Msisitizo mkubwa wa zama hizi ni kufanya vitu rahisi, kutokujiumiza na kujichosha na kutafuta njia za mkato za kupata kile ambacho mtu anataka.

Njia nyingi katika hizi siyo sahihi, huwa zinaleta matokeo kidogo ya haraka lakini baadaye zinakuwa mzigo. Lakini hilo ni tatizo moja, lipo tatizo jingine kubwa zaidi ya hilo.

Tatizo hilo ni kukosa ile maana inayotokana na sisi kufanya vitu kama watu.

Angalia, msisitizo upo kwenye kurahisisha vitu, kufanya kwa haraka na kutokutumia nguvu kabisa.

Lakini sisi binadamu tunapata maana kwenye kile tunachofanya, pale tunapotatua tatizo kubwa ndiyo tunaona tuna uwezo mkubwa ndani yetu, na tunapata hamasa ya kufanya makubwa zaidi.

Kufuata ushauri na msisitizo unaotolewa na wengi, kwamba tusifanye kazi kabisa, tupate fedha kwa njia rahisi na siku nzima tupumzike tukizurura mitandaoni na kufanya yasiyo na maana, ni njia rahisi ya kukosa maana kwenye maisha na kukata tamaa.

Hata kama utapata fedha unayotaka, kama hutaona mchango unaotoa kwa wengine, utakuwa na utupu ndani yako ambao hautaweza kujazwa na fedha au chochote.

Tuondoke kwenye utamaduni huu wa sasa wa kukimbilia kufanya vitu rahisi na kutafuta njia ya mkato, tuache kutafuta njia ya haraka ya kukamilisha vitu, tuweke juhudi na muda kutatua matatizo makubwa tunayokutana nayo na yanayowakumba wengine. Ni kwa njia hii ndiyo tunatengeneza maana ya maisha yetu na kuridhika na kile tunachopata.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha