#TANO ZA JUMA #9 2019; Uwazi Ni Nguvu Kubwa, Masomo 21 Kwa Karne Ya 21, Utumwa Mpya Uliowashika Wengi Mateka, Nguvu Ya Fedha Kwenye Karne Ya 21 Na Maadili Ni Kuelewa Mateso.
Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye tano za juma la 9 la mwaka huu 2019. Juma jingine zuri kwetu linakwenda kutuaga, tunachobaki nacho kwenye juma hili ni zile hatua tulizochukua na yale matokeo tuliyopata. Mipango yote mizuri ambayo tulikuwa nayo lakini hatukuifanyia kazi haijawa na maana yoyote.
Hivyo tujifunze kwamba kinachoacha alama kwenye maisha yetu siyo mipango tunayojiwekea, bali hatua tunazochukua. Hatua ndogo utakayochukua itaacha alama kuliko mipango mikubwa unayoweza kuwa nayo na usichukue hatua. Kuwa mtu wa kuchukua hatua na hutabaki pale ulipo sasa.
Kwenye juma hili la tisa tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa 21 Lessons for the 21st Century ambacho kimeandikwa na mwanahistoria Yuval Noah Harari. Kwenye kitabu hiki, Yuval amezichambua changamoto kubwa 21 zinazotukabili kwenye karne hii ya 21 na kupendekeza hatua tunazopaswa kuchukua ili tusiachwe nyuma na mabadiliko yanayotokea kwa kasi kubwa.
Karibu sana tujifunze kwa kina mambo matano makubwa ya juma hili, ambayo yanatokana na uchambuzi wa kina wa kitabu cha 21 Lessons for the 21st Century.
#1 NENO LA JUMA; UWAZI NI NGUVU KUBWA.
Tunaishi kwenye zama ambazo kuna mafuriko ya taarifa. Yaani maarifa na taarifa ni nyingi mno kiasi kwamba, badala ya maarifa na taarifa hizi kuwa msaada kwetu katika kufanya maamuzi, zinakuwa kikwazo. Hii ni kwa sababu unapokuwa na maarifa na taarifa nyingi, lakini ukakosa uwazi au ukashindwa kuzielewa kwa ubayana, unaishia kubaki njia panda, usijue ni hatua ipi ya kuchukua.
Wingi wa maarifa na taarifa zilizopo, unapelekea hali kubwa ya upinzani baina ya maarifa na taarifa. Taarifa moja inaweza kuwa inakuambia hiki, huku taarifa nyingine ikipingana na hicho cha mwanzo. Katika hali kama hii, ni vigumu sana kujua ni hatua ipi uchukue kama huna uwazi ndani yako.
Uwazi ni nguvu kubwa katika karne hii ya mafuriko ya maarifa na taarifa. Uwazi unaanza kwa kujijua wewe mwenyewe na kujua unataka nini kwenye maisha yako, kisha kuchagua taarifa na maarifa yanayoendana na kile unachotaka na kuachana na mengine. Ukijua kwamba unachochagua wewe siyo kitakachokuwa sahihi kuliko vingine vyote, bali ndiyo kitakuwa sahihi kwako kulingana na unachotaka kwenye maisha yako.
Upo usemi kwamba ukifa kwa kiu wakati umezungukwa na maji ni ujinga, lakini zama hizi watu wengi wanaangamia kwa kukosa maarifa, huku wakiwa wanazama kwenye mafuriko ya maarifa.
Kinachokosekana zama hizi siyo maarifa, bali uwazi. Unapaswa kuwa wazi kwako binafsi na kuwa tayari kuchagua kimoja na kuachana na vitu vingine. Jambo hili wanaliweza wachache, nina imani na wewe utakuwa mmoja wa hao wachache. Jua unachotaka kwenye maisha, chagua aina ya maarifa yanayoendana na kile unachotaka na achana na mengine yote.
#2 KITABU CHA JUMA; MASOMO 21 KWA KARNE YA 21.
Tunaishi kwenye ya 21, karne ambayo mabadiliko yanatokea kwa kasi kubwa sana. Kama hatutakuwa makini na kwenda vizuri na kasi hii ya mabadiliko, ndani ya muda mfupi tutaachwa nyuma. Na ubaya wa mabadiliko ya sasa ni kwamba yana nguvu kubwa ya kutugeuza binadamu kuwa watumwa, au kutufanya tukose maana kabisa.
Mwandishi na mwanahistoria Yuval Noah Harari amezichambua changamoto kubwa 21 za karne hii na kuja na mapendekezo ya hatua za kila mmoja wetu kuchukua ili kutokuachwa nyuma na kasi hii ya mabadiliko.
Mwandishi anaeleza wazi kwamba changamoto zote hizi zinatokana na mabadiliko makubwa mawili yanayoendelea.
Moja ni kwenye upande wa taarifa, ujio wa maroboti unatuweka kwenye hatari kubwa kwa sababu mifumo hii inaweza kukusanya taarifa zetu binadamu na kutusukuma katika kuchukua hatua mbalimbali. Tusipokuwa makini tutajikuta tunakuwa watumwa wa mifumo hii ya kiroboti inayotumika kuendesha huduma mbalimbali katika karne hii. Mfano mitandao ya kijamii inaendeshwa kwa mifumo hii ya roboti, ambapo kompyuta inafuatilia matumizi yako ya mitandao hiyo, na kuona ni vitu gani unapendelea kisha inakuletea aina hiyo ya vitu. Wewe unaweza kuona unakutana na habari fulani fulani na kujua hizo ni kweli, kumbe roboti limeshajua unapenda nini na linakuletea hayo tu.
Mbili ni mabadiliko ya kibaiolojia, kwa sasa wanasayansi wanakazana sana kuujua mwili wa binadamu na jinsi ya kuuboresha zaidi. Juhudi zinafanyika za kuweza kuunganisha mwili wa binadamu na mifumo ya kikompyuta, ambapo hutakuwa tena na haja ya kuhangaika wewe, bali mifumo ya kompyuta itaukagua mwili na kugundua matatizo mbalimbali na kupendekeza hatua za kuchukua. Mfano baadhi ya magonjwa yataonekana mapema kabla hayajaanza kuonesha dalili. Mwandishi anatuambia mtu utawekewa kadi kwenye mwili wako na mifumo ya kompyuta itaweza kusoma kila kitu kwenye mwili wako, mpaka hisia zao. Kama ukiwa na furaha mifumo hiyo itaelewa na kama ukiwa na huzuni pia itaelewa. Hili linaweza kuonekana ni jambo zuri na lenye manufaa kwa watu, lakini hatari yake inakuja pale watu wasio sahihi wanapopata nguvu ya kutumia taarifa hizi nyeti za watu.
Mwandishi anatoa mfano kwamba pale makampuni makubwa yanapopata taarifa zako za kibaiolojia, yataweza kukusukuma wewe kununua bidhaa mbalimbali wanazouza hata kama huna uhitaji nazo. Kadhalika serikali inapokuwa na taarifa zako, na ikawa siyo serikali nzuri, inaweza kuwageuza watu kuwa watumwa kwa kuzitumia vibaya taarifa zao. Mfano kwa kuwa na nguvu ya kubadili hisia za watu, serikali inaweza kuwafanya watu wafurahie wakati wote hata kama hakuna mazuri inafanya.
Hivyo changamoto kubwa kabisa kwenye karne hii ni namna tunavyodhibiti matumizi ya taarifa zetu. Maana hii ni karne ambayo mapinduzi makubwa ni ya taarifa, na wale wenye taarifa nyingi ndiyo wenye nguvu.
Yafuatayo ni masomo 21 ya karne hii ya 21 ambayo tunapaswa kuyazingatia ili tuwe na maisha bora na yenye uhuru.
SOMO LA 1; MWISHO WA HISTORIA UMEAHIRISHWA.
Sisi binadamu huwa tunafikiria kwa hadithi na siyo kwa ukweli, namba au maswali. Huwa tunapenda kufikiri kwa hadithi, na hadithi inapokuwa rahisi na inayoeleweka basi inakuwa bora zaidi. Katika kila zama ambazo tumepitia kama wanadamu, tumekuwa tunaishi kwa hadithi fulani. Tulipita kipindi cha kifashisti, ambapo hadithi kuu ilikuwa taifa moja ni bora kuliko mengine yote, na hii ilituingiza kwenye vita vya dunia. Tukaingia kipindi cha kikomunisti, ambapo msukumo ulikuwa kwenye watu kuishi kwa usawa na nchi kuwapa watu mahitaji yao, kwa tabia za binadamu, hadithi hii pia ikashindwa. Kwenye karne ya 21, dunia imeingia kwenye kipindi cha HURIA ambapo kila mtu yupo huru kuishi vile anavyotaka, bila ya kuingilia uhuru wa mwingine.
Tulipoingia kwenye kipindi hichi cha huria, wengi waliamini ndiyo mwisho wa historia. Kwamba kwa kuwa huria hakuna matatizo yoyote yatakayowasumbua watu na hakutakuwa na haja ya kuwa na kipindi kingine. Kwamba kama nchi itaendeshwa kwa demokrasia na watu wakawa huru kuishi wanavyotaka, maisha yatakuwa bora sana. Lakini tunaona dalili za kushindwa kwa mfumo huu zipo wazi wazi. Kwanza ni mataifa mengi ambayo yameshindwa kwa kufuata mfumo huu, mengi yameishia kwenye machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Pili ni mataifa makubwa ambayo yameacha kuifikiria dunia na kujifikiria yenyewe.
Kuingia kwenye mfumo huu huria siyo jawabu kwa matatizo yote ya binadamu, bali tunahitaji mfumo mpya ambao utaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na teknolojia ya kibaiolojia.
SOMO LA 2; UTAKAPOKUA HUENDA USIWE NA KAZI.
Zama zilizopita, mtu alikuwa anapata kazi moja na kudumu nayo maisha yake yote. Hii ni kwa sababu mabadiliko yalikuwa yanatokea kwa kasi ndogo sana hivyo wengi waliweza kudumu na kazi moja maisha yao yote. Na msukumo mkubwa ukawa kwenye kusoma na kuwa na taaluma ambayo itakuwezesha kuwa na kazi ya maisha.
Lakini katika karne hii ya 21, mabadiliko yanatokea kwa kasi kubwa mno, kazi nyingi zinapotea kila siku. Mifumo mipya ya teknolojia ya habari inaondoa uhitaji wa watu wengi kwenye kazi. Na hivyo wazo la kuwa na kazi ya maisha halipo tena. Maroboti yanaonekana kuchukua kila aina ya kazi ambazo zinafanywa na watu.
Njia pekee ya kukabiliana na hili ni kuwa tayari kubadilika kila wakati, kutokuishi na kufanya kazi kwa mazoea. Badala yake kujua mabadiliko yanaelekea wapi na kisha kuwa mbele ya mabadiliko hayo. Angalia kama kazi au biashara unayofanya sasa inaathiriwa na mabadiliko yanayoendelea kwenye teknolojia ya habari na baiolojia, kisha chukua hatua mapema.
Mfano mzuri ni kwenye biashara ya taksi, wapo watu ambao wamekuwa kwenye biashara hii kwa muda mrefu, ikaja huduma ua uba ambayo inamwezesha kila mtu kutoa huduma ya usafiri wa teksi, hii ikaathiri sana wale waliotegemea hii kama biashara yao kuu. Sasa ambacho kitaleta athari kubwa zaidi ni pale magari yanayojiendesha yenyewe yatakapokuwa yanatoa huduma za teksi, hakutahitajika kabisa uwepo wa dereva. Kama hujui ni kwamba tayari yapo magari yanayojiendesha yenyewe. Huu ni upande mmoja tu wa kazi ya udereva, lakini kila kazi inaathiriwa na mabadiliko makubwa yanayotokea. Mfano mpaka operesheni kwenye miili ya binadamu kubwa zinaweza kufanywa na maroboti na umakini mkubwa kuliko zinavyofanywa na madaktari wanadamu.
Using’ang’ane na kazi au biashara uliyonayo sasa, mambo yanabadilika kwa kasi, badilika pia.
SOMO LA 3; UNAFUATILIWA KWA KARIBU KULIKO UNAVYOFIKIRI.
Kipindi cha nyuma, wakati wa ukoloni, mataifa makubwa yalikuwa yanapigania kushika ardhi kwenye nchi nyingi. Na hili lilizalisha ukoloni. Kwenye karne ya 21, kuna aina mpya ya harakati kwa mataifa makubwa na hata kampuni kubwa. Katika karne hii makampuni haya yanapigania kupata taarifa za watu, kadiri kampuni au nchi inavyokuwa na taarifa nyingi kuhusu mtu, na kwa watu wengi, ndivyo inavyoweza kutumia taarifa hizi kuwasukuma watu kuchukua hatua fulani.
Makampuni makubwa kama Google, Facebook, Amazon, Alibaba, Cocacola na mengineyo yapo kwenye harakati kubwa za kukusanya taarifa nyingi za watu. Kwa kadiri yanavyokuwa na taarifa nyingi ndivyo yanavyowasukuma watu kutumia huduma zao. Kadhalika kila taifa linakazana kupata taarifa zaidi za watu wake na hata watu wa mataifa mengine.
Hivyo jua ya kwamba unafuatiliwa kwa karibu kuliko unavyofikiri. Unapoingia mtandaoni na kufanya mambo yako, jua kuna mifumo ya kikompyuta inayokufuatilia kwa kila unachofanya na kujifunza kuhusu wewe, unapendelea nini na kadhalika.
Tunakoelekea, na hili limeshaanza kuonekana, google na facebook zitakujua wewe vizuri kuliko unavyojijua wewe mwenyewe. Hali hii ni hatari kwa sababu itafika wakati tutaiamini mifumo hii ifanye maamuzi kwa ajili yetu na hapo tutakuwa tumechagua utumwa mbaya sana. sasa hivi karibu kila mtu anafanya maamuzi kwa kutumia google. Kama kuna kitu unataka kujua, unauliza google. Kama kuna mahali unataka kwenda lakini hupajui, ukiuliza google unapewa mpaka ramani ya kufika.
Tunapaswa kuwa makini na taarifa tunazotoa kwa mifumo hii. Tunapaswa kuweka nguvu kubwa kwenye kujiendeleza sisi wanadamu, kukuza ufahamu wetu ili tusiishie kuwa na mifumo yenye uwezo mkubwa na wanadamu tukabaki na uwezo mdogo. Kwani tukifikia hatua hii, tutakuwa tumekubali kuwa watumwa kwa vitu tulivyotengeneza wenyewe.
SOMO LA 4; ANAYEMILIKI TAARIFA ANAIMILIKI KESHO.
Dunia imepitia zama mbalimbali, zama za kilimo waliomiliki ardhi ndiyo waliokuwa watawala na waliomiliki uchumi. Katika zama za viwanda, waliomiliki viwanda ndiyo waliomiliki uchumi. Na sasa tupo kwenye zama za taarifa, wale wanaomiliki taarifa ndiyo wanaomiliki uchumi na wanaimiliki kesho pia.
Zama hizi za taarifa zinatoa uwezo mkubwa sana kwa yeyote anayemiliki taarifa. Wale wenye taarifa na wanaoweza kuzitumia, wanaweza kupiga hatua zaidi kuliko wasiokuwa na taarifa.
Hivyo unapaswa kuhakikisha una taarifa sahihi na kuzitumia vizuri kupata kile unachotaka. Pia kudhibiti taarifa zako binafsi zisiende kwa wale ambao wanaweza kuzitumia vibaya na kukugeuza wewe kuwa mtumwa wao. Miliki kesho yako kwa kuwa na taarifa muhimu za kile unachofanya, na epuka sana kutoa taarifa zako binafsi kwa wengine, hasa mitandao ambayo inakusanya taarifa za watu na kuziuza kwa wanaotangaza bidhaa na huduma mbalimbali.
SOMO LA 5; UMUHIMU WA JUMUIYA.
Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, tumezoea kuwa sehemu ya jamii kubwa. Kupona kwetu kama binadamu ni kwa sababu tuliishi kama jamii tangu enzi na enzi. Jamii ilikuwa msaada kwa wote, wale wenye nguvu na uwezo na wasiokuwa na nguvu na uwezo.
Katika karne ya 21 tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kuvunjika kwa jumuiya nyingi, kuanzia za watu binafsi mpaka za mataifa au kitaifa. Tumeona baadhi ya mataifa yaliyokuwa yameungana kutaka kuvunjika na mengine kuachana. Tumeona baadhi ya mataifa yakitaka kugawanyika.
Na katika maisha binafsi hali ndiyo mbaya zaidi, ile nafasi ya watu kukutana ana kwa ana kama jamii imepungua sana. Sasa hivi watu wamekuwa wanakutana zaidi mtandaoni. Na hata watu wanapopata nafasi ya kuwa pamoja, bado muda mwingi wanautumia kwenye kitandao ya kijamii, badala ya kutumia kwa mazungumzo ya pamoja.
Tunapaswa kurejea kwenye misingi ya jumuiya, kwa kuimarisha ushirikiano wetu na wengine, hasa wa ana kwa ana. Kwa sababu utegemezi wetu mkubwa kwenye teknolojia na mitandao ya kijamii umeleta hali ya kutengwa ndani yetu. Tafiti nyingi kwa sasa zinaonesha kiwango cha msongo na sonona kinaongezeka kwa wengi kwa kukosa nafasi ya kuwa ana kwa ana na wengine na kutegemea zaidi mitandao ya kijamii.
SOMO LA 6; KUNA USTAARABU MMOJA TU DUNIANI.
Dunia imepitia vipindi tofauti tofauti ambapo kila jamii ilikuwa na ustaarabu wake na namna ya kufanya mambo yake. Pia ndani ya jamii kumekuwa na mgawanyiko wa watu kulingana na dini au makabila yao. Hivyo ndani ya jamii moja bado kulikuwa na ustaarabu wa aina tofauti tofauti.
Lakini karne ya 21 mambo yamebadilika sana, kuna ustaarabu mmoja tu duniani, na jamii zote zinaishi kwa ustaarabu huo. Na hili limerahisisha mwingiliano baina ya jamii tofauti. Ukichukulia mfano wa michezo ya Olympic, ambayo inahusisha nchi zote duniani, kinachowezesha michezo hii kuwezekana ni kuwepo kwa ustaarabu ambao unakubalika na kila nchi.
Ukiangalia kila nchi ina bendera yake, kila nchi ina wimbo wake wa taifa, kila nchi ina sarafu yake, ambayo inaweza kubadilishwa na sarafu ya nchi nyingine.
Hali hii ya kuwepo kwa ustaarabu mmoja duniani inapelekea pia matatizo yanayotokea kwenye jamii moja kuathiri jamii nyingine. Hivyo tunapaswa kufikiri namna ambavyo kila tunachofanya kinavyoathiri wengine pia na siyo kujiangalia sisi wenyewe.
SOMO LA 7; MATATIZO YA KIMATAIFA YANAHITAJI MAJIBU YA KIMATAIFA.
Kama tulivyoona kwenye somo la sita, sisi binadamu ni viumbe wa kijamii na kwa sasa dunia nzima inakuwa kama jamii moja. Hii ni kwa sababu changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa haziwezi kuathiri nchi moja na hakuna nchi moja inayoweza kutatua changamoto hizo.
Na changamoto kubwa sana zinazoweza kuathiri dunia kwa ujumla ni vita ya kinyuklia na mabadiliko ya hali ya hewa. Iwapo itatokea vita na silaha za kinyuklia kutumika, sehemu kubwa ya dunia itaathirika. Na mabadiliko ya hali ya hewa yana athari kwa sehemu kubwa ya dunia.
Licha ya matatizo haya kuwa ya dunia nzima, miaka ya karibuni tunaona mataifa yakitaka kujitenga na kutokujihusisha na mataifa mengine. Uingereza kujitoa kwenye umoja wa ulaya na hata Marekani kutenga ukuta baina yake na Mexico, hizi ni juhudi za kujenga utaifa, lakini zina madhara kwa dunia.
Changamoto tunazokabiliana nazo ni za kimataifa na zinahitaji majibu ya kimataifa. Utaifa hautakuwa na msaada kwa taifa husika wala dunia kwa ujumla. Hivyo ni muhimu ushirikiano baina ya mataifa ukaimarishwa ili kutatua changamoto hizo kwa pamoja.
SOMO LA 8; MUNGU ANATUMIKIA TAIFA.
