Watu wengi huwa hawapendi pale wanapopata wasichotaka, huwa wanaona kama wamepoteza muda wao na juhudi walizoweka kwenye kile walichofanya.
Lakini hilo siyo sahihi, kupata usichotaka siyo kupoteza muda wala nguvu, bali ni kujisogeza karibu zaidi na kile unachotaka.
Kupata usichotaka siyo sawa na kukosa kabisa. Kwa sababu kwa kupata usichotaka unajifunza mengi kuliko kukosa kabisa.
Kwanza kabisa unajifunza njia ipi siyo sahihi ya kupata kile unachotaka na hivyo kutorudia tena njia hiyo uliyotumia, kwa sababu kurudia kile kile kutaleta matokeo yale yale.
Pili kupata usichotaka kunaongeza thamani ya kile unachotaka, kadiri inavyokuwa vigumu kwako kukipata au kukifikia ndivyo unavyokithamini zaidi. Kama utakipata kitu haraka na kwa urahisi, ndani ya fikra zako hutakijali sana.
Kupata usichotaka pia kunakupa funzo kubwa sana kwenye maisha, kwamba siyo kila wakati unapata unachotaka, hata kama utafanya kila unachopaswa kufanya. Kunakufundisha kwamba dunia haina upendeleo wala haijali sana wewe unataka nini. Dunia inajiendesha kwa namna inavyoenda yenyewe na siyo kwa namna ambavyo mtu unavyotaka.
Pia kupata usichotaka, ni kiashiria kwamba unaweza kupata unachotaka. Unapokosa kabisa unachotaka, unaweza kukata tamaa kwamba haiwezekani, lakini unapopata usichotaka, kunakupa matumaini kwamba ni rahisi kupata kile unachotaka.
Rafiki lengo langu leo nataka ukumbuke kwamba kupata matokeo ambayo hukutarajia kupata siyo sawa na kutokupata matokeo kabisa, hivyo usiumie wala kukata tamaa, badala yake weka juhudi zaidi ili uweze kupata matokeo unayotaka kupata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,