Moja ya sifa ya ziada unayopaswa kuwa nayo ili kufanikiwa kwenye biashara ni kuwa mtabiri.
Unapaswa kuweza kutabiri yale yanayokwenda kutokea kwenye biashara yako na wateja wako.
Na siyo tu kutabiri kwa kujifurahisha, bali kwa kuwa na maandalizi ambayo yataendana na mabadiliko yanayokwenda kutoka kwenye biashara yako na kwa wateja wako pia.
Biashara nyingi zinakufa kwa sababu zinapoteza wateja zaidi ya zinavyopata wateja wapya. Biashara hizi zinapoteza wateja kwa sababu wateja wanakua huku biashara ikiwa haikui.
Hivyo inawabidi wateja kutafuta huduma pengine kwa sababu pale walipo sasa hapawatoshelezi tena.
Lengo lako kubwa kwenye biashara linapaswa kukua na wateja wako. Kadiri wateja wanavyokua, ndivyo pia biashara yako inavyopaswa kukua.
Biashara yako inapaswa kuwa pale mteja wako alipo sasa, na wakati huo huo iweze kumtangulia kule anakokwenda.
Hii ina maana mteja atakapotoka pale alipo sasa na kwenda mbele zaidi, akutane na biashara yako huko mbele pia.
Utaweza kufanya hili kama unaijua biashara yako kwa kina, kama unawajua vizuri wateja wako na unafuatilia kila kinachoendelea kwenye biashara yako.
Unapokuwa karibu na biashara yako kwa kiwango cha aina hii, unaziona fursa za kuwa bora zaidi na kuwahudumia wateja wako kwa ubora wa hali ya juu zaidi.
Kamwe usiendeshe biashara yako kwa mazoea, usifanye kitu leo kwa sababu ndiyo ulichofanya jana. Na wala kesho usilazimishe iwe kama leo.
Kila siku mpya ni nafasi kwa biashara yako kuwajua wateja wako vizuri na kuweza kuwasaidia vizuri.
Kwa kujua matatizo na mahitaji ya wateja kabla hata hayajaanza kuwasukuma, kutakuwezesha kuwa mbele ya wateja wako na kuwahudumia vizuri pale watakapohitaji zaidi.
Kuna fursa nyingi sana za ukuaji kwenye biashara unayofanya sasa hivi, zitumie vizuri ili uweze kupiga hatua kwenye biashara yako na maisha yako pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,