Kusema ni rahisi, kupanga ni rahisi, lakini kuanza kuchukua hatua ni pagumu. Na hii ndiyo inapelekea wachache sana kuwa ndiyo wachukuaji hatua, na wachache zaidi kuwa wanufaikaje wa zile hatua wanazochukua.
Wengi wamekuwa wanaishia na maneno na mipango na wasichukue hatua. Zipo sababu nyingi zinazowazuia watu kuchukua hatua, lakini moja ni rahisi na wengi wamekuwa wanaanguka kwenye sababu hiyo bila ya kujua.
Njia rahisi ya kutokuanza chochote ni kutaka kila kitu kiwe sawa ndiyo uanze. Wengi, bila hata ya kujua, hutaka kila kitu kiwe sawa, mambo yote yaende kama wanavyotaka wao ndiyo waweze kuanza walichopanga kuanza.
Inapotokea maisha yamewaletea vitu vya tofauti, kitu ambacho kinatokea kwenye maisha ya kila mtu, wanaona bado hawajawa tayari kuanza, hivyo wanaahirisha, wakiamini hilo lililotokea likipita basi wataanza. Lakini kabla hawajamaliza hilo linatokea jingine, na jingine na jingine. Wanakuja kustuka miaka imeenda na hakuna walichofanya.
Rafiki, ninachotaka kukuambia ni kwamba hakuna wakati ambao kila kitu kwenye maisha yako kitaenda kama unavyotaka kiende, kila wakati kuna mambo yatakayotokea, ambayo hukuyatarajia na usipokuwa na msimamo yatakukwamisha kwenye mengi.
Watu wataumwa, utakoa fedha ulizotarajia kupata, uliokubaliana nao watakugeuka na mahitaji yako yataendelea kuua zaidi. Kusubiri mpaka ukamilishe kila kitu ndiyo uanze ni kujiweka kwenye nafasi ya kutokuanza.
Badala ya kusubiri mpaka kila kitu kiwe sawa, wewe anza, anzia pale ulipo sasa, na anza na kile ulichonacho sasa.
Kila mtu ana mahali anapoweza kuanzia, kila mtu anaweza kuanzia chini na akaendelea kukua kadiri anavyokwenda.
Jua yapo mambo yatakayotokea kwenye maisha, ambayo hukutegemea yatokee, lakini hayo yasiwe sababu ya wewe kutokuchukua hatua katika kufikia ndoto zako kubwa kwenye maisha.
Kumbuka sababu hazitaisha, ila muda unakwenda na nguvu zako zinapungua, usijisubirishe kwa sababu yoyote ile, chukua hatua, hakuna wakati ambao utakuwa umekamilika zaidi ya sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,