Maisha tayari ni magumu, lakini sisi wenyewe tumekuwa tunaogeza ugumu wake pale tunapojaribu kuyakwepa au kuyatoroka maisha yetu.
Tumekuwa tunatumia muda mwingi kutafuta njia za mkato za kupata tunachotaka, njia ambazo siyo sahihi. Ni baada ya kujaribu njia nyingi, kupoteza nguvu na muda mwingi ndiyo tunajifunza kwamba njia sahihi ni ile ndefu na ngumu, na njia yoyote ya mkato haileti matokeo yanayodumu.
Kama upo safarini kuelekea eneo fulani, utafika kwa kuweka umakini wako kwenye njia unayotumia, na siyo muda wote kuangalia huku na kule, kuona kama kuna njia ya mkato. Kama utafanya hivyo, utaishia kupata ajali, au ukaipata njia lakini ikakupoteza zaidi.
Hivyo ndivyo tunapaswa kuishi maisha yetu, kama kuna mahali tunataka kufika, tuangalie wale waliofika pale na njia waliyotumia, kisha tuingie kwenye safari na kuacha kupoteza muda na nguvu kwenye kutafuta njia za mkato.
Tunachopaswa kuelewa ni kwamba kila njia ina magumu yake, kila njia ina changamoto na vikwazo. Hivyo unapokutana navyo usikimbilie kutafuta njia mbadala au ya mkato, badala yake kabili vikwazo hivyo na uvivuke. Kwa kuvuka vikwazo na changamoto unazokutana nazo unajisogeza karibu zaidi na kile unachotaka kupata au kufikia.
Maisha hayapaswi kutorokwa wala kukwepwa, badala yake tunapaswa kuyaishi maisha, kwa magumu na changamoto zake, maana hayo yote ndiyo yanaleta maana kwenye maisha yetu.
Ukiacha kuhangaika na njia za mkato kwenye maisha, utapata muda na nguvu nyingi za kuwekeza kwenye maisha yako na kupata matokeo bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,