sana.
LikeLike