“Human beings have been made for the sake of one another. Teach them or endure them.” – Marcus Aurelius

Ni nafasi nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu,
Ni fursa ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WAFUNDISHE, WAVUMILIE AU ACHANA NAO…
Binadamu tupo hapa duniani kwa ajili ya wengine na siyo kwa ajili yetu binafsi.
Ungekuwa wewe mwenyewe dunia nzima, maisha yangekosa maana kabisa.
Maana ya maisha yetu inatokana na jinsi tunavyojihusisha na wengine.
Mahusiano yetu na wengine yana mchango mkubwa sana kwenye ubora wa maisha yetu.
Kuna wakati watu wanafanya vitu ambavyo hatukitegemea wafanye au wanashindwa kufanya vile ambavyo tulitegemea wafanye.
Na hapa ndipo changamoto zote za kimaisha zinapoanzia.

Kuna hatua tatu za kuchukua kwenye kutatua na kuboresha mahusiano yetu na wengine.
Moja; WAFUNDISHE, kama watu wanafanya tofauti na ulivyotegemea, wafundishe njia sahihi ya kufanya ili mambo yaweze kwenda vizuri. Pia wape sababu sahihi kwa nini wanapaswa kufanya vizuri chochote unachowataka wafanye.
Hatua ya kuwafundisha ni muhimu sana, maana inasaidia kujenga msingi muhimu. Lakini siyo wote wanafundishika, hivyo unaenda hatua ya pili.

Mbili; WAVUMILIE.
Kama watu hawafundishiki, lakini pia wana mchango mzuri kwenye kile unachotaka, unaweza kuwavumilia kwenye yale maeneo ambayo hawafundishiki. Lakini hapa unapima manufaa wanayoleta ukilinganisha na yale wanayoshindwa kufanya. Kama manufaa ni nakubwa, unawavumilia kwa sababu huwezi kumfanya kila mtu afanye kama unavyotaka wewe.
Lakini wapo ambao hawafundishiki na hawana manufaa, hasa sasa, hatua ya tatu inawafaa.

Tatu; ACHANA NAO
Kama mtu hafundishiki, na pia hana manufaa makubwa anayoyaleta, hatua pekee unayoweza kuchukua ni kuachana naye. Huo ni mzigo ambao ukiendelea kukaa nao utakuzamisha. Kwa sababu hafanyi unachitegemea afanye na pia hakuna manufaa yoyote anayoleta, yani awepo asiwepo hakuna tofauti.
Hawa ni watu unapaswa kuachana nao, na kadiri unavyoachana nao mapema, ndivyo inakuwa nafuu kwako.

Tumeumbwa kwa ajili ya wengine na hivyo tunapaswa kufundishana na kuvumiliana. Na pale hayo yanaposhindikana ni vyema kila mtu kushika njia yake ili kuepuka kupotezeana muda na kusumbuana kila wakati.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kushirikiana na wengine vizuri ili kuweza kupiga hatua kubwa kuelekea kwenye mafanikio yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha