Kosa kubwa ambalo wafanyabiashara wengi wanalifanya ni kuanza biashara zao upya kila wakati. Kila mara wanatafuta wateja wapya kama vile hawajulikani kabisa.
Tatizo hili linatokana na wafanyabiashara wengi kukosa mpango endelevu wa kibiashara. Kwao biashara ni kutafuta wateja wapya kila wakati. Hivyo wakishamhudumia mteja wanayempata, wanaachana naye na kuanza kutafuta mteja mwingine mpya.
Hakuna ubaya wowote kwenye kutafuta wateja wapya, kwa sababu kila wakati biashara inahitaji wateja wapya. Ubaya upo pale ambapo juhudi za kutafuta wateja wapya, zinapelekea wateja wa zamani kusahaulika.
Mteja mzuri wa biashara yako, ni yule ambaye tayari unaye, yule ambaye tayari ameshanunua kwako. Kwa sababu mpaka mteja ananunua kwako ina maana kwamba ameridhika na kile unachouza na pia amekuamini. Hivyo unapaswa kutumia hilo kumfanya mteja anunue zaidi na pia akuletee wateja wengi zaidi.
Katika mikakati yako ya kuikuza biashara yako, usiangalie kupata wateja wapya pekee, bali angalia unanufaikaje na wateja ambao tayari walishanunua kwako. Angalia wateja hao wanaweza kununua nini zaidi. Angalia wanaweza kuwaleta watu wengine wapya kiasi gani.
Kwa kumtumia vizuri kila mteja ambaye alishanunua kwako, unatumia nguvu uliyoweka mwanzo kupata matokeo makubwa.
Acha kuianza biashara yako upya kila wakati kwa kutafuta wateja wapya mara zote. Badala yake endeleza biashara yako kwa kuwatumia wateja ambao tayari unao. Watumie wateja ulionao sasa, wanunue zaidi kwako na pia wakuletee wateja wengine wengi zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,