Kwa kipindi kirefu dini zimekuwa na nguvu kubwa sana kwenye jamii. Katika zama zilizopita dini na serikali zilikuwa kitu kimoja, viongozi wa dini ndiyo waliokuwa wakileta utatuzi na suluhisho la changamoto mbalimbali ambazo watu walikuwa wanapotia. Kama mvua hazikunyesha basi viongozi wa dini walifanya ibada au kutoa kafara na miungu ikajibu kwa kunyesha mvua.
Lakini katika karne ya 21 dini zimepoteza nguvu hiyo ya kutatua changamoto kubwa za kijamii. Lakini bado dini zimebaki na nguvu kubwa ya kuweza kuwaleta watu pamoja. Watu wana imani kali kwenye dini na wengi wapo tayari kufanya chochote kwa jina la dini zao.
Tumeona watu wakifanya hata uhalifu kwa kisingizio cha kutetea dini zao. Kwa sasa mataifa yanayotaka kujitenga na kujenga utaifa, yanatumia nguvu ya dini katika kuwaleta watu pamoja. Hivyo dini zinakuwa chombo cha mataifa kuimarisha nguvu zao.
Katika karne hii lazima tuelewe kwamba matatizo makubwa tunayokutana nayo hayawezi kupata majibu kwa kutegemea dini pekee. Lazima tujue kwamba kujitenga kwa mataifa kwa mwavuli wa dini kutazidi kutengeneza matatizo makubwa duniani.
SOMO LA 9; BAADHI YA TAMADUNI NI BORA KULIKO NYINGINE.
Uhamiaji ni changamoto nyingine kubwa sana katika karne hii. Tangu enzi na enzi, kumekuwa na mwingiliano baina ya jamii, watu kutoka eneo moja kuhamia eneo jingine. Na mwingiliano huo ndiyo ulioweza kusambaza maarifa na ujuzi baina ya jamii hizo.
Lakini katika karne ya 21, uhamiaji umekuwa changamoto, baadhi ya mataifa yamekuwa yanaogopa kupokea wahamiaji kutoka kwenye mataifa mengine, wakiamini wahamiaji hao wanaenda kufurahia matunda ya wenzao huku wao wakiwa wameshindwa kutengeneza mazingira bora kwenye nchi zao.
Wale wanaozuiwa kuingia kwenye mataifa wanayotaka kuhamia nao wanayalaumu mataifa hayo kwa ubaguzi wa rangi au dini. Na sehemu kubwa ya watu wanafikiri changamoto kwenye uhamiaji ni rangi au dini. Lakini changamoto kubwa ipo kwenye utamaduni.
Tafiti zote za kisayansi zimeonesha kwamba hakuna tofauti yoyote ya kibaiolojia baina ya mtu mweusi na mtu mweupe, au mtu wa dini moja na mtu wa dini nyingine. Hivyo tunachotofautiana watu ni utamaduni ambao umejengwa ndani yetu. Tabia tulizonazo ni matokeo ya yale ambayo tumekuwa tunafundishwa na kusisitiziwa tangu tukiwa wadogo.
Hivyo tunapoangalia eneo la uhamiaji, tujue tunasumbuka na utamaduni na siyo rangi wala dini. Pia lazima tukubali kwamba tamaduni zinatofautiana na kila utamaduni una mambo mazuri na mabaya.
SOMO LA 10; TUSIWE NA HOFU YA UGAIDI.
Hofu kubwa inayowatawala watu kwa sasa, kuanzia uongozi wa jumuia za kimataifa, uongozi wa nchi na hata mwananchi mmoja mmoja ni ugaidi. Magaidi wameweza kutumia hofu zetu wenyewe kututawala.
Tukio kubwa kabisa la kigaidi ambalo limetokea kwenye karne ya 21 ni la Septemba 11 2001, lakini baada ya hapo matukio yanayofuatia ya kigaidi ni madogo mno.
Kwa mfano kwa mwaka watu 25,000 wanauawa kwenye matukio ya kigaidi, na hili linatupa taharuki kubwa sana kwamba ugaidi ni hatari kubwa ya dunia. Lakini angalia hizi namba nyingine za kifo; kwa mwaka watu 1,250,000 wanakufa kwa ajali duniani, watu zaidi ya milioni 3 wanakufa kwa kisukari, na uchafuzi wa hali ya hewa unaua watu zaidi ya milioni 7.
Ukilinganisha vifo vya ugaidi na vifo vingine, utaona namna ambavyo ugaidi unasababisha vifo vichache, lakini wote tunahofia sana ugaidi kuliko ajali au kisukari. Ugaidi unatumia hofu zilizopo ndani ya watu kuwaumiza wao wenyewe. Kwa kutokuwa na uhakika na kutokujua ni wakati gani tukio la kigaidi linaweza kutokea, watu wanakuwa na hofu mara zote.
Pia magaidi wanatumia hofu hii kuyasukuma mataifa kusaidia kazi zao. Kwa mfano kama kikundi cha kigaidi kinataka kuishambulia nchi ya Iraq lakini hakina uwezo wa kijeshi, kinachofanya ni kuendesha vitendo vya kigaidi kwenye nchi kama ya Marekani kwa mgongo wa Iraq, kisha taifa hilo linataharuki na kuvamia nchi ya Iraq. Hivyo kazi ya kikundi cha kigaidi inakuwa imekamilika bila ya wao kuingia kwenye vita, ni kama wanasaidiwa.
Hivyo kitu sahihi kufanya kwenye ugaidi ni kutokuwa na hofu na kwa taifa kutokutaharuki. Hii haimaanishi mataifa yasipambane na ugaidi, bali mataifa yawe na utulivu badala ya kutaharuki na kuzalisha matatizo zaidi, kama ilivyotokea mashariki ya kati.
SOMO LA 11; USICHUKULIE POA UPUMBAVU WA MWANADAMU.
Changamoto nyingine kubwa kwenye karne hii ni vita. Japo hakuna vita kubwa ambayo imewahi kuwepo hapa duniani tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia, bado vita ni changamoto kubwa.
Na kwa sasa vita ni changamoto kubwa kwa sababu uwezo mkubwa wa kijeshi na uwepo wa silaha za maangamizi ni hatari sana kwa dunia nzima. Iwapo itatokea vita ya tatu ya dunia, basi maangamizi yake yatakuwa makubwa sana kwa dunia nzima.
Hivyo tunaweza kusema kwamba uwezo huu wa maangamizi unaweza kuwa kitu cha kutupa hofu tusijihusishe na vita, lakini tusichukulie poa upumbavu wa mwanadamu.
Tangu enzi na enzi, binadamu tumekuwa wazuri katika kutengeneza zana bora, lakini hatuwezi kuzitumia vizuri. Hivyo tunapaswa kuwa na njia bora ya kuhakikisha maendeleo makubwa tuliyofikia hayawi chanzo cha kuondoa maisha duniani.
Njia bora kabisa ya kuzuia upumbavu wa mwanadamu usiwe angamizo kwa dunia ni kwa watu kujifunza unyenyekevu na kujali wengine. Ile dhana kwamba taifa letu ni bora kuliko mataifa mengine au dini yetu ni bora kuliko dini nyingine ndiyo imekuwa chanzo cha vita nyingi. Kama watu watajifunza kwamba kila mtu ni muhimu na kila mtu ni bora, ushirikiano utakuwa mzuri na hapatakuwa na vita.
SOMO LA 12; WEWE SIYO KITOVU CHA DUNIA.
Unyenyekevu ni changamoto nyingine kubwa kwa karne hii ya 21. Watu wengi wamekuwa wakiamini wao ndiyo bora kuliko wengine, kuanzia kwenye ngazi ya jamii, dini na hata taifa. Hali hii ya kujiona wa muhimu kuliko wengine ndiyo imezalisha matatizo makubwa sana hapa duniani. Kuanzia mapigano ya kikabila, machafuko ya kidini na hata vita vya dunia.
Ukweli ni kwamba mataifa na hata dini ni vitu vilivyotengenezwa na wanadamu, na havina miaka mingi ukilinganisha na muda ambao wanadamu wamekuwa hapa duniani. Tafiti zinaonesha binadamu ameishi hapa duniani kwa zaidi ya miaka milioni moja, lakini dini yenye umri mkubwa sana ni miaka elfu 3 tu, na mataifa mengi hayana hata miaka elfu moja ya kuwa kama taifa. Hivyo ukilinganisha uwepo wa binadamu na uwepo wa hizi taasisi, binadamu wamekuwepo muda mrefu. Hivyo kufikiri dini au taifa fulani ni bora kuliko upande mwingine ni kujidanganya.
Tunapaswa kuwa na unyenyekevu na kuelewa kwamba taasisi zote zinazotuleta pamoja hazina nguvu kutushinda sisi wanadamu. Taifa, dini na hata taasisi nyingine, ni vitu ambavyo vilitengenezwa na watu, hivyo vina uimara wake na madhaifu yake, kusema upande mmoja ni bora kuliko mwingine na kutaka kuonesha hilo, ndiyo upumbavu wa mwanadamu ambao huleta madhara makubwa kwa dunia nzima.
SOMO LA 13; USILITAJE BURE JINA LA MUGU.
Changamoto nyingine kubwa katika karne hii ya 21 ni uwepo wa mungu. Mjadala kama mungu yupo au la umekuwepo miaka na miaka, lakini katika zama zilizopita haukuwa unapata nguvu kwa kuwa majibu ya matatizo ya wengi yalikuwa yanatolewa na viongozi wa kidini. Kama mtu aliumwa alienda kuombewa au kufanyiwa uganga na akapona. Kama mvua haikunyesha basi watu waliomba na wengine kutoa kafara na mvua zikanyesha. Na pale ambapo watu walioombewa hawakuponea, au mvua haikunyesha baada ya maombi au kafara, ilionekana mungu alikuwa na hasira sana na kuamua kuwaadhibu watu wake.
Lakini zama hizi tuna uelewa mkubwa wa matatizo mbalimbali na namna ya kuyatatua. Ukiumwa unajua utakwenda hospitali kupata tiba, na hata kama utaombewa, lakini bado utategemea tiba ya kisayansi. Kama mvua hainyeshi tunajua kuna uchafuzi wa mazingira unaobadili hali ya hewa.
Maendeleo haya yamepunguza sana nguvu ya dini katika kutoa suluhisho la matatizo mbalimbali.
Lakini pamoja na hayo, bado jina la mungu limekuwa linatumika katika maeneo ambayo halipaswi kutumika. Amri ya tatu katika amri kumi za mungu inasema usilitaje bure jina la bwana mungu wako. Wengi wamekuwa wanachukulia amri hii kama kutokutamka jina la mungu kila wakati, lakini kama amri hii ukiitafakari kwa kina inamaanisha usimtumie mungu kama sababu ya wewe kufanya unachotaka kufanya. Tumekuwa tunaona nchi zinaingia kwenye vita kwa kisingizio cha kutetea jina la mungu, au watu kugombana na wengine kwa kumtetea mungu. Kama unataka kufanya mambo yako fanya, lakini usiyahusishe na jina la mungu. Kama mungu yupo ana majukumu makubwa ya kuiendesha hii dunia kuliko kukutegemea wewe uue wengine au kutesa wengine ili kumfurahisha yeye.
SOMO LA 14; TAMBUA KIVULI CHA MFUMO WA KIDUNIA.
Baada ya dini kushindwa, kutokana na machafuko mengi kuhusishwa na dini, njia bora ya kuendesha nchi na hata jamii imekuwa ya KIDUNIA, kwa kutokuegemea upande wowote wa dini. Hapa taifa linakuwa halina dini, ila mwananchi mmoja mmoja ana uhuru wa kuchagua dini yake na haruhusiwi kuingilia dini ya mwenzake.
Huu ni mfumo bora na ambao umeleta utulivu kwa nchi nyingi duniani, pia umetoa uhuru kwa wengi. Kwa sababu katika mataifa yanayoendeshwa kwa sheria za dini, kila mtu inabidi akubaliane na wengine wote, hata kama hana imani hiyo. Mfano kama wewe ni Mkristo na unaishi kwenye nchi inayoendeshwa kwa sheria za Kiislamu, hutaruhusiwa kula hadharani wakati wa mfungo wa Ramadhani.
Moja ya misingi muhimu sana kwenye kuishi kidunia ni kutafuta ukweli na kuutumia ukweli kama kigezo cha kufanya maamuzi, kitu ambacho kwenye dini hakipo. Dini nyingi zinaendeshwa kwa imani na siyo ukweli. Ukitaka kuhoji ukweli kwenye dini utaambiwa unakosa imani.
Kwa kutambua kivuli cha udunia na kutumia ukweli kama msingi wa kufanya maamuzi kunaufanya mfumo wa kidunia kuwa bora katika uongozi na ushirikiano kuliko mfumo wa kidini.
SOMO LA 15; UNAJUA KIDOGO KULIKO UNAVYOFIKIRI.
Kwa kuwa tunaishi kwenye zama za taarifa ambapo maarifa yanapatikana kwa urahisi, watu wengi wamekuwa wanafikiri wanajua sana. Watu wamekuwa wakiamini wanafikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi. Lakini tafiti zinaonesha huo siyo ukweli. Maamuzi mengi tunayofanya tunatumia kundi, kwa kuiga kile ambacho wengine wamefanya na kuamini ni sahihi na pia tunatumia hisia, tunatumia fikra zetu kwa kiasi kidogo sana.
Kuna vitu vingi sana vya kujua kiasi kwamba hakuna anayeweza kujua vyote, na kila siku vitu vipya vinagunduliwa. Hivyo badala ya kujidanganya kwamba tunajua sana na kufikiri tunafanya maamuzi kwa fikra zetu, ni vyema tukakubali udhaifu wetu ili tunapofanya maamuzi tujue hasa ni wapi tunaegemea.
Na zama tunazoishi sasa ni hatari zaidi kwa sababu ujuzi wetu unazidi kupungua. Hii ni kwa sababu tunategemea zaidi wengine katika kufanya maamuzi. Watu wamekuwa wavivu wa kusoma vitabu na wanapenda kusikiliza wengine wanasema nini au wanafanya nini na wao ndiyo wafanye.
Ili kuondokana na hatari hii, lazima tuwe tayari kuweka muda na nguvu katika kuboresha ujuzi wetu na kuongeza maarifa tuliyonayo, hasa kwa yale maeneo muhimu kwetu.
SOMO LA 16; MAANA TULIYONAYO KWENYE HAKI IMEPITWA NA WAKATI.
Dhana ya haki ni changamoto kubwa kwenye karne ya 21, hasa wakati ambapo nguvu ya dini inapungua na teknolojia inakua kwa kasi. Dhana ya haki tuliyokuwa nayo ni kufuata misingi na maadili fulani. Lakini kwa sasa dhana hii haiwezi kufanya kazi, kwa sababu unaweza kufuata misingi na maadili, na bado unachofanya kikawa siyo haki kwa wengine.
Chukua mfano unafuata msingi na maadili yako katika fedha na hivyo kuamua kuwekeza fedha zako ili baadaye usiwe na shida ya kipato. Lakini kampuni uliyowekeza fedha, ikawa inachafua mazingira, au inawanyonya wafanyakazi au wakulima au inazalisha bidhaa ambayo inaleta uharibifu kwenye afya za wengine, je hapo wewe umetenda haki?
Katika karne ya 21, dhana sahihi ya haki ni kuangalia kisababishi na matokeo. Tunapaswa kuangalia kila hatua tunayochukua inaleta madhara gani kwa wengine. Japokuwa siyo mara zote unaweza kuona madhara kwa usahihi, lakini kujua kwamba dhana uliyonayo kwenye haki imepitwa na wakati, kunakusaidia kufikiri na kukazana zaidi ili kuweza kutenda haki kwa wengine.
SOMO LA 17; HABARI ZA UONGO ZINADUMU MUDA MREFU.
Changamoto nyingine kubwa kwenye karne ya 21 imekuwa ni habari za uongo au kama ambavyo imekuwa inajulikana kama FAKE NEWS. Changamoto hii imechochewa zaidi na urahisi wa kusambaa kwa taarifa kupitia mitandao ya kijamii. Pia kwa mitandao ya kijamii kujua tabia za watu, habari hizi za uongo zinasambaa kitabaka na kuweza kutengeneza matabaka baina ya watu.
Changamoto ya habari za uongo haijaanza leo, tunaweza kusema maisha ya mwanadamu yamekuwa yanaongozwa kwa habari na hadithi za uongo. Nenda kwenye kila jamii utakutana na hadithi nyingi za kishujaa ambazo ni za uongo kabisa, hazina ukweli wowote. Lakini watu wameishi nazo milele na kuziamini. Kadhalika kwenye dini, zipo habari na hadithi nyingi ambazo ni za uongo kabisa, ambazo haziendani hata na uhalisia wa kawaida, lakini watu wanazichukulia kama ukweli.
Hivyo tunapaswa kujua ukweli siyo kitu ambacho watu wanakitafuta sana, na kama unataka ukweli, ni jukumu lako kuutafuta na siyo kutegemea wengine wakupe ukweli.
Kama unataka kupata habari na taarifa za ukweli, kwanza lazima uwe tayari kulipia, kama unapata taarifa na maarifa yako bure, jua kuna aliyelipia wewe uyapate bure na huyo atakuwa na ajenda yake binafsi. Pili soma vitabu na tafiti zilizofanyika kisayansi, usitumie habari unazopata kwenye vyombo vya habari na mitandao kama ndiyo ukweli, kila unachosikia kwa wengine chukulia kama maoni, na ukitaka ukweli nenda kauchimbe sehemu sahihi.
SOMO LA 18; WAKATI UJAO SIYO KAMA UNAVYOONA KWENYE SINEMA.
Kumekuwepo na sinema nyingi ambazo zinaonesha hali itakavyokuwa baadaye. Baadhi ya sinema hizi kama THE MATRIX zimekuwa zinaonesha nguvu kubwa ya teknolojia kuja kudhibiti na kutawala wanadamu. Lakini sehemu kubwa ya yale yanayooneshwa kwenye sinema hizi siyo yanayotokea.
Tuna wajibu wa kutengeneza sinema zinazoendana na uhalisia, zinazojengwa kwenye misingi ya tafiti za kisayansi ili kuwaelewesha watu mambo magumu kwa njia rahisi.
Sinema ni njia rahisi kutoa ujumbe mgumu na kueleweka kirahisi. Sisi binadamu tunaelewa zaidi kwa hadithi kuliko kupewa ukweli kama ulivyo. Zikitengenezwa hadithi nzuri za namna siku za mbeleni zitakavyokuwa, watu watajifunza na kuchukua hatua.
SOMO LA 19; MABADILIKO NDIYO KITU AMBACHO HAKITABADILIKA.
Kitu pekee ambacho hakitabadilika ni mabadiliko, kila kitu kinabadilika na kitaendelea kubadilika. Na eneo ambalo litaathiriwa sana na mabadiliko ni elimu. Namna ambavyo tumekuwa tunafundishwa na kufundisha imepitwa na wakati. Kufundishwa kwa kukariri kulifanya vizuri enzi ambazo maarifa yalikuwa adimu. Lakini katika zama hizi ambazo maarifa ni mengi, kukariri ni njia iliyopitwa na wakati.
Kukariri pia kunachosha kwenye zama hizi ambazo hutaweza kuwa na kazi moja na ukadumu nayo. Kila wakati utapaswa kubadilika kwa namna mambo yanavyobadilika, utapaswa kupata maarifa mapya na ujuzi mpya wa kufanya vitu vipya.
Mfumo wa elimu na hata kuifunza unapaswa kubadilika, badala ya kuwapa wanafunzi maarifa zaidi ya kukariri, elimu inapaswa kujengwa kwenye misingi minne; KUFIKIRI KWA KINA, MAWASILIANO, USHIRIKIANO NA UBUNIFU. Mtu akibobea kwenye maeneo hayo manne, ataweza kujifunza vitu vingine mwenyewe na pia kushirikiana na wengine vizuri, kitu ambacho ni muhimu kwenye karne hii ya 21. Pia watu wanapaswa kufundishwa zaidi stadi za maisha na namna ya kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea kutokea.
SOMO LA 20; MAISHA SIYO HADITHI.
Swali kubwa ambalo limekuwa linawasumbua watu tangu enzi na enzi ni nini maana ya maisha? Watu wamekuwa wakijiuliza swali hili na mengine kama mimi ni nani? Niko hapa duniani kufanya nini?
Katika kila zama swali la maana ya maisha na ufanye nini na maisha limekuwa linapata majibu mbalimbali. Na majibu yote yamekuwa yanaletwa kwa hadithi.
Hadithi moja maarufu ambayo imekuwa msingi wa dini nyingi ni kwamba kila mtu amekuja duniani akiwa na kusudi lake tayari, na mtu akilitambua kusudi hilo na kuliishi basi atakuwa na maisha bora. Kama hatajua kusudi lake, au akalijua na asiliishi, basi maisha yake yatakuwa hovyo sana, hata kama atakuwa na mali nyingi kiasi gani.
Hadithi nyingine maarufu ni kwamba tupo hapa duniani kuacha alama, kuacha kitu ambacho kutafanya tukumbukwe. Kuwasaidia wengine na kuyafanya maisha yao kuwa bora.
Lakini pia zipo hadithi kwamba maana ya maisha ni yale tunayokutana nayo kila siku, mkusanyiko wa kila tunachopitia ndiyo maana ya maisha. Na hadithi nyingine ni maisha ni mahaba, kwamba mtu akipata anachopenda na kuweka maisha yake yote kwenye kitu hicho amepata maana ya maisha yake.
Hadithi nyingi za maana ya maisha hazijakamilika na hili ndiyo linafanya watu wasiridhike na maisha licha ya kuishi hadithi hizo. Ili hadithi ya maisha ikamilike na iendane na wewe inapaswa kukidhi vigezo viwili, moja ikuhusishe wewe kama mhusika mkuu na pili iwe na maana ambayo ni kubwa kuliko wewe.
Hadithi nyingi tunazoziishi kwenye maisha ni za uongo, ni kitu ambacho kimetengenezwa na watu, lakini tunaziamini na kuziishi kwa sababu kila mtu anafanya hivyo. Na wakati mwingine inabidi tuziamini kwa sababu tulishajitoa sana huko nyuma kwa sababu ya hadithi hizo.
Njia pekee ya kujijua wewe mwenyewe, njia pekee ya kujua maana ya maisha yako siyo kwa kuangalia hadithi unayoiishi, bali kwa kuangalia mateso na kuelewa maana yake. Sehemu kubwa ya maisha yetu ni mateso, hivyo kuyaelewa maisha tunapaswa kuanza na kuyaelewa mateso. Maisha siyo hadithi kama tulivyozoeshwa, bali maana ya maisha ipo kwenye mateso tunayopitia.
SOMO LA 21; TUMIA TAHAJUDI KUYAELEWA MAISHA YAKO.
Tumeona kwamba njia pekee ya kuyaelewa maisha ni kuelewa mateso ambayo tunayapitia. Lakini watu wengi hawapati nafasi ya kuyaelewa mateso wanayoyapitia kwa sababu hawana udhibiti wowote kwenye akili zao. Wengi wanaruhusu akili zao zizurure hivyo bila ya kuelewa kwa nini zinazurura. Unakuta mtu anafanya kitu hiki, lakini akili na mawazo yake yapo kwenye kitu kingine.
Na pia inapotokea mtu amekutana na ugumu au changamoto, akili haipendi kukaa kwenye ugumu ule, badala yake inahama na kwenda kwenye vitu ambavyo siyo vigumu na wala siyo changamoto. Kwa njia hii inakuwa vigumu mtu kuyaelewa mateso na kuyaelewa maisha.
Jawabu la changamoto hii ni mtu kufanya tahajudi, kutenga muda kwenye siku yako ambao unautumia kuiangalia akili yako jinsi inavyohangaika na kuzurura. Tofauti na wengi wanavyofikiri kwamba tahajudi ni kudhibiti akili, hapa unatumia tahajudi kuiangalia akili, na kuona namna inavyozurura.
Njia rahisi ya kufanya tahajudi hii ni kukaa eneo tulivu, kufunga macho yako na kuelekeza akili yako kwenye pumzi zako, unapovuta pumzi ndani fikiria unavuta pumzi ndani, unapoitoa nje fikiria unatoa pumzi nje. Akili yako inapohama kutoka kwenye pumzi zako na kwenda kwenye mengine ona hilo kwamba akili yako imehama. Ni zoezi rahisi kwa kusoma hapa, lakini jaribu kufanya na hazitapita sekunde kumi akili yako itaanza kuhangaika na viti vingi kuliko unavyoweza kufikiri.
Tahajudi ndiyo njia pekee tunayoweza kuitumia kujijua sisi wenyewe na baada ya kujijua kuweza kupiga hatua zaidi kiutambuzi. Tahajudi ndiyo zana pekee tuliyonayo ambayo inaweza kutusaidia tusizidiwe utambuzi na maendeleo makubwa yanayotokea kwenye teknolojia, hasa ujio wa maroboti.
Tutenge muda wa kufanya tahajudi kwenye kila siku ya maisha yetu, mwandishi anasema amekuwa anatenga masaa mawili kila siku ya kufanya tahajudi tangu mwaka 2000 na hilo limemwezesha kuandika vitabu vitatu ambavyo vimekuwa na mchango mkubwa sana kwenye maisha ya wanadamu. Vitabu hivyo ni HOMO SAPIENS, kinachoelezea historia ya mwanadamu, tulipotoka mpaka tulipo sasa HOMO DEUS, kinachoelezea kesho ya mwanadamu na jinsi ambavyo watu wanaweza kuwa miungu na 21 LESSONS FOR 21 CENTURY ambacho kinaelezea hali tunayopitia sasa.
Haya ndiyo masomo 21 kutoka kwenye kitabu cha juma hili, nimejitahidi kuyaeleza kwa ufupi kwa namna itakayoeleweka. Elewa kila somo na chukua hatua sasa, maana mabadiliko yanakuja kwa kasi sana. Muhimu zaidi anza kufanya tahajudi kama bado hujaanza, na kama ulishaanza basi weka juhudi zaidi ili uweze kufikia utambuzi wa juu wa maisha yako.
#3 MAKALA YA JUMA; UTUMWA MPYA ULIOWASHIKA WENGI MATEKA.
Rafiki, katika zama hizi za mabadiliko makubwa ya kiteknolojia, kumekuja aina mpya ya utumwa ambao umewashikilia watu wengi sana mateka. Wengi wameishi kuwa watumwa bila ya wao wenyewe kujua, wanasukumwa kufanya vitu ambavyo hawajui kwa nini wanafanya.
Katika utumwa huu mpya, kuna kifaa kimoja ambacho tumekuwa tunaambatana nacho kwa masaa 24 ya maisha yetu, kabla ya kulala tunahakikisha tumekigusa, na pale tunapoamka, kabla ya kufanye chochote tunakigusa.
Siku hizi hata ukitembea barabarani, watu wameinamisha nyuso zao kwenye vifaa hivyo. Nenda eneo ambalo watu wangepaswa kujumuika pamoja, kila mtu yupo bize na kifaa chake.
Na hata watu ambao wamepotezana kwa muda mrefu, wakapata nafasi ya kukutana, kwa dakika chache sana wataongea, lakini baada ya hapo kila mtu atainama kwenye kifaa chake.
Mtu mmoja amewahi kusema kifaa hiki kipya kina nguvu ya kuwaleta karibu walio mbali, na kuwapeleka mbali walio karibu.
Katika makala ya juma hili, nimekushirikisha ina mpya ya utumwa ambao umewashikilia wengi mateka kupita kifaa nilichokueleza hapo juu. Kama hukupata nafasi ya kuisoma makala hii muhimu sana kwa ukombozi wako, isome sasa hapa; Kuwa Makini Na Aina Hii Mpya Ya Utumwa Ambayo Imewashika Wengi Mateka Na Kuwazuia Kufanikiwa. (https://amkamtanzania.com/2019/03/01/kuwa-makini-na-aina-hii-mpya-ya-utumwa-ambayo-imewashika-wengi-mateka-na-kuwazuia-kufanikiwa/)
Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, kila siku kuna makala mpya na nzuri zinazowekwa.
#4 TUONGEE PESA; NGUVU YA FEDHA KWENYE KARNE YA 21.
Watu walikuwa wanafikiri kwamba katika karne ya 21 kutakuwa na usawa mkubwa sana kwenye jamii zote. Hii ni kwa sababu vitu vilivyokuwa vinaleta mgawanyiko hasa kwa wenye nacho na wasiokuwa nacho vilionekana kukosa nguvu kwenye karne ya 21.
Ukichukulia zama zilizopita, katika mapinduzi ya kilimo, waliomiliki ardhi ndiyo waliokuwa watawala. Hawa walikuwa daraja la juu na wasiokuwa na ardhi walikuwa daraja la chini. Yakaja mapinduzi ya viwanda, ambapo waliomiliki viwanda na zana nyingine za uzalishaji wakawa tabaka la juu.
Karne ya 21, katika mapinduzi ya taarifa tunayoishi sasa, ikaonekana kutakuwa na usawa kwa watu wote, kwa sababu taarifa zipo wazi kwa kila mtu. Lakini tumekuja kugundua kwamba mapinduzi ya taarifa yanaleta mgawanyiko mkubwa kuliko mapinduzi yote ya nyuma. Kwa sababu wale wenye taarifa nyingi, hasa za watu wanakuwa na nguvu kubwa ya kuwatawala watu hao. Kama ambavyo tumeona kwenye uchambuzi wa kitabu cha juma hili, wanaomiliki taarifa ni sawa na wanawamiliki watu, bila ya wanaomilikiwa kujua kama wanamilikiwa.
Pia maendeleo makubwa kwenye teknolojia ya habari na baiolojia, yatatoa nafasi kwa wale wenye uwezo mkubwa wa kifedha kunufaika nayo zaidi. Mfano itakapowezekana kurefusha zaidi maisha, kitu ambacho kinafanyiwa kazi na wanasayansi wengi kwa sasa, wale wenye uwezo wataweza kutumia hilo na kuwa na maisha marefu zaidi. Kadhalika itakapowezekana kuongeza zaidi ufahamu, wenye uwezo ndiyo watanufaika.
Hii inafanya nafasi ya fedha kwenye karne hii ya 21 kuwa kubwa zaidi. Fedha ina nafasi kubwa sana kwenye maisha yetu kwa karne hii, na kama tunataka kuwa na maisha bora, yenye uhuru, marefu na yenye ufahamu mkubwa, basi tunapaswa kuwa na fedha nyingi zaidi.
Na uzuri ni kwamba, kupata fedha kwenye zama hizi siyo kugumu kama kipindi cha nyuma. Huhitaji kuwa na ardhi wala kiwanda ndiyo upate fedha. Unachohitaji ni kuwa na maarifa na taarifa ambazo wengine wanazihitaji, kuwapatia na wao watakuwa tayari kukupatia wewe fedha.
Hakuna kipindi ambacho fedha ni muhimu kama hiki, hakuna kipindi ambacho ni rahisi kwa yeyote kutengeneza fedha kama hiki na cha kushangaza sasa, hakuna kipindi ambacho tabaka la kati ya masikini na matajiri limekuwa kubwa kama kipindi hiki. Kazana kutumia vizuri kila nafasi ya kutoa taarifa na maarifa ili kujitengenezea kipato, hakikisha kuna aina ya taarifa au maarifa unayomiliki ambayo yana uhitaji kwa wengine.
Fedha ni muhimu na ina nafasi kubwa sana kwenye karne hii, kazana kuongeza zaidi kipato chako.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; MAADILI NI KUELEWA MATESO.
“Morality doesn’t mean ‘following divine commands’. It means ‘reducing suffering’. Hence in order to act morally, you don’t need to believe in any myth or story. You just need to develop a deep appreciation of suffering.” ― Yuval Noah Harari
Tumekuwa tunafikirishwa, na sisi wenyewe kuamini kwamba maadili ni kufuata amri fulani za dini au jamii. Lakini hii siyo sahihi, watu wengi wanafuata amri hizo lakini wanakosa maadili. Kama unataka kuona hilo angalia ni kiasi gani dini nyingi zimesababisha vita, angalia namna ambavyo viongozi wengi wa dini wanavyofanya mambo mabaya kwa wengine, kama kubaka, kulawiti, kudhulumu na kadhalika.
Kama ingekuwa maadili ni kuzijua na kuzifuata amri za kidini au kijamii, tungepaswa kuwa na jamii zenye maadili bora sana. Lakini hatuna jamii za aina hiyo, kwa sababu wengi hawaelewi maana halisi ya maadili.
Maana halisi ya maadili ni kuelewa na kupunguza mateso, kwako na kwa wanaokuzunguka. Kila unachofanya, jiulize ni mateso gani kinaleta kwako au kwa wengine. Kwa kuelewa mateso unayosababisha na matendo au maneno yako, na kubadili ili kupunguza au kuondoa mateso hayo, hayo ndiyo maadili.
Haihitaji amri za dini au kijamii kujua kwamba unapomwibia mtu mwingine unasababisha mateso kwake, ua unapoua mwingine unasababisha mateso kwake, kwa watu wake wa karibu na hata kwako pia. Hivyo maadili ni kutokuiba na kutokuua. Kadhalika kwenye mambo mengine kama uongo, uzinzi na mengineyo.
Maadili ni kuyaelewa mateso na kuchagua kuyapunguza.
Rafiki, hizi ndiyo tano za juma hili la 9, tumejifunza kwa kina sana mabadiliko tunayokabiliana nayo kwenye zama hizi na hatua sahihi za kuchukua ili tusiachwe nyuma. Nenda kafanyie kazi yale uliyojifunza, ili mwaka 2050, dunia itakapokuwa tofauti kabisa na ilivyo sasa, usiachwe nyuma na kuonekana huna maana. Badala yake uwe umepiga hatua kubwa zaidi.
#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.
Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.
Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.
Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu