Kama hujagundua hili ni kwamba fedha haina hisia, fedha haijali, kwa kifupi fedha haina upande.

Fedha ile ile ambayo mtu anaweza kumuua mtu akaiiba, anaweza kuipeleka kutoa sadaka na ikapokelewa bila ya shida yoyote, kwa sababu fedha haibebi alama yoyote kwamba imepatikana wapi.

Hili ni jambo muhimu sana tunalopaswa kuelewa kuhusu fedha na kufanyia kazi ili tusijizuie kupata fedha zaidi.

Kwa sababu kila wakati unapoweka hisia zako kwenye fedha, unajiweka kwenye nafasi ya kupoteza zaidi.

Angalia watu ambao wanaishia kupoteza fedha au kutapeliwa, unakuta kuna hisia ambazo wanakuwa wameingiza kwenye fedha ambazo zinaishia kuwagharimu.

Ukiwa na tamaa na fedha, utashawishika kuchukua hatua ambazo siyo sahihi na siyo tu utaishia kukosa fedha, bali pia utapoteza zile ambazo unazo kwa sasa.

Ukiwa na hisia za uhaba kwenye fedha, utahofia kuchukua hatua kwa kuogopa kupoteza fedha ulizonazo, na unaweza usipoteze, lakini hutapata zaidi.

Jukumu lako kubwa ni kuiona fedha kama fedha na kuondoa hisia zako zote unazoweza kuwa umeweka kuhusu fedha na hilo litaondoa vikwazo ambavyo unajiwekea katika kupata fedha zaidi.

Kumbuka msingi mkuu wa fedha, ni zao la thamani, hivyo weka nguvu zako kwenye kukazana kuzalisha thamani zaidi, achana na hisia nyingine zozote na utaacha kujizuia kutengeneza fedha zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha