Sisi binadamu ndiyo viumbe pekee ambao tumepewa nguvu ya kuyabadili mazingira yetu na kuyatengeneza kwa namna tunavyotaka sisi wenyewe.
Viumbe wengine hawajapewa uwezo mkubwa kama tulionao. Mti ukishaota mahali utakaa hapo maisha yake yote, iwe ni mazingira mazuri au mabaya.
Simba akishazaliwa maisha yake yote yatakuwa ya uwindaji, hakuna kingine atakachofanya kwenye maisha yake. Kadhalika swala akishazaliwa, maisha yake yote atayatumia kuwakimbia wanyama hatari wanaotaka kumla.
Lakini sisi binadamu tuna uwezo mkubwa wa kubadili na kuboresha mazingira yetu na kutengeneza chochote tunachotaka. Uwezo huu mkubwa upo kwenye utambuzi wetu, uwezo wetu wa kufikiri kwa kina na siyo kupokea mambo kama yalivyo.
Kwa uwezo huu, mtu unaweza kufikiri kwa kina kabla hujachukua hatua yoyote na unaweza kubadili chochote kwa kuanza na fikra zako.
Na hili ndiyo linalotokea upande wa fedha, kama hupati kipato unachotaka, tatizo linaanzia kwenye fikra zako na siyo pengine. Huenda umefika hatua ya kukubaliana na pale ulipo sasa, na kwa kufanya hivyo unakuwa umechagua kurudi maisha ya chini kama ya wanyama.
Kwa kutumia uwezo wako wa kipekee, unaweza kutengeneza vitu vingi ambavyo huna kwa sasa. Unachohitaji ni kuanza kufikiri tofauti na utaweza kupata matokeo tofauti.
Hatua kuu ni mbili, amua ni nini unataka kutengeneza, kisha kitengeneze. Usiwe mtu wa kulalamika na kulaumu wengine. Kama kuna kitu huna kitengeneze, kama kuna kitu hukipendi kibadili. Usilalamike na kukaa kama huna cha kufanya, wewe siyo mti au mnyama, ndani yako kuna uwezo mkubwa sana, utumie vizuri na utapiga hatua sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,