Msingi mkuu wa mafanikio umejengwa kwenye nidhamu, bila nidhamu hakuna hatua ambayo mtu anaweza kupiga. Bila nidhamu mipango mikubwa inabaki kuwa hadithi zisizotekelezeka.
Wengi wamekuwa wazuri kwenye kupanga, lakini inapofika kwenye utekelezaji, wengi wamekuwa wanashindwa kuchukua hatua, wapo ambao hata hawaanzi kabisa. Lakini pia wapo ambao wanaanza na kuishia njiani.
Nidhamu kama msingi wa mafanikio siyo kitu kigumu kama wengi wanavyodhani. Nidhamu ni kuweka mipango na kuitekeleza kadiri ambavyo mtu amepanga, na kutokuruhusu chochote kiingilie katika mipango hiyo.
Nidhamu inakaziwa zaidi na uhitaji na umuhimu. Chukua mfano wa siku ambayo kuna kazi inapaswa kukamilika, tarehe ya mwisho imefika, utaifanya bila ya kuwa na usumbufu wowote. Lakini kazi hiyo hiyo hukuweza kuifanya pale ambapo hukuwa na msukumo wa tarehe ya mwisho.
Nidhamu siyo ngumu, bali sisi wenyewe tumekuwa tunaifanya kuwa ngumu kwa kuangalia hatua tunazopaswa kufuata na kuona kama ni ngumu na nyingi. Tunapofikia kufanya kile tulichopanga, huwa tunaona kuanza ni kugumu, hatua za kupiga ni nyingi mwanzoni na hatutajiandaa vya kutosha. Hivyo inakuwa rahisi kwetu kujiambia wacha tujiandae kwanza.
Nidhamu ni rahisi pale unapojiwekea viwango kwenye maisha yako na kutokushuka kwenye viwango hivyo. Nidhamu ni kuchagua kilicho bora na kukazana na hicho, kutokwenda chini ya kiwango ulichojiwekea.
Nidhamu ni kuchagua kufanya maamuzi sahihi ambayo tayari unajua majibu yake ndani yako. Kila mtu anajua kazi inakuja kabla ya mapumziko, kila mtu anajua anapaswa kula vizuri, kufanya mazoezi na kuimarisha afya yake na mahusiano yake na wengine. Hakuna asiyejua kipi sahihi cha kufanya, ila tu wengi wanapotea kwenye kuona ugumu hasa mwanzoni.
Nidhamu ni kujua kilicho sahihi na kufanya kwa muda uliopanga kufanya. Hata kama hujisikii kufanya, unaanza kufanya na ukishaanza, ni rahisi kuendelea kufanya.
Usifanye nidhamu kuwa kitu kigumu kwako, bali ifanye kuwa sehemu ya maisha yako. Panga na fanya kilicho sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,