Kila kitu kwenye maisha kina kanuni zake, ndiyo maana watu wawili wanaweza kuwa wanafanya kitu kimoja, mmoja akafanikiwa sana huku mwingine akishindwa kabisa.

Tofauti haipo kwenye kile watu wanachofanya, bali ipo kwenye namna wanavyofanya. Ukijua namna ambavyo watu waliofanikiwa wanafanya mambo yao, na ukafanya kama wanavyofanya, hata kama hutawafikia, lakini utapata matokeo ya tofauti na unayopata sasa.

Leo nakushirikisha kanuni muhimu sana ya mafanikio kwenye biashara, ambayo ukiifuata kwenye biashara yako, utapiga hatua sana.

Kanuni hiyo inasema; eneo sahihi, muda sahihi, suluhisho sahihi, mawasiliano sahihi, hatua sahihi, malipo sahihi, rudia.

  1. Eneo sahihi.

Kuna biashara nyingi ambazo zinaanzishwa maeneo ambayo siyo sahihi, unakuta biashara ni nzuri, lakini kwa ilipo haina wateja. Unapawa kuanzisha biashara kwenye eneo sahihi, eneo ambalo wateja wapo ili uweze kuendesha biashara.

  1. Muda sahihi.

Kuna biashara ambazo zinaanzishwa kwenye eneo sahihi, lakini kipindi ambacho zinakuwa zimeanzishwa siyo sahihi. Labda watu wanakuwa hawajaielewa biashara hiyo, au siyo msimu wa watu hao kutumia kitu kinachouzwa. Unapaswa kuanzisha biashara kwa wakati sahihi.

  1. Suluhisho sahihi.

Unaweza kuanza biashara eneo sahihi na lenye wateja wenye uhitaji, lakini usiuze kama kile unachouza hakiwasaidii wateja kutatua tatizo walilonalo. Biashara yako inapaswa kutatua tatizo sahihi la mteja.

  1. Mawasiliano sahihi.

Unaweza kuwa na biashara uliyoanzisha eneo sahihi, ukawa na suluhisho sahihi kwa wateja wako na bado usiuze, kama hautakuwa na njia sahihi ya kuwasiliana na wateja wako. Ili watu wajue na kununua unachouza, lazima uwasiliane nao, lazima uwe na mpango wa masoko ambao unawafikia wateja wa biashara yako na wanajua kuhusu uwepo wako na wananufaikaje na kile unachouza.

  1. Hatua sahihi.

Hatua unazochukua kwenye biashara yako ni muhimu sana. Ili biashara ikue na kuleta faida, lazima uchukue hatua kubwa, kuwafikia wengi na kuwapa huduma bora kabisa. Kama unafanya biashara kwa ukawaida, huendi hatua ya ziada, usitegemee matokeo makubwa kutoka kwenye biashara hiyo. Kwenye biashara na kwenye maisha kwa ujumla, unapata kile unachotoa.

  1. Malipo sahihi.

Unaweza kuwa na biashara sahihi, eneo sahihi, suluhisho sahihi na wateja wananunua sana. Lakini malipo yasipokuwa sahihi, hutaweza kupiga hatua. Kama unauza bei rahisi ili wengi wanunue, na unapata faida ndogo, hutaweza kutoa huduma bora na hata kupiga hatua kutakuwa kugumu. Lazima uipangilie biashara yako kwa namna ambayo malipo unayopata yanakuwezesha kuendesha maisha yako na hata kutoa huduma bora zaidi kupitia biashara hiyo.

Ukishaanzisha biashara inayokidhi vigezo vyote hivyo sita, hapo sasa unayo biashara, unayo mashine ya kuchapa fedha. Sasa ukishakuwa na mashine ya kuchapa fedha unahitaji nini tena? Ni kurudia huo mchakato kila wakati. Kila siku boresha biashara yako kwenye maeneo hayo, na pia angalia fursa nyingine ambapo unaweza kutumia kanuni hiyo kuanzisha na kukuza biashara mpya.

Hiyo ndiyo kanuni muhimu ya mafanikio kwenye biashara, itumie.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha