Tumekuwa hatupati tunachotaka na wakati huo huo tunakuwa haturidhiki na maisha tuliyonayo.

Na hii siyo kwa sababu wengine wanapata wanachotaka au wana maisha bora sana kuliko sisi, bali kwa sababu tunajua tunajikwamisha wenyewe.

Tumekuwa tunajikwamisha sisi wenyewe pale ambapo maneno yetu hayaendani na matendo yetu.

Tunasema na kuweka mipango mikubwa, tunakuwa na malengo makubwa sana, na pia tunatamani kufika hatua za juu zaidi. Lakini hatua tunazochukua zinakuwa ni hatua za kawaida sana, hatua ambazo tumekuwa tunachukua maisha yetu yote.

Kwa hatua hizo tunazochukua, tunapata matokeo yale yale ambayo tumezoea kuyapata, na hapa ndipo tunapoona labda sisi hatuna bahati.

Ukweli uko wazi rafiki, huwezi kufika unakotaka kama matendo yako hayaendani na maneno yako. Kama unafikiria makubwa na kufanya kidogo, huwezi kamwe kupata makubwa.

Utaishi kupata matokeo yanayoendana na hatua unazochukua, bila ya kujali unafikiri makubwa kiasi gani, hata kama unaamini inawezekana kiasi gani. Utapata unachofanyia kazi, na siyo unachofikiri au kutamani.

Kila siku jikumbushe hili, kila unapoyaandika malengo yako, jiulize je kwa hatua unazochukua utayafikia malengo hayo? Kila hatua unayochukua jiulize ina mchango kiasi gani kukufikisha kwenye malengo yako makubwa.

Kama umeingia facebook au instagram mara 5 kwa siku, jiulize je kuingia kwako instagramu mara hizo 5 kwa siku kuna mchango gani kwako kufikia mafanikio makubwa?

Kama umebishana na watu kwa saa nzima, au umeangalia habari kwa saa nzima, jiulize je saa hiyo nzima umeiwekeza sawasawa ili kufika kule unakotaka?

Ukianza kufikiri hivi rafiki, utajirekebisha maeneo mengi sana, utajikamata ukiwa unafanya mambo yasiyo muhimu kwako na mara zote utakuwa na vipaumbele unavyofanyia kazi. Utaacha kufanya vitu kwa mazoea na kuiga wengine na utaanza kufanya vitu kwa umuhimu na kipaumbele.

Matendo yako yaendane na maneno yako, ndiyo njia pekee ya wewe kupata unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha