“Who then is invincible? The one who cannot be upset by anything outside their reasoned choice.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.18.21

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari JINSI YA KUTOKUYUMBISHWA NA CHOCHOTE…
Mtu pekee asiyeyumbishwa na chochote ni yule ambaye haruhusu kitu chochote kilicho nje ya fikra zake kimvuruge.

Kwa sababu njia rahisi ya kuyumbishwa na kila kitu, ni kutaka kila kitu kiende kama unavyotaka wewe.
Pale unapotambua ya kwamba vitu pekee unavyoweza kudhibiti ni vile ambavyo vinatokana na fikra zako kwenyewe, unajipunguzia sehemu kubwa ya mzigo.

Unapotaka kila kitu kiende kama unavyotaka wewe, hapo unajiandaa kuangushwa, kwa sababu dunia haiendi kama unavyotaka wewe, bali inaenda kwa mipango yake yenyewe.
Dunia haijali hata kaka upo au haupo, na hata usipokuwepo leo, dunia itaendelea na mambo yake kama kawaida.

Tujifunze kuhangaika na yale yaliyo ndani ya fikra na maamuzi yetu na kuachana na yale ambayo yapo nje ya fikra na maamuzi yetu.

Ukawe na siku bora sana leo, siku ya kutokuyumbishwa na lolote, kwa kutoruhusu kilicho nje ya fikra zako kukusumbua.
#HangaikaNaYako, #DuniaHaiendiKwaMatakwaYako #DhibitiFikraZako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha