Rafiki yangu mpendwa,

Kila mmoja wetu anapenda kuishi miaka mingi, na ndiyo maana kuna mpaka kichekesho kwamba kila mtu anataka kwenda mbinguni, lakini hakuna anayetaka kufa.

Tangu karne ya 20 na hii ya 21, umri wa maisha ambayo mtu anaweza kuwa nayo umekua unaongezeka. Kipindi cha nyuma umri ulikuwa chini sana, kwa sababu watu wengi walifariki utotoni kutokana na changamoto mbalimbali, za kiafya, kiuchumi, kimazingira na hata kisiasa.

Lakini kwa sasa sehemu kubwa ya changamoto hizo imetatuliwa, mfano kwenye afya upatikanaji wa urahisi wa madawa na chanjo mbalimbali kumepunguza sana vifo hasa vya utotoni. Kadhalika hali bora ya amani kwenye maeneo mengi imepunguza vita na mauaji kuwa chini.

generations_hero_0.png

Lakini pamoja na maboresho haya kwenye upande wa afya, mazingira, siasa na hata uchumi, vifo vya umri mdogo bado vimekuwa ni vingi. Na kwa sasa mambo yamebadilika, kinachowaua watu siyo tena yale magonjwa ya kuambukizwa ambayo watu hawakuwa na njia ya kuyazuia huko nyuma.

Bali kinachowaua watu kwa sasa ni magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, ambayo yanatokana na mtindo wa maisha na hivyo kuwa ni magonjwa ambayo mtu anaweza kuyaepuka kama atakuwa na mtindo bora wa maisha.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kujifunza mambo kumi muhimu ya kuzingatia ili uweze kuishi miaka mingi na kuwa na maisha bora.

Kabla hatujajifunza mambo hayo kumi, nianze na swali moja kwako, kama ukipewa uhakika huu, kwamba tarehe 31 mwezi wa 12 mwaka 2020 utafariki kwa ajali ya gari ukiwa morogoro, ni hatua zipi utakazochukua? Nina uhakika utafanya vitu viwili, kwanza utaepuka kuwepo morogoro kwenye tarehe hizo na pili utaepuka kuwa kwenye gari kwenye siku hiyo.

Hii ina maana kwamba ukishajua ni wapi ukienda au nini ukifanya utakufa, basi utaepuka kufanya kitu hicho.

Sasa kwenye mambo haya kumi tunayokwenda kujifunza hapa, ndiyo ambayo yanaweza kukuua, hivyo ukiyaepuka, utaweza kuishi miaka mingi na ukiwa na maisha bora.

SOMA; Siri Tisa (09) Za Kuishi Miaka Mingi Kutoka Kwa Watu Walioishi Miaka Zaidi Ya Mia Moja (100).

Bilionea Charlie Munger, mmoja wa watu wenye hekima sana kwa zama tunazoishi sasa, amewahi kunukuliwa akisema, kitu pekee ninachotaka kujua kwenye maisha ni wapi nikienda nitakufa na kuepuka kwenda hapo. Kwa sasa Munger ana umri wa miaka 95 na bado anajifunza na kufanya uwekezaji kila siku, hicho ni kiashiria kwamba ushauri wake unafanya kazi.

Kwenye kitabu kinachoitwa  How to Be the Luckiest Person Alive! Mwandishi James Altucher anatushirikisha maarifa mbalimbali ya kuwa na maisha bora na yenye mafanikio kwenye kila nyanja, kiafya, kifedha na furaha.

Kwenye moja ya sura za kitabu hicho, James ametushirikisha mambo haya kumi tunayokwenda kujifunza hapa.

Karibu ujifunze mambo kumi ya kuzingatia ili kuishi miaka mingi na kuwa na maisha bora.

  1. Usivute sigara.

Uvutaji wa sigara ndiyo kitu hatari zaidi unachoweza kufanya kwenye maisha yako.

Tafiti nyingi zimeonesha kwamba sigara ina zaidi ya kemikali 200 zinazosababisha saratani. Pia kila aina ya saratani, inachochewa zaidi na uvutaji wa sigara.

Uvutaji wa sigara pia unachangia sana kwenye magonjwa ya moyo, mishipa ya damu na hata magonjwa ya akili.

Kama haya unayojifunza hapa hayatoshi kukushawishi kuacha sigara, chukua pakiti ya sigara na soma nje, utakutana na maelezo haya; UVUTAJI WA SIGARA NI HATARI KWA AFYA YAKO. Hii ina maana kama utavuta, basi umechagua kufa mapema kabla ya muda wako.

  1. Usiwe mlevi.

Unywaji wa pombe kiasi umekuwa unashauriwa kiafya, japo pia kuna tafiti zinapinga hilo. Lakini kilicho kibaya kwenye pombe ni ulevi, kutumia pombe kwa kiwango kilichopitiliza kuna madhara makubwa kiafya.

Ulevi umekuwa unachangia magonjwa kama saratani, magonjwa ya moyo na hata magonjwa ya ubongo. Kadhalika ulevi umekuwa chanzo kikubwa cha ajali mbalimbali na hata kuvunjika kwa mahusiano muhimu.

Epuka kuwa mlevi, kama unapendelea kunywa, basi kunywa kiafya. Na kama hujui, kunywa kiafya ni kutokuzidisha bia mbili kwa siku kwa mwanamke na bia tatu kwa siku kwa mwanaume.

  1. Ufanyaji wa mapenzi.

Ufanyaji wa mapenzi una manufaa mengi kiafya na hata kiakili. Kwa maisha ya sasa, watu wamekuwa wanatingwa na kazi zao kiasi cha kukosa muda wa kufanya mapenzi, hasa ambao wapo kwenye ndoa. Tafiti zimekuwa zinaonesha wengi waliopo kwenye ndoa wanafanya mapenzi chini ya mara moja kwa wiki. Kiwango kinachoshauriwa ni angalau mara mbili kwa wiki.

Muhimu, hapa hakikisha unafanya mapenzi ambayo ni salama kwako, kwa sababu kuna hatari unazoweza kutengeneza na zikakatisha maisha yako kama hutakuwa makini kwenye hilo.

  1. Epuka vitu vitamu.

Uzito uliopitiliza ni chanzo kikubwa cha magonjwa kama shinikizo la damu (presha), kisukari na hata baadhi ya saratani. Chanzo kikuu cha uzito uliopitiliza ni kula vitu vitamu, ambavyo huwa tunavipenda sana.

Kuondokana na hili na ili uweze kuishi miaka mingi, epuka kabisa vitu vitamu. Futa kabisa sukari kwenye maisha yako. Vitu kama soda, juisi, biskuti na vitafunwa vingine ambavyo ni rahisi kula bila ya mpangilio achana navyo.

Na muhimu zaidi, punguza sana matumizi yako ya vyakula vya wanga. Kula zaidi mbogamboga, mafuta na protini. Wanga uwe kiwango kidogo sana na kwenye mlo mmoja wa siku yako.

SOMA; Sukari Ni Madawa Ya Kulevya Yaliyohalalishwa, Jihadhari Nayo Kama Unataka Kuwa Na Afya Bora.

  1. Fanya mazoezi.

Ufanyaji wa mazoezi unakuwezesha kutumia chakula ambacho umekula na hukitumii kutokana na mabadiliko ya maisha yetu, kwenye zama hizi, ambapo tunakaa zaidi kuliko kuusumbua mwili.

Unashauriwa kufanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku. Mazoezi yanaboresha afya, yanaleta furaha, yanaondoa msongo, na kukupa nguvu ya kutekeleza majukumu yako mengine.

Tafiti zinaonesha kama una magonjwa ya kisukari, presha na sonona, ufanyaji wa mazoezi unasaidia kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na matumizi ya dawa.

  1. Pata muda wa kutosha wa kulala.

Unapolala ndipo mwili unapata nafasi nzuri ya kufanya marekebisho kwenye maeneo ambayo umeumia au kuharibika. Hivyo kama unataka kuishi miaka mingi, hakikisha unapata muwa wa kutosha wa kulala na kupumzika.

Kiafya inashauriwa kupata masaa 7 mpaka 8 ya kulala kwa siku, chini ya hapo unatengeneza msongo ambao unakuwa na madhara kwako kiafya. Na pia kulala zaidi ya masaa 8 kuna madhara kiafya.

Ili kupata usingizi bora, lala eneo ambalo ni tulivu, acha kutumia mwanga wa simu, kompyuta au tv saa moja kabla ya kulala, mlo wako wa mwisho uwe masaa mawili kabla ya kulala, usitumie pombe au kahawa masaa 8 kabla ya kulala.

  1. Kujisaidia.

Hili linaweza kukushangaza na huenda hukutegemea, lakini kama unataka kuishi miaka mingi na kuwa na maisha bora, basi hakikisha unajisaidia (haja kubwa) kila siku. Unapojisikia haja ya kwenda kujisaidia, basi unapaswa kufanya hivyo. Choo kina uchafu na bakteria wengi, kadiri unavyokiacha mwilini ndiyo unavyotengeneza madhara zaidi ya kiafya.

Kiafya unashauriwa kupata choo angalau mara tatu kwa wiki, lakini ni bora zaidi kama utapata choo kila siku, kwa kuhakikisha unaondoa uchafu na kuacha tumbo yako ikiwa katika hali nzuri.

Ili kupata choo kila siku na kuepuka tatizo la kukosa choo, zingatia yafuatayo; unapopata choo kitoe hapo hapo, ukikiacha kinakuwa kigumu. Kula mbogamboga kwa wingi na matunda yenye nyuzinyuzi. Kunywa maji kwa wingi. Fanya mazoezi.

  1. Kuwa mtu wa shukrani.

Utaishi miaka mingi na kuwa na maisha bora kama hutakuwa na msongo wa mawazo au wasiwasi. Na moja ya vitu unavyoweza kufanya ili kuondokana na msongo na wasiwasi ni kuwa mtu wa shukrani.

Shukuru kwa kila jambo linalotokea kwenye maisha yako na angalia unawezaje kulitumia kwa ubora zaidi. Usiwe mtu wa kulalamika au kuangalia umekosa nini. Kuwa mtu wa kushukuru kile ulichonacho na kuangalia una nini na unawezaje kutumia kile ulichonacho.

Tafiti zinaonesha watu wenye mtazamo chanya wanaishi miaka mingi kuliko wale wenye mtazamo hasi.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu BULLETPROOF DIET (Mfumo Bora Wa Ulaji Utakaokuwezesha Kupunguza Uzito, Kuwa Na Nguvu Na Umakini Mkubwa Na Kuwa Na Afya Bora)

  1. Fanya mazoezi ya akili.

Kadiri umri wetu unavyokwenda, ndivyo ubongo wetu unavyochoka na kupoteza baadhi ya uwezo wake, ndiyo maana wengi hupoteza kumbukumbu umri unavyokwenda. Njia pekee ya kuondokana na hili ni kuipa akili yako mazoezi mara kwa mara. Kama ambavyo kufanya mazoezi ya mwili yanaimarisha afya, mazoezi ya akili yanaimarisha ubongo wako na kukufanya uwe na kumbukumbu nzuri kwa muda mrefu.

Baadhi ya mazoezi ya akili unayoweza kufanya ni kusoma vitabu vigumu, kukariri majina ya watu unaokutana nao, kukariri baadhi ya namba za simu unazotumia mara kwa mara, kucheza michezo inayohusisha akili, mara moja moja kutumia mkono ambao hujazoea kuutumia, mfano kama huwa unatumia mkono wa kulia zaidi, basi siku moja moja unajilazimisha kutumia mkono wa kushoto kwenye kila unachofanya.

Kama tulivyoona kwenye nukuu hapo juu, Charlie Munger ana miaka 95, lakini anasoma vitabu kila siku na anaendelea na uwekezaji. Ni watu wangapi unaowajua wenye miaka 80 mpaka 90 lakini hawana kumbukumbu sahihi? Fanya mazoezi ya akili yako, na utaweza kutunza kumbukumbu zako na hata uwezo wako wa kufikiri kwa muda mrefu.

  1. Epuka hospitali.

Hospitali ni sehemu ya kwenda kutibiwa, lakini mara nyingi imekuwa ni sehemu ya kwenda kupata magonjwa.

Tafiti zimekuwa zinaonesha kwamba watu wanaokwenda hospitali huwa wanapata magonjwa ambayo hawakuwa nayo, hasa yale ya kuambukizwa.

Hivyo kama unataka kuishi miaka mingi na kuwa na maisha bora, epuka hospitali. Na siyo kwa kugoma kwenda hospitali pale unapoumwa, bali kwa kujikinga ili usipate magonjwa. Ukifanyia kazi haya uliyojifunza hapa, hutakuwa na kitu cha kukupeleka hospitali na maisha yako yatakuwa bora.

Kumbuka, kinga ni bora kuliko tiba, hivyo weka juhudi zako kwenye kujikinga na magonjwa kuliko kuyatibu.

Mambo mawili ya nyongeza ambayo James anatushirikisha ni USAFI na KUEPUKA AJALI.

Kwenye usafi hakikisha mwili wako unakuwa safi, mavazi na malazi yako yawe safi na eneo lako la kazi liwe safi pia. Unapozungukwa na mazingira safi unaepuka magonjwa na changamoto nyingine za kiafya.

Epuka ajali kwa kupunguza safari zisizo na msingi, kama unaendesha gari usifanye kitu kingine kwa wakati mmoja, kama kuongea na simu au kaundika ujumbe huku unaendesha. Pia weka umakini kwenye kila unachofanya, vitu kama kuanguka, kujikata, kuungua huwa vinatokana na mtu kufanya kitu bila ya umakini.

Ukizingatia vitu hivi 12 ulivyojifunza hapa, utaweza kuishi miaka mingi na kuwa na maisha bora. Kama unatafuta siri ya kuishi muda mrefu, basi hujitaji kupoteza fedha zako kwenye kujaribu madawa mbalimbali, badala yake fanyia kazi mambo haya yasiyohitaji gharama za ziada na maisha yako yatakuwa bora sana.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha