“There is no fun in doing nothing when you have nothing to do. Wasting time is merely an occupation then, and a most exhausting one.” – Jerome K. Jerome

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNAPOKUWA HUNA CHA KUFANYA…
Hakuna jambo linaloumiza na kuchosha kama kutokufanya chochote pale unapokuwa huna cha kufanya.
Inakuchosha japo hujafanya chochote, hivyo kupoteza muda inakuwa kama kazi ya kuchosha kwako.
Unajikuta muda unaenda, umechoka, lakini hakuna ambacho umefanya.

Rafiki, unapoipangilia siku yako, hakikisha huachi uwazi, hakikisha hujikitu kwenye hatua ambayo huna cha kufanya.
Hata kama ulichokuwa umepanga kufanya hakiwezekani kufanyika, kuwa na mbadala wa kitu kingine cha kufanya.

Ratiba yako ya siku nzima inapaswa kuwa imejaa kabisa, na usiwe na muda ambao huna cha kufanya.
Pia kama ni mapunziko yawe mapumziko kweli na isiwe ni mapumziko unayojitengenezea unapokuwa huna cha kufanya.

Mara zote kuwa na kitu mbadala cha kufanya, ili pale mambo yanapobadilika, ili kile ulichotegemea kinapokosekana, usibaki huna cha kufanya, badala yake tayari unakuwa na kitu cha kuendelea kufanyia kazi.

Na kitu kibaya zaidi ni kufika kwenye wakati ambao huna cha kufanya na kuanza kujiuliza nifanye nini. Hapa utajikuta unapoteza muda mwingi kubishana ndani yako kuhusu kipi muhimu zaidi kufanya.
Lakini unapokuwa umeweka kila kitu kwenye mipangilio yako ya siku, kimoja kinapokwama, unaingia kwenye mbadala wake bila ya kupoteza muda wowote.

Kitu kibaya sana kwenye siku yako, ni kujikuta kwenye hali ambayo huna cha kufanya, itakupotezea muda, nguvu na hata umakini wako. Mara zote jua nini utafanya na kwa wakati gani na mbadala wake ni nini.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupangilia muda wako vizuri ili usiwe na muda wa kupoteza kwa kuwa huna cha kufanya.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha