#TANO ZA JUMA #6 2019; Unajiibia Miaka 10 Ya Maisha, Jinsi Unavyoweza Kuishi Miaka 100, Siri Tisa Za Kuishi Miaka Mingi, Mchango Wa Fedha Kwenye Kuishi Maisha Marefu Na Ushawishi Wa Marafiki Kwenye Urefu Wa Maisha Yako.
Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye TANO ZA JUMA NAMBA 6 la mwaka huu 2019. Hongera sana kwa kumaliza juma hili la sita, juma ambalo nina imani limekuwa bora sana kwako na umeweza kukamilisha mengi uliyopanga kufanya.
Kwenye TANO ZA JUMA hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa THE BLUE ZONES; LESSONS FOR LIVING LONGER FROM THE PEOPLE WHO’VE LIVED THE LONGEST ambacho kimeandikwa na DAN BUETTNER.
Karibu sana kwenye tano hizi za juma ambapo tunakwenda kupata nafasi ya kujifunza kwa kina jinsi tunavyoweza kuwa na maisha marefu na yenye afya bora.
#1 NENO LA JUMA; UNAJIIBIA MIAKA 10 YA MAISHA YAKO.
Tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba asilimia 25 ya kinachopelekea ni miaka mingi kiasi gani unaweza kuishi inaathiriwa na jene zako, asilimia 75 inaathiriwa na mtindo wa maisha unaochagua.
Hii ina maana kwamba, sehemu kubwa ya matokeo unayopata kwenye maisha yako kiafya, na umri unaoishi hapa duniani, inachangiwa na mtindo wa maisha uliochagua kuishi.
Kwa aina ya maisha tunayoishi sasa, maisha ambayo shughuli nyingi ni za kukaa, ulaji ni wa vyakula vilivyosindikwa na vinavyoandaliwa haraka na maisha ambayo hatuna muda wa kufanya mazoezi, tunajiibia wenyewe miaka ambayo tungeweza kuishi.
Na ukikokotoa kwa wengi, unapata wastani wa miaka 10 ambayo wengi wanaipoteza. Yaani kama utakufa ukiwa na miaka 70, kama ungechagua kuishi vizuri basi ungefika miaka 80.
Rafiki, wakati sahihi wa kuchagua kuongeza miaka kumi kwenye maisha yako ni sasa, wakati huu ambapo bado una nguvu na afya yako haijaharibika sana. Unaweza kuchagua kuishi mtindo bora wa maisha leo na ukaongeza miaka kumi kwenye maisha yako.
Kujua mitindo bora ya maisha unayopaswa kuishi, soma kipengele namba tatu cha makala ya juma.
# KITABU CHA JUMA; JINSI UNAVYOWEZA KUISHI MIAKA 100.
Rafiki, juma hili la sita tunakwenda kujifunza kutoka kwenye kitabu kinachoitwa THE BLUE ZONES; LESSONS FOR LIVING LONGER FROM THE PEOPLE WHO’VE LIVED THE LONGEST ambacho kimeandikwa na DAN BUETTNER.
Hiki ni kitabu ambacho kimetokana na utafiti uliofanywa kwenye maeneo ambayo watu wanaishi miaka mingi zaidi duniani ukilinganisha na maeneo mengine.
Mwandishi wa kitabu hiki, Dan Buettner aliweza kutembelea maeneo manne na kujifunza kwa kina kutoka kwenye maisha ya wakazi wa eneo hilo, mazingira yao, mitindo yao ya maisha na mambo mengine ya kijamii ambayo yanaweza kuchagia watu hao kuishi miaka mingi ukilinganisha na watu wengine.
Pia aliweza kuwahoji watu ambao walikuwa wameishi miaka zaidi ya 100 huku wakiwa na afya bora na kuweza kuendelea na maisha yao, na wengi wakiwa bado wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kifamilia na kijamii.
Kupitia utafiti huu wa kina, Dan ametushirikisha mafunzo muhimu sana ya jinsi tunavyoweza kuishi miaka mingi.
Kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, nakwenda kukushirikisha masomo ambayo Dan anatushirikisha kutoka kwenye kila eneo ambalo lina watu wanaoishi miaka mingi. Na katika makala ya juma, nimekushirikisha SIRI TISA ZA KUISHI MIAKA mingi, ambazo ni mjumuisho wa masomo yote kutoka kwenye kitabu hiki.
Hivyo soma uchambuzi huu na pia hakikisha unasoma makala ya juma kwenye kipengele namba tatu ili kukamilisha somo lako la kuweza kuishi miaka mingi.
MAENEO YENYE WATU WANAOISHI MIAKA MINGI DUNIANI.
Kupitia utafiti wa mwandishi wa kitabu cha THE BLUE ZONES, yapo maeneo manne ambayo yameonesha kuwa na watu wanaoishi miaka mingi kuliko maeneo mengine.
Maeneo hayo ni kama ifuatavyo; Sardinia nchini Italy, Okinawa nchini Japan, Loma Linda Calfornia nchini Marekani na Nicoya nchini Costa Rica.
Hapa tutakwenda kujifunza masomo ambayo mwandishi ameondoka nayo kwenye kila eneo na jinsi ya kuyatumia kwenye maisha yetu ili tuweze kuishi miaka mingi.
MAMBO YA KUJIFUNZA KUHUSU KUISHI MIAKA MINGI KUTOKA SARDINIA.
Sardinia ni eneo ambalo lipo nchini Italia. Ni kisiwa ambacho kipo umbali wa maili 120 magharibi mwa Italia.
Sardinia ni moja ya maeneo ambayo watu wake wanaishi miaka mingi, na wengi wanavuka miaka 100 ya maisha wakiwa na afya njema.
Yafuatayo ni mambo ya kujifunza kuhusu kuishi miaka mingi kutoka kwenye maisha ya watu wa Sardinia.
- Kula chakula kinachotokana na mimea na nyama iwe kiasi kidogo.
Chakula cha kawaida cha watu wa Sardinia kina wanga, kunde, mbogamboga, matunda na mafuta yatokanayo na mimea. Pia wamekuwa wanatumia siagi inayotokana na kondoo, ambayo ina kiwango kikubwa cha mafuta ya omega-3, ambayo ni muhimu kwa ufanisi wa akili. Nyama huwa zinaliwa mara moja kwa wiki(jumapili) na kwa kiasi kidogo.
- Weka kipaumbele kwa familia.
Watu wa Sardinia wanaweka kipaumbele kikubwa sana kwenye familia. Familia zimekuwa zinaishi pamoja na hili linapunguza sana watu kuingia kwenye matatizo ya afya ya akili kama sonona, kujiua na hata msongo wa mawazo. Katika familia moja unakuta kuna wazee, watoto wao, wajukuu na hata vitukuu.
- Kunywa maziwa ya mbuzi.
Kikombe kimoja cha maziwa ya mbuzi kina virutubisho ambavyo vinasaidia kuepukana na magonjwa yanayotokana na umri mkubwa, kama magonjwa ya moyo na hata ugonjwa wa Alzheimer ambao ni changamoto sana kwa wazee.
- Heshimu na kufurahia kuwa na wazee.
Kwenye jamii nyingi wazee huonekana kama ni watu waliopitwa na wakati. Lakini kwenye jamii ya Sardinia, wazee wanaheshimiwa na kufurahiwa sana. Wazee ni nguzo muhimu kwenye familia yoyote ile. Hawa ndio wanaotoa mwongozo wa maisha na hata kuwalea wajukuu kwa misingi sahihi. Hili linaiwezesha familia kuishi kwa msingi mizuri ambayo inapelekea watu kuishi miaka mingi.
- Tenga muda wa kutembea.
Watu wengi wa Sardinia ni wafugaji, hivyo huwa wanatembea umbali mrefu kila siku kulisha mifugo yao. Hili linawafanya wawe imara sana kiafya na kutokuruhusu uzito wa mwili kuwa mkubwa. Kwa wastani wanatembea maili tano kwa siku, sawa na kilometa nane.
- Kunywa glasi moja au mbili za mvinyo mwekundu kila siku.
Watu wa Sardinia wamekuwa wanywaji wa mvinyo mwekundu kwa kiasi kila siku ya maisha yao. Mvinyo mwekundu una virutubisho ambavyo vinazuia mafuta kujikusanya kwenye mishipa ya damu. Pia mvinyo hupunguza msongo wa mawazo kwa wengi.
- Cheka na marafiki.
Watu wa Sardinia wana utani mwingi, kila siku wanakusanyika pamoja kwa ajili ya kutaniana na kucheka kwa pamoja. Uchekaji unapunguza msongo wa mawazo kitu kinachopunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
Hizi ndizo siri za kuishi maisha marefu kutoka kwa watu wa Sardinia, ambao wengi wao wameweza kuishi kwa zaidi ya miaka mia moja.
MAMBO YA KUJIFUNZA KUHUSU KUISHI MIAKA MINGI KUTOKA OKINAWA.
Okinawa ni eneo ambalo lipo nchini Japani. Okinawa ipo kwenye milima ya Ryukyu kati ya bahari ya Pacific na China. Ni eneo ambalo limeonekana kuwa na watu wengi wanaoishi kwa miaka mingi kuliko maeneo mengine yanayozunguka eneo hilo. Watu wengi kwenye eneo hili wameweza kuvuka miaka zaidi ya 100 ya maisha yao.
Yafuatayo ni mambo ya kujifunza kutoka kwa watu wa Okinawa ili kuweza kuwa na maisha marefu.
- Kuwa na kusudi la maisha yako.
Watu wa Okinawa wanaita hili ‘ikigai’, unapaswa kuwa na kitu kinachokusukuma kila siku, kitu ambacho kina msaada kwa wengine. Watu wa Okinawa wanajua kusudi la maisha yao na hilo linawafanya waendelee kuishi kwa muda mrefu, kwa sababu wanajua bado wanahitajika.
- Chakula chako kitegemee zaidi mimea.
Watu wa Okinawa wanakula chakula ambacho kinatokana na mimea zaidi ya wanyama. Wanakula zaidi viazi vitamu, mbogamboga na soya ambazo zinawafanya wawe na afya bora. Watu wa Okinawa pia wamekuwa wanakula nyama ya nguruwe, lakini ni mara chache sana, tena wakati wa sherehe mbalimbali.
- Kuwa na bustani.
Karibu watu wote walioishi zaidi ya miaka 100 Okinawa wana bustani au wamewahi kuwa na bustani kwenye maisha yao. Bustani inakuwa sehemu ya mazoezi ya kila siku kwa kuitunza kila siku na wakati huo pia inakuwa chanzo cha mbogamboga ambazo ni chakula cha afya.
- Kula soya zaidi.
Vyakula vya watu wa Okinawa vina soya kwa wingi. Virutubisho vilivyopo ndani ya soya vinasaisia kukinga magonjwa ya moyo na pia vinapunguza hatari ya kupata kansa ya titi. Pia soya iliyochachushwa ni nzuri kwa afya ya tumbo.
- Kuwa na kikundi cha marafiki mnaokutana pamoja mara kwa mara.
Watu wa Okinawa wanaita hili ‘moai’, ambapo watu wanakuwa na kikundi cha marafiki ambao wanakutana kila siku jioni kwa mazungumzo na kuwa pamoja. Kwa kuwa na kikundi cha aina hii inamsaidia sana mtu kupunguza msongo wa mawazo na hata kusaidiwa pale anapokuwa amekwama.
- Furahia jua.
Watu wa Okinawa wamekuwa wanatenga muda wa kukaa nje kwenye jua. Vitamin D ambayo inazalishwa na ngozi kutokana na jua huwa ni muhimu kwa mifupa imara na hata afya ya mwili.
- Uweke mwili kwenye mazoezi muda wote.
Watu wa Okinawa wanaweka miili yao kwenye mazoezi mara zote. Siyo watu wa kukaa eneo moja kwa muda mrefu. Wanatembea, wanatunza bustani zao na hata kwenye nyumba zao hawana samani nyingi. Wanakaa chini na kuinuka mara kwa mara na hilo linafanya miili yao kuwa imara kiafya.
- Kuwa na bustani ya kitabibu.
Watu wa Okinawa wana bustani maalumu kwa ajili ya mimea na miti shamba ambayo ni dawa na kinga. Kwa kuwa na bustani hizi na kutumia mimea hiyo kila siku wanaimarisha sana kinga zao za mwili na kujiepusha na magonjwa mbalimbali.
- Kuwa na mtazamo bora.
Wazee wa Okinawa wamepitia magumu sana kwenye maisha yao, hasa kipindi cha vita ya pili ya dunia, wengi walipoteza watoto wao na hata watu wa karibu. Lakini wote hawajachukulia hilo kama kikwazo cha maisha kwao. Badala yake wameachana nalo na kufurahia maisha waliyonayo kwa sasa. Kuwa na mtazamo sahihi wa maisha kumewawezesha kuishi miaka mingi, licha ya kupitia hali ngumu kwenye maisha.
Hizo ndiyo tabia zinazowawezesha watu wa Okinawa kuishi maisha marefu ukilinganisha na watu wengine wanaowazunguka.
MAMBO YA KUJIFUNZA KUHUSU KUISHI MIAKA MINGI KUTOKA LOMA LINDA.
Loma Linda ni eneo ambalo lipo kwenye jimbo la Calfornia Kusini nchini Marekani. Loma Linda ni moja ya maeneo ambayo watu wake wameonekana kuishi miaka mingi ukilinganisha na watu wengine wa maeneo ya karibu. Jamii hii ina watu wengi ambao ni waumini wa dini ya Wasabato na misingi yao ya kidini inaonekana kuwa na mchango kwao kuishi miaka mingi.
Yafuatayo ni mambo ya kujifunza kuhusu kuishi miaka mingi kutoka kwenye jamii ya watu wa Loma Linda.
- Tafuta utulivu kwenye muda.
Jamii ya watu wa Loma Linda ni Wasabato ambao wanaiishi misingi ya dini hiyo. Kila ijumaa jua linapozama mpaka jumamosi jua linapozama ni wakati wa sababu ambapo hawafanyi kazi yoyote ile. Badala yake wanatumia muda huo kumwabudu Mungu, kuwa pamoja na familia na watu wengine muhimu kwao. Kitendo hichi cha kupumzika kwa siku moja kila wiki kinawaondolea msongo wa mawazo, kuimarisha mahusiano yao ya kijamii na kuwapa mazoezi pia.
- Kuwa na uzito sahihi wa mwili.
Wasabato wengi wanakuwa na uzito sahihi wa mwili ukilinganisha na urefu wao. Wanafikia hilo kwa kuwa wafanyaji wa mazoezi na pia wengi siyo walaji wa nyama. Hili linawafanya wawe na shinikizo la damu ambalo ni dogo ukilinganisha na watu wengine, pia hawana mafuta mabaya kwenye damu zao na hatari ya magonjwa ya moyo kwao ni ndogo ukilinganisha na jamii nyingine.
- Pata mazoezi ya kawaida, ya mara kwa mara.
Utafiti uliofanya kwa jamii ya watu wa Loma Linda ambao ni wasabato unaonesha kwamba mtu anapaswa kufanya mazoezi ya kawaida ya mwili mara kwa mara badala ya kufanya mazoezi makali mara chache. Mazoezi kama kutembea kila siku yanachangia kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na hata baadhi ya saratani.
- Tenga muda wa kuwa na marafiki mnaonendana.
Wasabato huwa wanatumia muda mwingi na Wasabato wengine. Wanapata muda mzuri wa kushirikiana nao na hata kupata msaada pale wanapokuwa na changamoto mbalimbali.
- Kula karanga na jamii yake.
Wasabato wanaokula karanga na vyakula vingine vya jamii ya karanga kama korosho au lozi angalau mara tano kwa juma wana hatari ndogo ya magonjwa ya moyo na wanaishi miaka miwili zaidi kuliko wale ambao hawali karanga. Tafiti kubwa nne zimedhibitisha kuwa ulaji wa karanga na jamii zake una mchango mkubwa kwenye kuongeza urefu wa maisha.
- Kuwa mtoaji.
Kama ilivyo kwa imani nyingine, Wasabato wanahamasishwa na kupewa nafasi za kutoa na kujitolea kwa ajili ya wengine. Kwa kuwasaidia wengine, wanakuwa na kusudi kubwa la maisha yao na inawapunguzia kupata msongo wa mawazo na sonona.
- Kula nyama kwa kiasi.
Wasabato wengi siyo walaji wa nyama. Utafiti uliofanywa kupitia jamii hiyo ya Wasabato unaonesha ulaji wa matunda na mbogamboga una kinga dhidi ya baadhi ya saratani. Kwa wale wanaochagua kula nyama, wamekuwa wanakula kiasi kidogo sana na kama nyongeza kwenye chakula badala ya nyama kuwa chakula kikuu.
- Chakula cha usiku kiwe chepesi na kula mapema.
“Kula kifungua kinywa kama mfalme, chakula cha mchana kama mwana mfalme na chakula cha jioni kama ombaomba.” Hii ni kauli ya ushauri wa ulaji kutoka kwa Adelle Davis ambaye ni mtaalamu wa lishe. Hivi pia ndivyo Wasabato wanavyoishi. Ulaji wa chakula chepesi jioni na kula mapema kunazuia mwili kuwa na virutubisho vingi wakati wa kulala kitu kinachowazuia wasiwe na uzito mkubwa.
- Weka mimea zaidi kwenye mlo wako.
Wasabato ambao wanakula matunda mara mbili au zaidi kwa siku wanaonekana kuwa na hatari ndogo ya kupata kansa ya mapafu ukilinganisha na wale wanaokula matunda mara moja kwa siku, hata kama wote hawavuti sigara. Wale wanaokula jamii ya kunda mara tatu kwa juma wana hatari ndogo ya kupata saratani ya utumbo mpana. Wanawake Wasabato wanaokula nyanya mara tatu mpaka nne kwa wiki wana nafasi ndogo ya kupata kansa ya mifuko ya mayai ya uzazi. Ulaji wa nyanya kwa wingi unaonekana kupunguza hatari ya kupata saratani ya tezi dume kwa wanaume.
- Kunywa maji mengi.
Utafiti uliofanywa kwenye jamii hii ya Wasabato unaonesha wanaume wanaokunywa glasi 5 mpaka 6 za maji kila siku wana punguzo kubwa la hatari ya kupata shambulio la moyo ukilinganisha na wale wanaokunywa maji kidogo.
Rafiki, hivi ndivyo jamii ya watu wa Loma Linda ambao wengi ni Wasabato wanavyoyaendesha maisha yao na kuweza kuishi miaka mingi ukilinganisha na jamii nyingine inayowazunguka.
MAMBO YA KUJIFUNZA KUHUSU KUISHI MIAKA MINGI KUTOKA NICOYA.
Nicoya ni eneo ambalo lipo nchini Costa Rica. Hili ni moja ya maeneo ambayo watu wake wameonekana kuishi miaka mingi ukilinganisha na jamii nyingine zinazowazunguka. Katika kuwatembelea na kufanya utafiti, yapo mambo ambayo wameonekana kuyafanya kwa utofauti na yakachangia kwa wao kuishi miaka mingi.
- Kuwa na kusudi la maisha.
Watu wa Nicoya wanaita hili ‘plan de vida’, wanalijua kusudi la maisha yao na hivyo wanajua wanahitajika na wengine katika kutoa mchango na kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Hili linawafanya waishi miaka mingi kuliko wale ambao hawana kusudi la maisha.
- Kunywa maji magumu.
Maji wanayokunywa watu wa Nicoya ni maji magumu, ambayo yana madini ya kalshamu kwa wingi. Madini haya ni muhimu sana kwa uimara wa mifupa. Kwa utumiaji wa maji hayo wamekuwa na hatari ndogo ya magonjwa ya moyo na pia kuwa na mifupa imara ambayo haivunjiki kwa urahisi.
- Weka mkazo kwenye familia.
Wazee wa Nicoya wanaishi pamoja na familia zao na wajukuu na vitukuu wanawafanya wazee hao kujiona wana jukumu kubwa la kuwalea na kuwajengea misingi mizuri ya maisha, kitu kinachowasukuma kuishi miaka mingi.
- Chakula cha jioni kiwe chepesi.
Watu wa Nicoya wanakula chakula chepesi na mapema jioni, hili linawapa virutubisho vichache na kuongeza miaka kwenye maisha yao.
- Tengeneza mtandao wa kijamii.
Wazee wa Nicoya wanatembelewa mara kwa mara na majirani zao. Wanapata muda wa kuwa na wengine, kusikiliza, kucheka na kujali kuhusu wengine, hili linawapunguzia msongo na kuwapa maisha zaidi.
- Fanya kazi kwa nguvu.
Watu wa Nicoya wamekuwa ni wafanyaji wa kazi kwa nguvu na wanapenda kazi wanazozifanya. Hawaachi kufanya kazi kwa sababu umri umeenda, na kufanya kwao kazi kunakuwa sehemu ya mazoezi na sehemu ya kusudi la maisha, kitu kinachowapa miaka mingi zaidi.
- Pata jua.
Watu wa Nicoya wamekuwa wanahakikisha wanapata jua ambalo linasaidia miili yao kuzalisha vitamini D ambayo ni muhimu kwa mifupa na afya ya mwili. Upungufu wa vitamini D unahusishwa na matatizo mengi ya mifupa na magonjwa ya moyo.
- Furahia asili yako.
Watu wa Nicoya wanafurahia na kuishi asili yao ambayo imewasaidia kuishi maisha yasiyo na msongo. Vyakula vyao vya asili ambavyo ni mahindi na maharage yaliyoongezwa virutubisho vinaonekana kuwa na mchango mkubwa kwenye urefu wa maisha yao.
Hivi ndivyo watu wa Nicoya wanavyoweza kuishi miaka mingi ukilinganisha na jamii nyingine za watu wanaowazunguka.
Rafiki, hizi ndizo jamii nne ambazo maisha yao yamechambuliwa kwa kina kwenye kitabu cha THE BLUE ZONES, kama ukiangalia, baadhi ya vitu vinajirudia kwenye kila jamii.
Na pia hakuna kitu kigumu ambacho wewe huwezi kukifanya na ukaongeza miaka kwenye maisha yako. Kupata mpango wa kuishi ambao utakuwezesha kuongeza miaka zaidi kwenye maisha yako, soma kipengele namba tatu hapo chini cha SIRI TISSA ZA KUISHI MIAKA MINGI.
#3 MAKALA YA JUMA; SIRI TISA ZA KUISHI MIAKA MINGI.
Rafiki, kama unataka kupata kile ambacho wengine wamepata, hatua ya kwanza ni kujifunza kwa wale ambao tayari wana kitu hicho. Ndivyo tunavyofanya kwenye mafanikio na hata kwenye fedha.
Tunajifunza siri na misingi ya mafanikio kutoka kwa waliofanikiwa. Pia tunajifunza siri na misingi ya fedha kutoka kwa wale wenye fedha nyingi.
Sasa kama tunataka kujifunza siri za kuishi miaka mingi, tunapaswa kujifunza kutoka kwa watu gani? Hakuna tofauti, tunapaswa kujifunza kutoka kwa wale walioishi miaka mingi.
Kupitia kitabu cha juma hili cha BLUE ZONES, zipo siri tisa za kuweza kuishi miaka mingi kutoka kwa wale ambao wameweza kuishi miaka zaidi ya 100.
Na kwenye makala ya juma hili nilikushirikisha siri hizo tia. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo ya juma, unaweza kuisoma sasa hapa. Nakusihi sana usome makala hii kwa sababu ina mafunzo bora sana ambayo ukianza kuyafanyia kazi leo, utaongeza miaka kumi kwenye maisha yako.
Makala ya juma; Siri Tisa (09) Za Kuishi Miaka Mingi Kutoka Kwa Watu Walioishi Miaka Zaidi Ya Mia Moja (100). (https://amkamtanzania.com/2019/02/08/siri-tisa-09-za-kuishi-miaka-mingi-kutoka-kwa-watu-walioishi-miaka-zaidi-ya-mia-moja-100/)
#4 TUONGEE PESA; MCHANGO WA FEDHA KWENYE KUISHI MAISHA MAREFU.
Rafiki, fedha ina mchango mkubwa sana kwenye urefu wa maisha yetu. Watu wengi wamekuwa wanafikiria wenye fedha wanaishi umri mfupi kuliko wasio na fedha, lakini huu siyo ukweli.
Kwanza tukianza na historia ya dunia, kipindi cha nyuma ambapo umasikini ulikuwa mkubwa watu waliishi miaka michache sana, na watoto wengi walikufa kabla ya kufika umri wa miaka mitano. Na ndiyo maana watu walikuwa wakizaa watoto wengi, kwa sababu walijua wengi watakufa. Lakini baada ya dunia kuendelea na umasikini kupungua, umri wa kuishi umeongezeka sana, na kwa sasa watoto wengi wanazaliwa na kufika utu uzima. Haya yote yametokana na maboresho yaliyofanyika kwenye mfumo wa afya, kwa kuwepo kwa matibabu sahihi, chanjo na hata ulaji sahihi.
Tukija kwenye upande wa mataifa, iko wazi kwamba mataifa ambayo ni tajiri watu wake wanaishi miaka mingi ukilinganisha na mataifa masikini. Kwenye mataifa masikini ambapo wengi hawana uwezo wa kupata huduma bora za afya, kupata mahitaji muhimu kama chakula na malazi, watu wanakufa mapema.
Hivyo rafiki yangu, kwa lengo lako la kuishi miaka mingi, unapaswa kuweka kipaumbele kwenye fedha. Kwa sababu kama utaishi miaka 100, una zaidi ya miaka 20 ambayo utakuwa unaishi na huwezi kufanya kazi kubwa kwa sababu unapofika miaka 80, nguvu zako zinapungua sana.
Sasa kama unafika miaka 80, huwezi kufanya kazi kubwa halafu huna fedha, msongo tu wa mawazo, kwamba utayaendeshaje maisha yako, unatosha kukatisha maisha yako.
Hivyo kama una lengo la kuishi miaka mingi, anza kufanya uwekezaji sasa, uwekezaji ambao utakuwezesha kupata fedha za kuendesha maisha yako kwa zaidi ya miaka 30 hata kama hufanyi kazi inayokuingizia kipato moja kwa moja.
Pia kwa kuwa vizuri kifedha, utaweza kujihudumia vizuri kwa yale mahitaji muhimu na pia utaweza kumudu gharama bora kabisa za afya, ambazo ni ghali kuzipata.
Rafiki, nimalize kwa kusema fedha ina mchango mkubwa sana kwenye kuishi miaka mingi, hivyo ipe kipaumbele cha kwanza na kuwa na mipango bora ya uwekezaji ambao utaweza kukuzalishia baadaye hata kama hufanyi kazi.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; USHAWISHI WA MARAFIKI KWENYE UREFU WA MAISHA YAKO.
“The people you surround yourself with influence your behaviors, so choose friends who have healthy habits.” – Dan Buettner
Watu wanaokuzunguka wana ushawishi mkubwa sana kwenye tabia zako, hivyo chagua marafiki ambao wana tabia bora za kiafya.
Rafiki, huwa tunawachukulia marafiki zetu kirahisi sana, huwa tunaona tunakaa nao tu kwa muda na hawawezi kuyaathiri maisha yetu. Sasa leo nakuambia kwamba unajidanganya.
Tafiti zinaonesha kwamba kama una rafiki ambaye ana uzito uliopitiliza, na wewe pia una hatari kubwa ya kuwa na uzito uliopitiliza. Na hizi ni tafiti za kisayansi, zilizofanywa kwa kuwafuatilia wengi.
Angalia sana tabia za kiafya za marafiki unaochagua kuwa nao, kama wana tabia mbaya kiafya, tabia ambazo zinafupisha maisha yao, waepuke sana kama ukoma kwa sababu watakuambukiza tabia hizo na wewe utapunguza umri wako wa kuishi.
Kuwa na marafiki ambao wana tabia za kiafya zinazoongeza umri wa kuishi, wanakula kwa afya, wanakunywa kwa kiasi, wanafanya mazoezi na wanajua kusudi la maisha yao na kuliishi kila siku. Hawa ndiyo aina ya marafiki watakaokushawishi wewe kuwa na tabia bora pia na ukaishi miaka mingi.
Rafiki, hizi ndizo tano za juma la 6 la mwaka huu 2019, hapa umejifunza kwa kina sana jinsi unavyoweza kuishi miaka mingi kwa kuongeza angalau miaka 10 kwenye maisha yako. Umejifunza kwa wale walioishi miaka mingi, umejua umuhimu wa fedha kwenye urefu wa maisha yako na pia ushawishi wa marafiki kwenye umri utakaoishi. Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kuwa na maisha marefu na yenye afya tele.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu