“We have the power to hold no opinion about a thing and to not let it upset our state of mind—for things have no natural power to shape our judgments.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 6.52

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari; SIYO LAZIMA UWE NA MAONI KWENYE KILA JAMBO…
Siku hizi, kila mtu ana maoni kwenye kila jambo linalotokea, iwe analijua jambo hilo kwa undani au halijui.
Wengi wamekuwa wanakimbilia kutoa maoni yao kama vile ni muhimu sana na yanayohitajika mno.

Hupaswi kuwa na maoni kwenye kila jambo, hata kwa yale yanayokuyokea wewe mwenyewe.
Usione vibaya kuacha mambo yapite bila ya kuweka maoni yako, kupuuza yale ambayo hayana umuhimu mkubwa kwako.

Kadiri unavyokazana kuwa na maoni kwenye kila jambo, ndivyo unavyopoteza muda na nguvu zako kwa mambo yasiyokuwa muhimu kwako, na ambayo hayako ndani ya uwezo wako kuyaathiri.

Una nguvu ya kujizuia kutokuwa na maoni kwenye kitu fulani, una nguvu ya kuzuia chochote kinachotokea kisivuruge akili yako.
Tumia vizuri nguvu hii ili upate utulivu wa akili yako na uweze kuitumia kwa yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

Kuwa tayari kusema sijui au sina maoni, kwa sababu siyo kila eneo maoni yako yanahitajika.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuepuka kuwa na maoni kwenye kila jambo.
#SiyoLazimaKuwaNaMaoni, #HangaikaNaYanayokuhusu, #TunzaNguvuZakoKwaYaliyoMuhimu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha