“We must give up many things to which we are addicted, considering them to be good. Otherwise, courage will vanish, which should continually test itself. Greatness of soul will be lost, which can’t stand out unless it disdains as petty what the mob regards as most desirable.
—SENECA, MORAL LETTERS, 74.12b–13
Siku mpya, siku nzuri na siku ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora kabisa kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUONA URAIBU WETU…
Kuna tabia fulani ambazo huwa tunazianzisha kwenye maisha yetu, tabia ambazo wala hazina madhara makubwa kwetu, zinaonekana ni za kawaida kabisa.
Lakini kadiri muda unavyokwenda, tabia hizi zinazidi kushika mizizi na baadaye zinakuwa uraibu na ulevi kwetu. Tunajikuta hatuwezi tena kuacha kufanya tabia zile. Tunajikuta tumekuwa watumwa wa tabia zile na zinayaendesha maisha yetu kama vile hatuna maamuzi.
Hupaswi kujiruhusu kuwa na ulevi au uraibu wa kitu chochote, kwamba ushindwe kufanya mengine kwa sababu inabidi kwanza ufanye kile ulichozoea.
Kagua maisha yako na tabia zako sasa, na ujue tabia zipi zimeshajipa nafasi kubwa kwenye maisha yako. Je ni unywaji wa soda au kahawa ambao unajiambia huwezi kuacha? Au ni matumizi ya mitandao ya kijamii ambayo unatamani sana kuyaacha lakini unajiambia huwezi? Je ni kufuatilia maisha ya wengine kiasi kwamba unaona maisha hayawezi kwenda mpaka ujue kila kinachoendelea kwenye maisha ya wengine?
Kwa tabia yoyote ambayo imeshafikia hali ya wewe kufikiri huwezi kuiacha, unapaswa kuiacha mara moja. Kwa kuiacha unajenga upya uwezo wako wa kufikiri kwa usahihi na kufanya maamuzi bora kwako. Huwi tena mtumwa, bali unakuwa msimamizi wa maisha yako.
Uaikubali chochote kiwe na nafasi ya kuyatawala maisha yako bali fikra zako ndiyo zinapaswa kuyatawala.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuvunja kila aina ya ulevi na uraibu ili uweze kuwa huru na kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
#KuwaHuru, #VunjaUraibu, #FikiriKwaUhuru
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,