Rafiki yangu mpendwa,
Mara kwa mara nimekuwa nasema maisha ni kama vita.
Kila mtu yupo kwenye mapambano ili kuweza kufanikiwa.
Lakini katika mapambano hayo, ni wachache ambao huwa wanaupata ushindi. Wengi huishia kushindwa na kuanguka vibaya.
Japokuwa wengi wanaoshindwa hutoa sababu nyingi za nje, kushinda au kushindwa huwa kunaanzia ndani ya mtu. Kunaanza kabla hata hajaingia kwenye mapambano.
Moja ya vitu muhimu vinavyochangia sana kwenye kushinda au kushindwa kwa mtu ni afya yake.
Na afya hii imegawanyi kwenye makundi matatu; mwili, akili na roho.
Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza mambo matatu muhimu ya kuzingatia kwenye afya ya mwili ili kufanikiwa.

Kwenye makala zinazokuja, tutaangalia pia afya ya akili na roho na jinsi ya kuziboresha ili kufanikiwa.
Afya ya mwili.
Mwili ndiyo hekalu la maisha yako, mwili ndiyo unaokupa nguvu ya kupambana ili ufanikiwe.
Mafanikio siyo rahisi, kuna kipindi yatakutaka ufanye kazi ngumu na kwa muda mrefu.
Bila ya afya imara ya mwili, hutaweza kuhimili msongo wa mafanikio na hilo litapelekea kushindwa.
Mambo matatu ya kuzingatia kwenye kujenga afya ya mwili.
Ili kujenga na kuimarisha afya yako ya mwili na uweze kupambana ili kufanikiwa, mambo haya matatu ni muhimu kuzingatia.
Jambo la kwanza ni ulaji ulio sahihi.
Unakuwa kile unachokula, chakula kinachoingia kwenye mwili wako kinajenga au kubomoa afya yako na hivyo kuathiri sana mafanikio yako.
Unapaswa kula kwa usahihi, vyakula vinavyoupa mwili nguvu na kinga ya kuweza kupambana na mambo mbalimbali.
Kuna sumu tatu kubwa unapaswa kuepuka kwenye ulaji.
Epuka vitu vyenye utamu, hivi vina sukari kwa wingi ambayo siyo nzuri kwa mwili.
Epuka vyakula vyenye weupe kwa wingi, hivi ni wanga ambao hauhitaji kwa wingi sana.
Epuka vitu vyenye kilevi cha aina yoyote, hivyo huuchosha mwili zaidi.
Vyakula unavyopaswa kuvipa kipaumbele ni vile vinavyotokana na mimea moja kwa moja au vinavyotokana na wanyama wanaokula mimea moja kwa moja.
Epuka vyakula vilivyochakatwa viwandani na kutunzwa kwa muda mrefu.
Mtu mmoja anayeshauri mambo ya ulaji amewahi kushirikisha msingi muhimu wa kula vyakula sahihi, anasema kama mtu aliyekufa karne ya 19 hawezi kutambua unachokula kama ni chakula basi usile.
Hapo anaonesha jinsi usindikaji wa vyakula viwandani ulivyochangia kuharibu ubora wa vyakula.
Jambo la pili la kuzingatia kwenye afya ya mwili ni mazoezi.
Sisi binadamu ni viumbe wa mwendo.
Kwa kipindi kirefu cha historia ya jamii yetu hapa duniani, shughuli nyingi tulikuwa tunafanya kwa mwendo na kuhusisha mwili mzima.
Chukua mfano wa kulima, kuwinda, kukusanya na mengine, yote hayo yalihusisha kazi kubwa kwenye mwili.
Lakini sasa mambo yamebadilika, kazi zetu nyingi siyo tena za kutumia mwili, bali kutumia akili.
Hilo linapelekea tukae kwa muda mrefu.
Na ukaaji kwa muda mrefu ndiyo hatari kubwa kiafya kwa zama hizi.
Kwa kuwa misuli ya mwili haifanyi kazi, sehemu kubwa ya chakula unachokula inahifadhiwa kwenye mwili, kitu kinachopelekea mtu kuwa na uzito uliopitiliza.
Uzito uliopitiliza unachochea mtu kupata magonjwa sugu kama presha na kisukari.
Kuondokana na hali hiyo, unapaswa kuupa mwili kazi, ambayo itahusisha misuli yote ya mwili.
Njia rahisi ya kufanya hivyo ni kupitia ufanyaji wa mazoezi.
Mazoezi ya mwili yanauweka mwili kwenye kazi, ambao unatumia chakula ulichokula na kile kilichohifadhiwa kwenye mwili pia.
Mazoezi yana faida nyingi mno, kuanzia kupunguza uzito wa mwili, kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza hatari ya magonjwa sugu.
Kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi angalau nusu saa kila siku. Mazoezi mazuri ni ya kukimbia kwa sababu yanahusisha misuli yote ya mwili. Na kama kukimbia huwezi, unaweza kuanza na kutembea na itakuwa ni afadhali kuliko kutokufanya mazoezi kabisa.
Jijengee utaratibu wako wa kufanya mazoezi na ufanyie kazi huo kila siku.
Jambo la tatu muhimu kuzingatia kwenye afya ya mwili ni kupumzika.
Ukisikiliza hadithi na hamasa nyingi za mafanikio, ufasikia watu wakijigamba kwamba wamekuwa wanakesha mara kwa mara au kulala masaa manne tu kwa siku, huku masaa 20 ya siku wakitumia kwenye kazi.
Hiyo siyo kweli, miili yetu siyo mashine. Unaweza kukesha kwa siku chache lakini siyo kila siku.
Mwili wako unahitaji mapumziko, na ukiyakosa hayo utakulazimisha upumzike kwa kukutengenezea ugonjwa.
Watu wengi sasa wamekuwa na uchovu uliopitiliza (burnout), kitu kinachowafanya wajione wanaumwa, ila wakipima hakuna ugonjwa wowote.
Usisubiri mpaka mwili ukulazimisha kupumzika, tengeneza utaratibu wako mwenyewe wa mapumziko.
Anza kwa kujua ni muda kiasi gani unaohitaji kulala ili mwili kuondokana na uchovu. Hili linatofautiana baina ga watu, lakini wastani ni kati ya masaa 6 mpaka 8. Jua kiasi ambacho mwili wako unahitaji na upatie.
Kitu cha pili ni kutenga muda wa kuwa peke yako na kujitafakari pamoja na kuyatafakari maisha yako.
Usigawe muda wako kwa kila mtu na kila kitu halafu ukajinyima wewe mwenyewe.
Ni muhimu mno uwe na muda wako kama unataka kufika kwenye mafanikio makubwa.
Rafiki, hayo ndiyo mambo matatu muhimu ya kuzingatia kwenye afya yako ya mwili ili uweze kuwa imara kwa mapambano ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Yafanyie kazi haya uliyojifunza ili yaweze kuwa na tija kwenye maisha yako.
Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz
