“Learn to express, not impress.” – Jim Rohn
Siku mpya,
Siku bora,
Siku ya kipekee sana kwetu.
Tumapata nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JIFUNZE KUJIELEZA NA SIYO KUJIONESHA…
Tunaishi kwenye zama ambazo kila mtu anataka kujionesha,
Lakini ni wachache sana wanaoweza kujieleza na wakaeleweka.
Tumezungukwa na vifaa na teknolojia ambazo ni rahisi kujionesha kuliko kujieleza.
Angalia mitandao ya kijamii, inavyopenda na kuhamasisha watu kuweka picha za kuonesha wana nini au wanafanya nini.
Lakini mitandao hiyo haihamasishi watu kujieleza kwa kuandika zaidi.
Watu nao wanazidi kuwa vilema wa kujionesha na kushindwa kujieleza.
Mwambie mtu ajieleze yeye ni nani, anafanya nini na anataka nini kwenye maisha yake na utakuwa umempa mtihani mgumu wa maisha yake.
Lakini mwambie akuoneshe ana nini au amefanya nini kwenye maisha yake (ambacho hata siyo muhimu) atakuonesha picha mpaka utachoka.
Siku za nyuma watu walikuwa wakikaa chini kuandika jinsi siku zao zilivyokwenda, yale waliyofanya na yale waliyojifunza.
Lakini siku hizi mwisho wa siku watu wanakaa chini kuangalia picha zipi wamepiga vizuri na marekebisho gani ya kufanya kabla hawajazituma kwenye mitandao.
Tunageuzwa kuwa watu wa kujionesha badala ya kuwa watu wa kujieleza.
Ona hatari hii na iepuke mara moja,
Usikimbilie kujionesha, kimbilia kujieleza.
Usitake kupiga picha kuonekana,
Badala yake andika au sema kitu kinachoeleweka.
Kujifunza namna bora ya kujieleza kuna manufaa makubwa sana kwako.
Na hatua ya kwanza ni kujifunza kuandika na kuandika kila siku, hata kama hakuna anayesoma unachoandika.
Kitendo cha kukaa chini na kuandika, kinalazimisha akili yako kunyoosha maelezo, kitu ambacho wa kujionesha hawakipati.
Jifunze kujieleza na siyo kujionesha, kujieleza kutayafanya maisha yako kuwa bora kuliko kujionesha.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujieleza na siyo kujionesha, siku ya kuandika na siyo kupiga picha.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha