Rafiki,
Umewahi kugundua kwamba mara nyingi huwa unajipa kila aina ya sababu kwa nini kile ulichonacho au unachofanya ndiyo sahihi?
Labda ni kazi au biashara fulani unafanya na unajiambia hiyo ndiyo sahihi kufanya. Halafu baadaye unaondoka kwenye kazi au biashara hiyo na kwenda kwenye nyingine, unajipa tena sababu kwa nini ile uliyoenda ni sahihi kuliko ya mwanzo.
Au upo kwenye mahusiano fulani unajipa sababu kwa nini ni sahihi, kisha mahusiano hayo yanavunjika na unajipa tena sababu kwa nini mahusiano hayo hayakuwa sahihi.
Kama usipokuwa makini, ni rahisi sana kujidanganya kwenye kila kitu kwa kujipa sababu kwa nini ni sahihi, hata kama kwa wengine kinaonekana siyo sahihi.
Ili kuepuka kujidanganya kwa sababu unazojipa za usahihi wa kila unachofanya, jipe nafasi ya kuwa mtu wa pembeni. Yaani kuangalia kile unachojipa sababu ni sahihi kwako kama ambavyo angeangalia mwingine ambaye hahusiki nacho.
Na njia nzuri ya kuweza kuangalia hivi ni kumuuliza mtu ambaye hana uhusiano wa karibu na yeye, akupe maoni yake juu ya kitu hicho. Ila usimpe upande wako kabla ya kumuuliza.
Kwa mfano kama unataka mtu akupe maoni kama kitu A ni kizuri, usimuulize; eti kitu A si kizuri? Hapo atajua unataka kitu A kiwe kizuri na hivyo atakujibu ni kizuri. Lakini ukimuuliza unaonaje kitu A, hapo atamwagika na kueleza vile anavyokiona yeye.
Rafiki, unapaswa kuwa makini sana na kujidanganya huku kwa kujipa sababu za kwa nini kile unachofanya ndiyo sahihi, hivyo kuwa makini ili uweze kufanya kilicho sahihi na siyo kujidanganya unafanya kilicho sahihi.
Kiangalie kila unachofanya au kujihusisha nacho kama anavyokiona mtu wa pembeni na fanya maamuzi kabla hujaingiza hisia zako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana nazidi kujifunza mungu azidi kukupa uzima
LikeLike
Karibu sana
LikeLike
Ahsante sana kocha hakika kila tunachokifanya tujiweke pemben kuangalia kama wengine watakavyokiona na ndo uhalisi tunapoteza muda mwing kwa kutotumia mbinu hii kwa kuwa tunaona tunachokifanya ndo sahihi kwa vile tunakipenda ahsante sana kocha makirita
LikeLike