Rafiki, moja ya rasilimali muhimu ambazo ni adimu sana kwetu ni muda. Muda ukishapita haurudi tena, ukipoteza fedha unaweza kuipata, lakini ukipoteza muda ndiyo umeupoteza moja kwa moja, haurudi tena.

Hivyo tunapaswa kuwa waangalifu sana kwa namba tunavyotumia muda tulionao, kwa sababu tukishaweka muda kwenye kitu chochote kile, hatuwezi kuurudisha tena muda huo, ndiyo unakuwa umeondoka moja kwa moja.

Moja ya msingi utakaokusaidia sana kwenye kulinda muda wako na kufanya yale ambayo ni muhimu pekee ni msingi wa fanya vizuri au usifanye kabisa.

Msingi huu unakwenda hivi; chochote unachofanya kwenye maisha yako, unapaswa kukifanya vizuri sana na kama huwezi kukifanya vizuri basi ni bora usikifanye kabisa. Hii ina maana kwamba unajitoa kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana na siyo kufanya kwa kawaida.

Kwa sababu kufanya chochote kwa kawaida, ni kupoteza ule muda ambao umetumia kufanya kitu hicho, kwa sababu kawaida haina thamani, kawaida hailipi, hakuna anayejali kawaida, kawaida ni kupoteza muda na nguvu zako.

Kama kitu unataka kufanya kawaida, okoa tu muda wako kwa kutokukifanya kabisa, kwa sababu muda unaoweka kwenye kile unachofanya kawaida, ni muda ambao umechagua kuupoteza.

Weka juhudi zaidi kwenye chochote unachofanya, nenda hatua ya ziada, kuwa mbunifu zaidi na fanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kama unaruhusu muda wako wa thamani uende kwenye kile unachofanya, basi kazana sana kukifanya kwa ubora, jisukume mpaka tone la mwisho kuhakikisha umefanya kwa ubora wa hali ya juu sana.

Na usiishie kufanya kadiri ya uwezo wako, bali nenda mbele na kufanya kadiri inavyopaswa kufanywa. Usifanye kile unachoweza, bali fanya kile kinachopaswa kufanyika na kwa namna hiyo utapata matokeo bora sana.

Usipoteze muda na nguvu zako kwenye vitu vya kawaida, vitu ambavyo kila mtu anaweza kufanya. Badala yake wekeza muda na nguvu zako kwenye vitu vya kipekee, vitu ambavyo hakuna mwingine anayeweza kufanya kama ulivyofanya wewe.

Chochote unachogusa, kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana, na kama hilo haliwezekani basi achana nacho, usikifanye kabisa. Kwa sababu haitakuwa na msaada kwako wala kwa mwingine yeyote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha