Washindi wote wana vitu vilivyopo ndani ya fikra zao ambavyo vinawawezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako na kupata kile wanachotaka.
Washindi wote wanaamini kwenye kile wanachofanya na wana uhakika wa kupata matokeo mazuri. Hawafanyi kwa kubahatisha au kutegemea muujiza, wanajua kile sahihi kufanya na kinacholeta matokeo sahihi.
Washindi wote wana uwezo mkubwa wa kufokasi, kuweka mawazo yao kwenye kile wanachofanya na kutokuruhusu usumbufu uingilie kazi zao. Wakati wengi wanahangaika na kila aina ya usumbufu, washindi wao wanajikinga na usumbufu na kufanya yale muhimu zaidi kwao.
Washindi wanamezwa na kile wanachofanya, wanaweka akili na nguvu zao zote kwenye kile wanachofanya kiasi kwamba wanasahau kabia mambo mengine yote. Wanasahau hata muda au kama wamekula au la, akili yao yote inaenda kwenye kile wanachofanya na siyo pengine. Hali hii inawapa mtiririko mzuri kwenye kazi zao na kuwaletea matokeo makubwa.
Washindi wanajua jinsi ya kutumia hisa zao na hata hisia za wengine kwa manufaa kwao kuweza kupata wanachotaka. Wakati wengine wanakuwa watumwa wa hisia zao na kuruhusu ziwapeleke zinavyotaka, washindi wanatawala hisia zao na kuzitumia kupiga hatua zaidi. Pia wanaposhirikiana na wengine, wanajua jinsi ya kuibua hisia sahihi kwa wengine zitakazowafanya wachukue hatua zaidi.
Washindi wamejitoa kweli kwenye kile wanachofanya, hawafanyi kwa kujaribu au kuangalia watapata matokeo gani. Wanafanya kwa uhakika wa kupata wanachotaka na hakuna kinachowazuia au kuwakatisha tamaa.
Wewe ni mshindi, anza kuishi maisha ya ushindi kwa kuzingatia haya muhimu unayopaswa kuyajenga kwenye fikra zako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,