Mpendwa rafiki,
Habari njema ni kwamba kila mtu ni kiongozi katika maisha yake. Kila mtu anajiongoza katika maisha yake licha ya kuwa na viongozi wanaotuongoza katika maeneo mbalimbali ya maisha yetu. Lakini wewe ndiyo kiongozi unajiongoza katika kila eneo la maisha yako.
Tukishindwa kujiongoza sisi wenyewe maana yake hatuwezi kuwaongoza hata wengine. kumbe basi, nidhamu ya uongozi bora unaanza na sisi wenyewe kwanza, tukiweza kuwa na nidhamu ya kujisimamia sisi wenyewe kwenye maisha yetu hata kuwaongoza wengine inakuwa rahisi sana.
Kuna watu katika maisha yao wamekuwa ni watu wa kusumwa kwenye kila kitu, yaani mtu anaishi kwa oda tu mpaka aambiwe fulani huu ni muda wa kuamka, kula na kufanya mengine. Ukishindwa kujiongoza na kuwa na nidhamu binafsi unakuwa mzigo kwako mwenyewe na kwa wanaokuzunguka. Hakuna maisha mazuri kama ya kujongoza na siyo maisha mabaya ya kutaka kuongozwa na kuambiwa kila kitu cha kufanya.
Sifa bora ya uongozi ambayo kila kiongozi anapaswa kuwa nayo ni usikilizaji. Kila kiongozi anapaswa kuwa msikilizaji. Kazi tunazofanya zinadai kusikiliza sana ili tuweze kuwahudumia vizuri wateja wetu kile tunachotaka. Unatakiwa uanze kujisikiliza wewe mwenyewe na kuwasikikiliza wengine wanafanya nini.
Bila kuwasikilizaji maana yake hakuna huduma ya uongozi tunayotoa. Na cha ajabu ni kwamba kila huduma tunayotoa inadai kuwa msikilizaji, kama wewe ni tabibu huwezi kutoa huduma kwa mgonjwa kama hujamsikiliza maelezo yake anaumwa nini. Huwezi kujua maendeleo ya watoto wako kama huwapi muda wa kuwasikiliza.
Kila kitu ni biashara duniani na kila biashara huwa ina mtoa huduma na mteja hivyo basi unatakiwa kumsikiliza sana mteja wako kile anachotaka mteja na siyo kile unachotaka wewe. Kwenye kila biashara mteja ndiyo mfamle kwa sababu yeye ndiyo analipa kila aina ya bili katika biashara yako. Kama una kazi halafu huna mtu wa kumhudumia basi hiyo siyo kazi tena.
SOMA; Hiki Ndiyo Kitu Hatari Sana Katika Uongozi
Kama wewe ni kiongozi basi kubali kutumika, na falsafa bora ya uongozi ni kwamba umekuja kutumika na siyo kutumikiwa. Hii ni falsafa bora sana, kwenye kila eneo la maisha yako jua kwamba umekuja kutumika na siyo kutumikwa.
Hatua ya kuchukua leo; Kama unataka kuwa kiongozi bora basi kuwa msikilizaji bora. Huwezi kuwa kiongozi bora kama huna sifa ya kusikiliza.
Kwahiyo, maisha yetu yanahitaji kusikiliza sana ili tuweze kuwasaidia wengine bila kuwa wasikilizaji tutashindwa kutimiza yale makusudi yetu duniani. Ili uweze kutimiza kusudi lazima kusudi hilo liwe ni la kuhudumia watu.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana