Mara nyingi utawasikia watu wakilaumu ushauri ambao walipewa na watu wengine, pale wanapokuwa wameufanyia kazi halafu ukaleta matokeo ambayo ni tofauti na waliyotarajia.

Hapa unaweza kujiuliza je ushauri ni lazima ufanyiwe kazi, kwani mtu anapokupa ushauri anakuambia lazima uufanyie kazi? Majibu ni hapana, ushauri, na unapaswa kuutafakari kisha kuona kama unakufaa au la, na kama unaweza kuufanyia kazi au la.

Lakini wengi huwa wanapokea ushauri na kuufanyia kazi, bila ya kutafakari. Na sababu kuu ni moja, wanapenda kuwa na mtu wa kumlaumu baadaye.

Kwa mfano mtu anapopewa ushauri na akaufanyia kazi, halafu matokeo yakaja tofauti, hatajisikia vibaya kwamba yeye amekosea, badala yake anakuwa na mtu wa kumlaumu, yule ambaye amempa ushauri huo.

Lakini kama mtu huyo atapewa ushauri, akautafakari na kuamua kuchukua hatua zake mwenyewe, kama atashindwa, atajiona yeye ndiye amekosea na hilo litamuumiza sana yeye.

Wengi hawapendi kujiumiza, wengi hawapendi kukubali kwamba wameshindwa, hivyo wanapenda kuwa na mtu wa kumpa lawama zao.

Ondoka kwenye huu mtego ambao wengi wamekuwa wanajiingiza, usitengeneze watu wa kuwalaumu wengine pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea.

Jibebeshe jukumu la maisha yako na kila unachofanya kwa asilimia 100, kubali kwamba chochote kibaya au kizuri kinachotokea kwenye maisha yako ni wewe umesababisha kwa asilimia 100.

Kwa njia hii utachukua hatua sahihi na utajifunza kwa kila hatua unayochukua na hata kama utakosea, wakati mwingine utakuwa bora zaidi kwa sababu huna unayemrushia mzigo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha