Rafiki yangu mpendwa,

Ipo kauli kwamba kila mtu anapenda kwenda peponi lakini hakuna anayetaka kufa. Kwa kifupi maisha ni mazuri, yawe magumu au rahisi, watu tunapenda kuishi zaidi na zaidi.

Na kitu kinachotusukuma kutunza afya zetu, kufanya mazoezi na kupata matibabu pale tunapougua ni kwa sababu tunataka kuishi zaidi. Tunataka kutoka kwenye utoto, kuwa watu wazima, kuwa na watoto na kuwalea mpaka wakue, na pia tupate wajukuu na wao pia tuwasaidie kukua na kuwa watu bora.

Pamekuwa na tafiti nyingi sana juu ya kuishi miaka mingi. Pamekuwa pia na matangazo ya dawa au vyakula fulani ambayo mtu akitumia ataishi miaka mingi zaidi. Lakini vitu vingi ambavyo vimekuwa vinatangazwa vya kumwezesha mtu kuishi miaka mingi, vimekuwa havifanyi hivyo kweli.

Badala yake kama mtu unataka kujua siri ya kuishi miaka mingi, unapaswa kuiangalia kwa wale ambao wameweza kuishi miaka mingi. Kama ambavyo ukitaka kujua siri za kupata utajiri, utawaangalia matajiri.

Mwandishi DAN BUETTNER kwenye kitabu chake cha THE BLUE ZONES; Lessons For Living Longer From The People Who’ve Lived The Longest, anatushirikisha siri za kuishi miaka mingi, kutoka kwa wale ambao wameweza kuishi kwa zaidi ya miaka mia moja.

Dan aliweza kufanya utafiti kwenye maeneo manne tofauti duniani, maeneo ambayo yana watu wengi waliofikisha miaka zaidi ya 100 ya maisha hapa duniani. Maeneo hayo ni Sardinia nchini Italy, Okinawa nchini Japan, Loma Linda Calfornia nchini Marekani na Nicoya nchini Costa Rica.

 

 

blue zone 3

Ukiangalia maeneo hayo manne yanatofautiana kijografia, kitamaduni na hata kiuchumi, lakini yote yameweza kuwa na watu wenye umri mkubwa zaidi duniani.

Kupitia utafiti wake wa muda mrefu, pamoja na kupitia tafiti nyingine nyingi zilizofanywa kuhusu watu wanaoishi miaka mingi, mwandishi ameweza kuja na SIRI TISA ambazo mtu yeyote akizijua na kuzifuata anaweza kuongeza miaka angalau kumi ya ziada kwenye maisha yake.

Hii ina maana kwamba kama ilikuwa ufe ukiwa na miaka 70, kwa kuishi siri hizi tisa utaishi mpaka miaka 80. Japokuwa hakuna uhakika wa asilimia 100 kwenye hili, kwa sababu afya zetu zinatofautiana na kuna vitu kama ajali, lakini kwa kuishi siri hizi tisa, maisha yako yatakuwa bora kuliko kutokuziishi siri hizi.

Karibu sasa ujifunze siri tisa za kuishi miaka mingi kutoka kwa wale walioishi miaka zaidi ya mia moja.

blue zones 2

SIRI YA KWANZA; UWEKE MWILI WAKO KWENYE MWENDO.

Mazoezi ya mwili ni siri ya kwanza ya kuishi miaka mingi. Katika utafiti wake, Dan aliweza kuona hili kwa kila aliyeishi miaka mingi. Watu hawa wamekuwa ni watu ambao kila siku miili yao iko kwenye mwendo. Siyo watu ambao wanakaa eneo moja kwa muda mrefu. Na licha ya kuwa na miaka zaidi ya 100, wengi bado walikuwa wanafanya majukumu yao wenyewe.

Na mazoezi ambayo yanakuwezesha kuishi miaka mingi siyo mazoezi magumu sana, bali mazoezi madogo madogo ambayo yanaufanya mwili utumie vyakula unavyokuwa umekula.

Katika kuiishi siri hii ya kuweka mwili kwenye mwenzo, zingatoa yafuatayo;

  1. Ondoa urahisi kwenye maisha yako. Hapa jisukume kutembea na kufanya kitu badala ya kutumia urahisi uliopo. Kwa mfano kama kuna ghorofa unapanda na kuna lifti na ngazi, wewe panda ngazi badala ya lifti. Kama unaangalia tv na uko mbali nayo, kama unataka kubadili chaneli au kuongeza sauti, badala ya kutumia rimoti amka na uende ukabadili mwenyewe. Mazoezi madogo madogo kama haya yanakusaidia sana.
  2. Fanya mazoezi kuwa kitu unachofurahia. Usifanye mazoezi magumu na ya kukuumiza, badala yake fanya mazoezi ambayo unayafurahia, kama kuna eneo la karibu unaloenda, badala ya kutumia gari basi tembea au nenda kwa baiskeli. Kadiri unavyopata nafasi kama hizi za kuupa mwili wako mazoezi, zitumie.
  3. Kuwa na muda wa matembezi kwenye siku yako. Kuwa na matembezi ya peke yako au pamoja na wengine kunaufanya mwili wako kuwa kwenye mwendo.
  4. Kuwa na mkutano wa kutembea. Kama kuna mtu ambaye unataka kuwa na mazungumzo naye, iwe ni ya kikazi, kibiashara au hata ya kindugu na kirafiki, unaweza kutumia mkutano huo kuwa sehemu ya mazoezi. Mnaweza kufanya mazungumzo yenu mkiwa mnatembea eneo tulivu na hii itakuwa msaada zaidi kwenu.
  5. Kuwa na bustani. Kwa kuwa na bustani ambayo unaihudumia kila siku ni zoezi tosha kwa mwili wako. Kupanda, kupalilia na hata kuvuna mazao kwenye bustani yako kunatosha kuupa mwili wako zoezi.
  6. Jiunge na darasa la yoga. Yoga ni mazoezi ya mwili yanayouwezesha mwili wako kuweza kuwa na usawa. Ukiweza kufanya zoezi hili la yoga angalau mara mbili kwa wiki inakusaidia sana.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kupata AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA Kwa Mwaka Huu 2019.

SIRI YA PILI; USILE MPAKA UKASHIBA KABISA.

Wajapani wana kauli yao huwa wanajiambia pale wanapoanza kula, kauli hiyo ni ‘hara hachi bu’ ikiwa na maana kula mpaka unapofikia asilimia 80 ya kushiba kisha acha.

Usile mpaka tumbo likajaa kabisa, badala yake kula mpaka pale unaposikia njaa imeisha na acha kula. Usile mpaka ukamaliza chakula chote, kula kwa kiasi na unapokaribia kushiba acha.

Kwa kufanya hivi utapunguza sana chakula kingi unachokula, ambacho hakiendi kutumika na mwishowe kinahifadhiwa kwenye mwili kama mafuta ambayo yanapelekea uzito uliopitiliza na kukaribisha magonjwa hatarishi.

Mambo yafuatayo yatakusaidia kula mpaka kufikia asilimia 80 na kutozidisha chakula.

  1. Pakua chakula ambacho ni asilimia 80 ya kile unachofikiri ukila utashiba kabisa. Kisha kula kiasi hicho cha chakula na usiongeze. Pia unapopakua chakula, nenda ukale mbali na kulipo chakula kilichobaki. Wengi husukumwa kuongeza chakula pale kinapokuwa mbele yako. Ondoa chakula cha ziada mbele yako.
  2. Kifanye chakula chako kuonekana kingi. Mara nyingi watu huongeza chakula pale wanapoona siyo kingi, hivyo ukipakua chakula kwa namna ambayo kinaonekana ni kingi, utaridhika nacho haraka. Mfano chakula kinapokuwa na mbogamboga na matunda kwa wingi, hutasukumwa kuongeza zaidi.
  3. Tumia sahani ndogo. Mara nyingi watu wamekuwa wanapakua chakula na kujaza sahani, kisha kula mpaka wamalize sahani hiyo. Kwa kutumia sahani au chombo ambacho ni kidogo, utapunguza sana kiasi cha chakula unachotumia.
  4. Jizuie kula vitu vidogo vidogo. Mara nyingi watu hujikuta wanakula vitu vidogo vidogo kama pipi, biskuti na kadhalika, ambavyo vinaishia kuongeza sukari mwilini. Fanya zoezi la kupata vitu hivi kuwa gumu kwako, kwa sababu vinapokuwa karibu yako vinavutia kula.
  5. Nunua vyakula kwenye ujazo mdogo. Unaponunua vyakula, nunu kwa ujazo mdogo badala ya ujazo mkubwa.
  6. Kuwa na mizani nyumbani kwako na kila siku pima kilo zako. Kwa kujikumbusha kila siku uzito wako kunakusukuma kuchukua hatua kuupunguza pale ambapo unakuwa mkubwa.
  7. Kula taratibu, unapokula kwa haraka unasahau ni kiasi gani umekula na unajikuta unakula zaidi. Lakini unapokula taratibu ni rahisi kujua kiasi cha chakula ulichokula na kuacha mapema.
  8. Usifanye kitu kingine wakati wa kula, usitumie simu wala kuangalia tv wakati unakula. Unapokula huku unafanya vitu vingine unajikuta unakula zaidi ya ulivyopanga kula.
  9. Kula ukiwa umekaa. Kula ukiwa umesimama au ukiwa unatembea kunapeleka ule zaidi.
  10. Kula mapema, chakula cha jioni kinapaswa kuwa chakula chepesi na kiliwe mapema kabla ya muda wa kulala.

SOMA; Kula Chakula, Siyo Kingi Sana Na Zaidi Mimea.

SIRI YA TATU; KULA MIMEA.

Chakula chako kinapaswa kuwa mimea zaidi. Epuka kula nyama na vyakula vilivyosindikwa. Watu wengi walioishi miaka zaidi ya 100 sehemu kubwa ya chakula chao ni mimea. Nyama wanakula kwa kiwango kidogo sana na mara chache.

Ili kuongeza mimea zaidi kwenye vyakula vyako, zingatia mambo yafuatayo;

  1. Kula mbogamboga na matunda mara nne mpaka sita kwa siku. Kwa kila mlo wa siku, kuwa na matunda na matunda.
  2. Punguza ulaji wa nyama, kama unaweza acha kabisa, kama huwezi kula siyo zaidi ya mara mbili kwa wiki na kula kiasi kidogo cha nyama.
  3. Weka matunda sehemu ambayo ni rahisi kuyaona na kuyatumia unapokuwa unaendelea na shughuli zako. Hili litakusukuma kutumia matunda zaidi.
  4. Kula kunde zaidi. Vyakula vya jamii ya kunde vina virutubisho vya kutosha kwa mwili wako, fanya hivi kuwa sehemu kubwa ya chakula chako.
  5. Kula karanga kila siku, vyakula vya karanga na jamii yake, kama korosho na lozi vina mafuta mazuri kwa mwili wako na tafiti zinaonesha vinapunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
  6. Kuwa karibu na karanga na vyakula vya jamii ya karanga ili iwe rahisi kwako kutumia mara kwa mara. Unaweza kuziweka kwenye chombo ambacho inakuwa rahisi kwako kutumia.

SIRI YA NNE; TUMIA MVINYO KWA KIASI.

Tafiti zinaonesha watu wanaotumia mvinyo kwa kiasi kila siku wanakuwa na afya bora na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo. Katika wale walioishi zaidi ya miaka 100, wengi wamekuwa na tabia ya kunywa mvinyo mwekundu, angalau glasi moja kwa siku. Mvinyo mwekundu unasaidia pia kupunguza sumu mwilini.

Mambo ya kuzingatia kwenye matumizi ya mvinyo;

  1. Tafuta mvinyo mwekundu ambao ni bora. Siyo kila mvinyo una faida zinazoelezwa. Mvinyo mwekundu ambao ni bora ndiyo wenye manufaa.
  2. Tenga muda wa mapumziko kwenye siku ambapo wewe pamoja na wengine mnaweza kupata kinywaji hicho cha mvinyo.
  3. Tumia kwa kiasi, glasi moja inatosha kabia, usinywe mpaka ukalewa.

SIRI YA TANO; KUWA NA KUSUDI LA MAISHA.

Kila ambaye ameishi kwa zaidi ya miaka 100 amekuwa na kusudi la maisha ambalo linaonekana ni kubwa kwake kuliko tu kusukuma siku. Wengi ambao wameishi miaka mingi wanajua nini kinawaamsha kila siku, wengi wamejipa majukumu kwa ajili ya familia zao na hata jamii zinazowazunguka.

Ili uweze kuishi miaka mingi, unapaswa kuwa na kusudi la maisha linalokusukuma kuamka kila siku. Kusudi hilo ndiyo litakuzuia usife mapema.

Ili kujua kusudi la maisha yako, fanya yafuatayo;

  1. Tengeneza maelezo ya dhumuni na kusudi la maisha yako. Jipe majibu ya maswali haya; je nini kinakusukuma kuamka kitandani kila siku asubuhi? Ni vitu gani unapenda sana kufanya ambavyo upo tayari kufanya hata kama hakuna anayekulipa? Ni vitu gani ambavyo wengine wanakusifia unafanya vizuri, vile ambavyo wengine wanapohitaji wanakuja kwako? Kwa kupata majibu ya maswali hayo, utajua kusudi la maisha yako.
  2. Kuwa na mtu ambaye atakusaidia kujua na kuishi kusudi la maisha yako. Huyu ni mtu ambaye anakuelewa na kuwa tayari kukupa moyo katika kuishi kusudi la maisha yako.
  3. Jifunze kitu kipya, kama mchezo mpya, lugha mpya au kutumia kifaa kipya cha muziki. Kwa kujifunza kitu kipya unaifanya akili yako kuwa vizuri na huenda ukapata kusudi lako kwenye kujifunza vitu vipya.

SOMA; Swali Moja La Kujiuliza Kila Siku Ili Kupata Hamasa Ya Kufikia Mafanikio Makubwa.

SIRI YA SITA; TENGA MUDA WA KUPUMZIKA.

Tunaishi kwenye dunia inayoenda kasi, dunia ambayo tuna mengi ya kufanya kuliko muda tulionao. Lakini hii ni kinyume na maisha ya wale ambao wameishi miaka zaidi ya 100, wengi wamekuwa wanatenga muda wa mapumziko kwenye siku yao. Wengi jioni baada ya kazi wanatenga muda wa kujumuika na wengine na kuondoa uchovu wa siku.

Kwa kupata muda wa kupumzika, unaondokana na msongo wa siku kitu ambacho kinaupa mwili wako afya.

Katika kupata muda wa kupumzika, fanya yafuatayo;

  1. Punguza kelele kwenye siku yako. Tunazungukwa na kelele nyingi kwenye siku zetu, tv, redio, simu, mitandao ya kijamii na kadhalika. Kadiri unavyokuwa na kelele nyingi ndivyo unavyochoka na kuwa na msongo. Tenga muda ambao unakuwa bila ya kelele za aina hii na utapata utulivu mzuri kwenye siku yako.
  2. Wahi kwa dakika 15. Kama kuna sehemu unaenda, basi jitahidi ufike dakika 15 kabla ya muda unaopaswa kufika. Kwa kuwahi kufika mahali unakuwa na utulivu kabla ya kile ulichoendea kuanza. Tofauti na unapofika ukiwa umechelewa, unakosa utulivu na kuwa na msongo.
  3. Kufanya tahajudi ni njia bora ya kutuliza akili na mwili, na tafiti zinaonesha tahajudi ina faida nyingi kiafya na kiakili. Tenga dakika 10 mpaka 30 kila siku za kufanya tahajudi na utaituliza akili na mwili wako na kuondokana na msongo.

SIRI YA SABA; JIUNGE NA JUMUIA YA KIIMANI AU KIROHO.

Wale ambao wameishi miaka zaidi ya 100, wanaonekana kuwa ndani ya jumuia za kidini, kiimani au kiroho. Wengi ni waumini wazuri ambao wanashiriki ibada za imani zao. Na hata wale ambao hawapo kwenye dini za kawaida, bado wana mifumo yao ya kiimani ya asili ambayo wanaishiriki kikamilifu.

Tafiti zinaonesha watu ambao ni waumini wa dini na wanashiriki ibada za dini zao mara kwa mara wanaishi miaka mingi kuliko wale ambao hawashiriki ibada. Na hakuna tofauti ni dini ya aina gani, kitendo tu cha kuwa kwenye imani na kushiriki ibada kinaongeza miaka kwa mtu.

Katika kuwa ndani ya jumuia ya kiimani au kiroho, zingatia yafuatayo;

  1. Jihuishe na shughuli zaidi za imani yako. Haitoshi tu kuwa muumini na kushiriki ibada, bali kushiriki zaidi shughuli za kiimani kunakuongezea miaka ya kuishi. Kuimba kwaya, kujitolea na mengine kama hayo yana manufaa zaidi.
  2. Tafuta jumuia ya kujihisisha nayo. Kama kwa sasa hauna dini au imani unayofuata, angalia kwenye jamii yako ni imani au jumuia gani ya kiroho unauweza kujihisisha nayo. Muhimu ni uwe ndani ya jumuia yenye kusudi kubwa kuhusu maisha na ushiriki kikamilifu. Hata kama ni klabu inayojihuisha na kutoa misaada kwa watu, itakusaidia.
  3. Hudhuria ibada. Tenga muda mara moja kila wiki na hudhuria ibada. Acha kila kitu na shiriki kwenye ibada unayohudhuria. Kitendo hichi ambacho ni kidogo sana kina manufaa makubwa sana kwako. Kwa kuweza kuachana na kila kitu kinachoendelea kwenye maisha yako na kushiriki ibada hata kama ni kwa saa moja tu kwa wiki, kuna manufaa makubwa kwako kiafya.

SIRI YA NANE; WEKA KIPAUMBELE KWA FAMILIA.

Wote ambao wameweza kuishi kwa miaka zaidi ya 100, wamekuwa na kipaumbele kikubwa kwa familia zao. Wengi wanakuwa wanaishi na familia zao, na hata wale ambao wanaishi wenyewe, wana muda wa kuwa pamoja na familia zao. Tafiti zinaonesha wazee ambao wanaishi na watoto wao wanaishi kwa muda mrefu kuliko wale wanaoishi wenyewe au wanaoishi kwenye vituo vya kulea wazee.

Familia ndiyo msingi mkuu wa maisha bora, ya kiafya na mafanikio. Wale wanaoweka kipaumbele cha kwanza kwenye familia wanakuwa na maisha marefu.

Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweka kipaumbele kwa familia;

  1. Weka mazingira ya kuwa karibu na familia. Kwa kuishi kwenye nyumba moja kunawafanya muwe karibu zaidi kama familia. Pia kuishi kwenye nyumba ambayo ni ndogo, ambayo wote mnaweza kuonana kila siku kuna manufaa zaidi.
  2. Kuwa na utaratibu wa familia, utaratibu ambao unawaleta pamoja. Mfano kuwa na mlo mmoja kila siku ambao mnakula kwa pamoja kama familia kunawafanya kuwa karibu kuliko pale ambapo kila mtu anakula kwa muda wake.
  3. Tengeneza eneo la kumbukumbu ya familia. Mnaweza kuwa na chumba au eneo ambalo kumbukumbu mbalimbali za kifamilia zinatunzwa. Mnaweza kuweka picha za matukio mbalimbali ya kifamilia. Mtu anapokuwa kwenye eneo hilo anapata kumbukumbu ya umoja wenu wa kifamilia.
  4. Weka familia yako mbele. Tenga muda wa kukaa na wale wa muhimu kwako, watoto wako, mwenza wako na hata wazazi wako. Mahusiano bora yanajengwa kwa muda na kujali.

SOMA; Ishi Kwa Tabia Hizi Kumi (10) Kila Siku Ya Maisha Yako Na Utaweza Kupata Mafanikio Makubwa Sana Kwenye Maisha Yako.

SIRI YA TISA; KUWA NDANI YA KUNDI SAHIHI.

Itakuwa vigumu kwako kuishi siri hizi za kiafya za kuweza kuishi miaka mingi, kama wale wanaokuzunguka wanaishi maisha ya hovyo. Kwa kifupi tunakuwa kama wale ambao wanatuzunguka. Hivyo ili uweze kuishi miaka mingi, unapaswa kuzungukwa na watu sahihi, ambao nao wanakazana kuishi maisha marefu.

Wale waliohojiwa kwenye utafiti wa kitabu cha BLUE ZONES, wameonekana kuwa na kikundi ambacho wamekuwa pamoja kwa muda mrefu. Kwa kuwa na kundi sahihi kwako, ambapo wote mna malengo sawa na mnasaidiana pale mmoja anapokwama, inakusaidia kuishi miaka mingi.

Zingatia yafuatayo katika kuwa na kundi sahihi kwako;

  1. Chagua kundi lako la ndani. Hawa ni wale watu watakaokuwa wa karibu sana kwako. Watu hawa wanapaswa kuwa na malengo na maono kama uliyonayo wewe. Angalia katika ndugu, jamaa na marafiki ulionao na chagua ni wapi ambao mnaweza kuwa karibu na mkasaidiana sana.
  2. Kuwa mtu unayependeka na kuwavutia wengine kuja kwako. Ili kuweza kuwa na kundi sahihi na kuwavutia watu sahihi, lazima kwanza uwe mtu ambaye unawavutia wengine kuja kwako. Hivyo jali kuhusu wengine na wao watajali kuhusu wewe.
  3. Tenga muda wa kuwa pamoja na kundi lako. Tenga angalau dakika 30 kila siku za kuwa pamoja na wale watu ambao wapo kwenye kundi lako la ndani. Kwa muda huu mnashirikishana yale yanayoendelea kwenye maisha yenu na hata kushauriana na kusaidiana pale mmoja anapokuwa amekwama.

Rafiki hizo ndiyo SIRI TISA za kukuwezesha wewe kuishi miaka mingi. Mambo haya siyo ya kubahatisha, bali ni namna ambavyo wale walioishi zaidi ya miaka 100 walivyoendesha maisha yao.

Kama unapenda kuishi maisha marefu, lakini pia maisha yenye afya, basi ishi misingi hii uliyojifunza hapa. Hakuna msingi hata mmoja unaokutaka utumie nguvu nyingi au uwe na fedha nyingi. Kwa kila msingi unaweza kuanzia hapo ulipo sasa na ukawa na maisha bora sana.

Mwandishi wa kitabu anamaliza kwa kutuambia, uchaguzi ni wetu, kama tunataka kuishi maisha marefu na yenye afya au kuishi maisha mafupi na yasiyo na afya.

Ni imani yangu wewe rafiki yangu, kwa kusoma mpaka hapa unataka maisha marefu na yenye afya. Hivyo ishi misingi hii na huenda tukakutana kwenye kilele cha miaka zaidi ya 100 ya maisha yetu.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu