Rafiki yangu mpendwa,

Dunia inakwenda kasi sana, na maendeleo makubwa yanayotokea kwenye dunia, yamekuwa na manufaa makubwa kwa wachache, huku kwa wengi yakiwa hayana manufaa kabisa. Na kibaya zaidi, maendeleo haya yamewafanya baadhi ya watu kuwa watumwa wa maendeleo hayo na hivyo kuwa kikwazo kwao kufanikiwa.

Kwenye makala ya leo nakwenda kukushirikisha aina mpya ya utumwa ambayo imewashika wengi mateka na kuwazuia kufanikiwa. Kwa kujua utumwa huu, utaweza kujitoa haraka na kuwa huru na maisha yako ili uweze kufanikiwa.

Mwandishi na mwanahistoria Yuval Noah Harari kwenye kitabu chake kinachoitwa 21 LESSONS FOR THE 21ST CENTURY ametushirikisha changamoto 21 ambazo tunazipitia kwenye karne hii ya 21. Kwa kila changamoto ameeleza hali ya mambo ilivyo na kinachoweza kutokea kwa siku zijazo.

21 lessons yuval

Katika kitabu hiki, Yuval ameainisha changamoto mbili kubwa zinazotukabili ambazo ni maendeleo ya kiteknolojia, hasa upande wa TEHAMA na maendeleo ya kibaiolojia, hasa upande wa kuunganisha tehama na mwili.

Mwandishi anatuambia juhudi zinaendelea za kuweza kutumia mifumo ya taarifa na mifumo ya mwili ambapo itakuwa rahisi kwa kompyuta kuweza kuelewa mtu anafikiria nini, hisia zake zikoje na anahitaji nini. Hii ni hali ya juu kabisa ya maendeleo kwenye tehama na biolojia, lakini inakuwa na hatari kubwa moja ambayo ni iwapo taarifa za watu zitatumika vibaya, basi watu wataishia kuwa watumwa kwa wale wenye udhibiti wa taarifa zao.

Mwandishi anaeleza jinsi ambavyo makampuni makubwa ya zama hizi siyo yale yenye mali wala njia kubwa za uzalishaji, bali ni yale yenye taarifa za watu. Angalia mwenyewe makampuni makubwa ya teknolojia kama Facebook, Google, Amazon na mengineyo, kitu kikubwa ambacho kampuni hizi inamiliki ni taarifa za watu. Na makampuni hayo yanauza taarifa hizi kwa wafanyabiashara ili kuwatangazia watu kulingana na taarifa walizonazo.

Kama umekuwa makini na matumizi yako ya mtandao, utagundua ukiingia kwenye mtandao kutafuta kitu fulani, basi baada ya muda kila mtandao utakaotembelea unakuwa na matangazo yanayohusu kitu kile. Au ingia kwenye mtandao wa Youtube na angalia video moja, baada ya hapo utapendekezewa video nyingi zinazoendana na ile uliyoangalia. Haya hayatokei kwa bahati, bali kuna mfumo wa kompyuta ambapo unafanya kazi ya kuangalia machaguo yako, kisha unakuletea mapendekezo yanayoendana na kile unachotafuta au ulichoangalia.

socia-media-slave

Nafikiri unapata picha ni jinsi gani makampuni haya yenye taarifa zako yanavyoweza kuyatumia.

Mwaka 2017/2018 kampuni ya Facebook iliingia kwenye kashfa ya kuuza taarifa za watu kwa makampuni mengine. Katika kuhijiwa na Congress, mwanzilishi wa Facebook aliuliza, nyie huduma yenu watu wanatumia bure, je mnapataje kipato? Na bila kusita alijibu tunapata kipato kupitia matangazo. Na huu ndiyo ukweli. Makampuni haya ya teknolojia yanakuchukulia mtu siyo kama mteja, bali kama bidhaa.

Hii ina maana kwamba, unapotumia makampuni haya, hasa mitandao ya kijamii, wewe ndiye unayekuwa bidhaa ambayo wanaiuza na kupata faida. Na wanachouza ni taarifa zako ili wanataka kuzitumia wafanye hivyo. Unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo hatari, iwapo taarifa zako zitauzwa kwa watu wasio sahihi.

Na vipi pale ambapo taarifa zako kamili zitakuwa zimeunganishwa pamoja, yaani fikra zako, hisia zako na hata yanayoendelea kwenye mwili wako, yanapokuwa yameunganishwa pamoja, watu wenye taarifa zako wataweza kukuendesha kama roboti. Tunapaswa kuwa makini sana kama tunataka kuwa huru na kuepuka kuwa watumwa.

SOMA; Hasara Mbili Kubwa Unazopata Kwenye Mitandao Ya Kijamii (Na Kwa Nini Sipo Tena Kwenye Mitandao Ya Kijamii)

Mwandishi pia anatuambia dunia imekuwa inapitia hatua tofauti za maendeleo. Mfano kwenye zama za mapinduzi ya kilimo, ardhi ndiyo ilikuwa nyenzo kuu ya uzalishaji, hivyo waliokuwa na umiliki wa ardhi kubwa walikuwa watawala na wasio na ardhi wakawa watawaliwa.

Zikaja zama za mapinduzi ya viwanda, ambapo viwanda vilikuwa nyenzo kuu ya uzalishaji na waliokuwa na umiliki wa viwanda ndiyo walikuwa watawala, wasiokuwa na umiliki waliishia kuwa watawaliwa, wakifanya kazi kwenye viwanda kwa malipo kidogo.

agile-how-to-manage-change

Sasa tupo kwenye zama za mapinduzi ya taarifa, na mapinduzi haya ni makubwa kuliko hayo mawili ya nyuma. Kwa sasa wale wenye umiliki mkubwa wa taarifa za wengine ndiyo wanaokuwa watawala, na wasiokuwa na udhibiti, hata wa taarifa zao wenyewe wanaishia kuwa watawaliwa. Na huhitaji kuangalia mbali kuona hili, Facebook ina zaidi ya watumiaji bilioni 2.32 ambao wanatumia huduma hiyo kila mwezi, hii ni karibu theluthi moja ya watu duniani wanaotumia huduma hii. Hii ina maana kwamba kampuni moja ina udhibiti wa taarifa za zaidi ya theluthi moja ya watu duniani, hivi ndivyo utumwa mpya unavyotengenezwa.

Na unapoingia kwenye mitandao hii ndiyo unaona wazi jinsi ambavyo utumwa huu mpya unatengenezwa. Kwanza inakutengenezea utegemezi, kila mara unataka kuangalia nini kinaendelea, ukikaa muda mrefu bila kutembelea mitandao hii unaona kama kuna kitu umekosa. Na unapoingia, siyo rahisi kutoka, ukitaka kutoka unaletewa picha nzuri ya mtu unayemjua, unaiangalia, mara inakuja nyingine na nyingine na nyingine, ukija kustuka muda mwingi umetumia kwenye mitandao hii.

Hapo ni upande wa kushika umakini wako, sasa upande wa pili ni kuuza umakini huo. Ukiwa kwenye mitandao hii kuna matangazo mbalimbali unaletewa, matangazo hayo yanaletwa kwako kwa kuchakata taarifa zako na kuangalia unapendelea kufuatilia nini au kuna vitu gani unatafuta, na hivyo matangazo yanakuwa ya namna ambayo huwezi kuyakwepa. Kwa sababu ni vitu unavyofikiria muda mrefu au unavyotafuta. Ona jinsi utumwa huu mpya ulivyokuwa na nguvu ya kuwashikilia wengi mateka.

Taarifa za aina hii mpya ya utumwa zilianza kusambaa baada ya uchaguzi wa uraisi wa Marekani uliofanyika mwaka, ambapo ilikuja kugundulika mitandao hii, hasa Facebook ilitumika kuwashawishi watu kuchagua mtu fulani. Kabla ya kashfa hizi, watu waliona mitandao hii kama kitu cha kujiburudisha, lakini baada ya matumizi haya mabaya ya taarifa za watu, ndiyo watu wanaamka usingizini na kujaribu kudhibiti matumizi haya ya taarifa za watu.

Mwandishi anatuambia kwamba utumwa huu wa taarifa hauna tofauti na utumwa wa zamani. Anasema zamani wazungu walienda Afrika na kuwakuta watu wakiwa na ardhi kubwa na yenye madini. Waliwapa viongozi wa maeneo hayo shanga na vitu vingine vya urembo na watu hao wakawapa ardhi yenye madini na thamani kubwa.

Katika zama hizi, hatuwezi kuwacheka wale waliouza nchi zao kwa shanga na urembo, kwa sababu sisi wenyewe tumekuwa tunatoa taarifa zetu bure kabisa kwa kuambiwa tunapata nafasi ya kuunganishwa na wengine bila ya kulipia chochote. Lakini ambacho hatuelewi ni kwamba kwa kutumia huduma hizo bure, tunauza uhuru wetu. Wale tunaowapa taarifa zetu wanaziuza kwa wengine ambao wanatusukuma kufanya vitu kinyume na matakwa yetu.

Fikiria huduma zote unazotumia bure sasa, mitandao kama Facebook, Instagram, Whattsapp na mingineyo, yote hiyo inaendeshwa kwa gharama, lakini wewe hulipi chochote kuitumia, kwa sababu wewe ni bidhaa kwenye mitandao hii, wewe ni mtumwa ambaye unauzwa kwa wengine.

Rafiki, hii ndiyo aina mpya ya utumwa ambayo imewashikilia wengi mateka, utumwa wa taarifa, ambapo wachache wenye umiliki wa taarifa za wengine wanazitumia kuwatawala na kuwadhibiti.

Kama tusipoamka na kushika udhibiti wa taarifa zetu, tutaishia kutumiwa na wale wanaoweza kuzipata taarifa zetu kwa urahisi.

Je tunawezaje kuondokana na utumwa huu mpya?

Japokuwa wengi wameshachelewa, kwa sababu taarifa zao zimeshakusanywa na kusambazwa sana, bado ipo nafasi ya kushika udhibiti wa taarifa zako. Na hatua ya kwanza ni kujiondoa kwenye mitandao yote unayotumia ambayo inakusanya taarifa zako na kuuza kwa watangazaji. Mitandao yote ya kijamii ndiyo inavyofanya kazi, hivyo kama upo kwenye mitandao ya kijamii na hakuna kipato unachoingiza kutoka kwenye mitandao hiyo, ondoka mara moja. Angalau kama kuna kipato unaingiza unaweza kusema taarifa zako zinatumika vyema, lakini kama hakuna kipato, unaishia kutumiwa, ondoka mara moja.

Mtu mmoja amewahi kusema, kama kitu ni bure kuwa makini nacho, kuna namna unalipa. Na inapokuja kwenye hii mitandao, usifurahie ubure wake, jua mitandao hii inakugeuza wewe kuwa bidhaa na kukuuza kwa wale wenye uhitaji. Tunza sana taarifa zako na usizigawe hovyo kwa wale wanaokuahidi kukupa huduma za bure, wananufaika sana na taarifa zako kuliko wewe unavyonufaika na kile wanakupa bure.

Mwisho, nimegundua watu wengi wamesambaza taarifa zako kwenye maeneo mengi kiasi kwamba hata hawakumbuki wapi taarifa zao zinatumika. Ipo huduma ya kukuonesha taarifa zako umezisambaza wapi na pia kukuwezesha kujitoa kwenye huduma mbalimbali na kufuta taarifa zako. Unaweza kutumia huduma hiyo kwa kuingia hapa; www.deseat.me

SOMA; Hii Ndiyo Njia Rahisi Ya Kujiondoa Kwenye Mitandao Yote Ya Kijamii Unayotumia.

Ukiingia kwenye mtandao huo unaweka email yako na itakuonesha ni wapi ambapo taarifa zako umezisambaza, na unaweza kujitoa kwenye huduma hizo kwa kuchagua kudelete ile huduma ambayo hutaki iendelee kuwa na taarifa zako. Ni njia rahisi kwako kujiondoa kwenye itandao yote ya kijamii unayotumia.

Rafiki yangu, usikubali kuwa mateka kwenye aina hii mpya ya utumwa ambayo inakua kwa kasi, dhibiti sana taarifa zako na usikubali kuzitoa hivyo kwa ahadi ya kupata vitu vya bure. Kutoa taarifa zako ni kuwapa wengine nafasi ya kukutawala na kukutumia watakavyo.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge