Mara nyingi ufanyaji wetu wa kazi huwa unatokana na namna wengine wanafanya. Ndiyo maana unapoenda eneo fulani la kazi au la biashara, unakuta aina ya huduma unazopata hazitofautiani sana.

Wengi wanafanya hivi kwa sababu ni rahisi na haiumizi. Ni rahisi kufanya kile ambacho wengine wanafanya na imezoeleka, huhitaji kutoa maelezo ya ziada kwa nini umefanya vile.

Na kwa kuwa wengi wanapenda urahisi, basi wanakimbilia kufanya kile ambacho kinafanywa na wengine. Lakini hii siyo njia ya kuelekea kwenye mafanikio, hii ni njia ya kuwa kawaida, na kawaida ni njia ya kuelekea kushindwa.

Chochote unachofanya, usifanye kama wengine wanavyofanya, bali fanya kama ilivyo bora kwako kufanya. Hata kama ni wewe pekee utakayekuwa unafanya hivyo na watu wanakupinga na kukushangaa, kama ndiyo namna sahihi kufanya basi fanya hivyo.

Acha wengine wafanye kwa kuigana, acha wengine wakimbie vitu vigumu na kufanya vitu rahisi. Lakini wewe kazana kufanya kilicho sahihi, fanya yaliyo magumu.

Tengeneza viwango vyako vya ufanyaji na fanya kwa namna inavyohitajika kufanya, na siyo kwa namna unavyojisikia kufanya. Acha kufanya kwa kujisikia kwa wachanga na wasiojua wapi wanakwenda. Ila wewe fanya kwa viwango vya juu zaidi, fanya kwa ubora zaidi.

Usitegemee vitu viwe rahisi, jua vitakuwa vigumu, jiandae kwa hilo na wakati mwingine tafuta kabisa palipo na ugumu na nenda hapo. Hili litakufanya ukomae zaidi na uweze kupata matokeo bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha