Shida ya wengi kwenye biashara huwa inakuja pale wanapobadili biashara zao.

Mwanzoni biashara inakuwa inafanya vizuri sana, na wanaona hapa sasa wanaweza kuikuza zaidi. Ni pale wanapokuza biashara ndiyo wanakaribisha matatizo ambayo hawakuwahi kuyafikiria hapo awali.

Mwingine anaweza kuwa na biashara kubwa ambayo inamsumbua, anaona suluhisho ni kuishusha chini ili kupunguza matatizo, kinachotokea inakuwa ni matatizo mapya ambayo mtu hakujua kama angekutana nayo.

Rafiki, kila biashara ina viwango vyake sahihi vya kuifanya. Hivyo kabla hujabadili biashara kutoka kiwango kimoja kwenda kingine, ni vyema ukajua kwanza kiwango sahihi kwa biashara hiyo ni kipi. Na kama utataka kubadili, uanzie wapi ili usiende kwenye matatizo.

Kama biashara inakutegemea wewe ndiyo iende, kama wateja wanakuja kununua kwa sababu ni wewe unauza, kujaribu kuikuza biashara hiyo kwa sababu inafanya vizuri utakutana na matatizo makubwa. Utaweza kufungua matawi zaidi, lakini usione wateja. Na kama ukiamua kuacha tawi la mwanzo na kwenda kwenye tawi jipya, ndiyo kabisa unaua ile biashara ya kwanza na ya pili ikishindwa kukua.

Unapojikuta kwenye hali kama hiyo, kwamba biashara inakutegemea wewe ndiyo iende, hatua yako ya kwanza kuchukua inapaswa kutengeneza misingi ya kuiwezesha biashara kujiendesha yenyewe bila ya kukutegemea wewe.

Kama wateja wanakuja kununua kwa sababu wewe ndiyo upo, cha kuanza kufanyia kazi ni kuhamishia imani ya wateja kwenye biashara na siyo kwako. Wateja waiamini biashara, wajue mara zote watahudumiwa vizuri iwe upo au haupo. Zoezi kama hili siyo la haraka, linajengwa taratibu kwa jinsi ambavyo wateja wanaendelea kupata huduma kwenye biashara yako.

Kadhalika kama unaondoka kwenye biashara ya juu na kushuka ya chini, lazima uwe umejipanga wewe kuwa ndiyo kila kitu. Kama ulishazoea majukumu fulani ni ya kitengo fulani, unaposhuka chini vitengo vinafutika na wewe unakuwa kila kitu. Na hili ndiyo huwasumbua wengi wanaotoka kwenye ajira na kuingia kwenye biashara, wanakuwa wamezoea kufanya kitu kimoja tu au vichache, wanapoingia kwenye biashara inayowataka wafanye kila kitu, wanashindwa kwenda na kasi hiyo.

Rafiki, elewa kiwango sahihi cha kuifanya biashara yako kabla hujafanya mabadiliko makubwa. Na hii haimaanishi kwamba utaendelea kubaki hapo ulipo, badala yake utafanya mabadiliko yanayoanzia kwenye msingi na ambayo hayatashindwa au kupelekea biashara kuanguka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha