Pata picha una mche wako wa mwembe, mche ambao unataka uzae matunda haraka.

Hivyo unapanda mche wako huo, lakini huoni matunda yakitoka haraka, unaona eneo ulilopanda siyo sahihi, unaung’oa na kwenda kuupanda sehemu nyingine, hapo pia matunda hayatoki haraka. Unaung’oa tena na kwenda kuotesha sehemu nyingine. Unaendelea na zoezi hilo kila wakati.

Swali ni je unafikiri mche huo wa mwembe utatoa matunda kwa kuhamishwa hamishwa kiasi hicho? Jibu ni hapana, mti hautoi matunda kwa kuhamishwa hamishwa.

Mti unaozaa matunda ni ule ambao unaota na kukomaa kwenye eneo uliopo, unapeleka mizizi yake kwenye kina kirefu na kuwa imara, kisha unaanza kuzaa matunda. Kama mti unachelewa kuzaa matunda, kuuhamisha hakuharakishi zoezi, badala yake kunaurudisha nyuma. Kitu bora unachoweza kufanya ni kuuhudumia vizuri pale ulipo, kuupa mbolea, maji na virutubisho vingine.

Sasa peleka hali hiyo ya mti kwenye maisha yako, umeingia kwenye kazi ya kwanza, ukaona hailipi, ukaenda kwenye kazi nyingine nayo pia hailipi, ukaenda nyingine na nyingine. Je unafikiri kuhamahama kazi ndiyo kutaongeza kipato chako?

Kadhalika kwenye biashara, unaanza biashara fulani, unaona hailipi, unaenda kwenye biashara nyingine, nako kipato kinakuwa siyo bora kama ulivyodhani, unahama tena.

Kuhama hama kwa lolote unalofanya hakutakusaidia kupata kile unachotafuta, badala yake kunakuchelewesha. Ili kuweza kupata matokeo bora, unahitaji kuweka muda kwenye kile unachofanya ili kuweza kukomaa na kuzalisha matokeo bora. Unahitaji kujenga uzoefu ambao utakuwezesha kutoa thamani zaidi. Na pia unahitaji kutengeneza mtandao bora wa watu ambao wanakujua kwenye kile unachofanya.

Vitu hivyo ndiyo vitakuwezesha kulipwa zaidi na kupata mengine mazuri unayotaka.

Chagua wapi upo tayari kuweka muda na nguvu na weka vitu hivyo bila ya kuhama hama na utaweza kufikia mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha