“Set your life on fire. Seek those who fan your flames.” ~ Rumi
Amka mwanamafanikio,
Amka siyo tu kutoka kwenye usingizi, bali kutoka kwenye maisha ya kawaida, maisha ambayo hayana uelekeo na amka uweke sawa uelekeo wa maisha yako.
Amka ujikumbushe malengo yako makubwa kwa kuyaandika,
Na amka uipangilie siku yako vyema kabla hujaianza.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WATAFUTE WANAOCHOCHEA MOTO…
Rafiki, unapaswa kujiwasha moto, kisha kuwatafuta wale ambao wanachochea moto uliopo ndani yako.
Hupaswi kuhangaika na wale wanaozima moto huo, badala yake tafuta wanaouchochea.
Ni wale wanaochochea moto uliopo ndani yako ndiyo wanaokusukuma kwenda mbele zaidi.
Kwenye maisha yako unahitaji watu wa kukuambia unaweza, inawezekana na utayashinda magumu unayopitia.
Huhitaji watu wa kukuambia huwezi, haiwezekani na utashindwa kwenye ugumu unaopitia.
Wazimaji wa moto wapo wengi, kwa sababu wao wenyewe hawana moto ndani yao, hivyo unapaswa kuwajua na kukaa nao mbali.
Watakaochochea moto wako ni wale ambao wana moto ndani yao pia.
Wale ambao wanataka makubwa na wanayafanyia kazi.
Hawa ndiyo watakaokupa hamasa ya kufanya makubwa pia.
Jiwashe moto ili uwaone wengine ambao wamejiwasha moto pia, ambao watachochea moto uliopo ndani yako.
Na achana kabisa na wale ambao hawana moto ndani yao, kwa sababu hawa ni wataalamu wa kuzima moto kwenye maisha ya wengine.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwavutia kwako wale ambao wanachochea moto uliopo ndani yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha