“When you have accustomed your body to a frugal regime, don’t put on airs about it, and if you only drink water, don’t broadcast the fact all the time. And if you ever want to go in for endurance training, do it for yourself and not for the world to see.” – Epictetus

Hongera sana rafiki yangu mpendwa kwa nafasi hii nyingine nzuri na ya kipekee sana tuliyoipata leo.
Ni fursa bora kwetu kwenda kufanya yale ambayo jana tulijiambia tutafanya kesho.
Kesho yenyewe ndiyo hii, tafadhali usipeleke tena mbele.
Tunakwenda kuianza siku hii kwa shukrani kubwa sana kwa sababu siyo wote wameweza kuiona.
Na tunaiendea siku hii kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo leo tutaweza kufanya makubwa sana.

Asubuhi ya leo tutafakari SIYO KWA AJILI YA MATANGAZO…
Unapochagua kuyabadili maisha yako,
Unapochagua kuyafanya maisha yako kuwa bora,
Fanya kwa sababu unataka kuwa bora,
Na siyo ufanye kwa ajili ya matangazo.

Tunaishi kwenye zama ambazo watu wanafanya mambo kwa ajili ya matangazo na kuonekana kuliko kwa ajili yao binafsi.
Watu wanafanya vitu ili kuweza kuonesha kwenye mitandao kwamba wao wako vizuri kuliko wengine.

Angalia kila mwanzo wa mwaka kila mtu mtandaoni anaanza mwaka na mambo mazuri.
Kila mtu anaanza mwaka na mazoezi, dayati, kusoma vitabu na kadhalika.
Lakini hazipiti siku nyingi hutaona tena watu hao wakitangaza yale waliyoanza yanaendeleaje.
Wanakuwa wameshaishia njiani, kwa sababu kilichowasukuma kufanya siyo sahihi.

Chochote unachochagua kufanya kwenye maisha yako, chagua kukifanya kwa sababu unataka matokeo yake yaboreshe maisha yako, na siyo kukifanya kwa sababu unataka uonekane.
Na kama kile unachofanya ni sahihi, wala huhitaji kupiga kelele, watu watajionea wenyewe.

Kama kweli unafanya mazoezi kama unavyotangaza, hilo litaonekana kwenye uimara wa afya yako.
Kama kweli unaishi kwa dayati unayosema, hilo litaonekana kwenye uzito wako.
Na kama kweli unasoma kama unavyosema, hilo litaonekana kwenye hekima yako, maamuzi yako na namna unavyotatua changamoto unazokutana nazo.

Okoa nguvu unazoweza kupoteza kwenye kupiga kelele na kutangaza kila mtu ajue, badala yake peleka nguvu hizo kwenye kufanya kweli na matokeo yataonekana na kila mtu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya kwa sababu unataka kufanya na siyo kufanya kwa sababu ya maonesho.
#IshiMaishaSiyoMaonesho, #AchaManenoWekaKazi, #MatokeoYataongeaYenyewe

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha