“These things don’t go together. You must be a unified human being, either good or bad. You must diligently work either on your own reasoning or on things out of your control—take great care with the inside and not what’s outside, which is to say, stand with the philosopher, or else with the mob!”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 3.15.13

Ni siku nyingine mpya na ya kipekee sana kwetu,
Tumeiona siku hii siyo kwa sababu tuna nguvu sana au kwa sababu tunastahili sana, ila kwa sababu bado tuna jukumu kubwa la kukamilisha hapa duniani.
Hivyo tuipokee siku hii kwa shukrani na kuitendea haki ili tuweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari CHAGUA UPANDE…
Maisha siyo rahisi kwa sababu kila wakati tunakutana na mambo mengi ambayo yanakinzana.
Kama mtu hutaweza kuchagua upande mmoja na kutulia nao, kila wakati utakuwa unahangaika na upande huu au upande ule. Utachoka kwa mahangaiko hayo na hakuna hatua ambayo utakuwa umepiga.

Chagua kuwa upande wa wema au upande wa ubaya. Chagua kuongozwa na fikra zako au kufuata mkumbo.
Chagua kusimama na mwanafalsafa au chagua kufuata kundi la watu.
Kwenye maisha lazima uchague upande na kuufanyia kazi ndiyo uweze kupiga hatua.
Na upande sahihi kwako kuchagua ni ule ambao unakuwezesha kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yako.
Hivyo chagua upande wa kutumia fikra zako na siyo kufuata mkumbo.
Chagua upande wa kusimama na falsafa na siyo kufuata kundi la watu, ambao hawajui hata wanaenda wapi.

Inashawishi sana kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, kwa sababu ni rahisi kujiambia hakuna ubaya kama kila mtu anafanya.
Ni rahisi sana kutaka kudhibiti hali ya nje au kuwabadili wanaokuzunguka kwa kuamini ni njia rahisi ya kupata unachotaka.
Lakini huo siyo upande sahihi wa wewe kuwa, ni upande ambao utakupa mateso sana na bado hutapata unachotaka.

Upande sahihi ni kuchagua kuwa mwema, siyo kwa sababu unataka uonekane, bali kwa sababu unajua ndiyo kitu sahihi kwako kufanya.
Upande sahihi ni kuchagua kufikiri kwa akili yako na siyo kufuata kile ambacho wengine wanafanya.
Upande sahihi ni kusimamia falsafa na kuacha kufuata kundi la watu, ambao hawajui hata wanakwenda wapi.

Maisha tayari ni magumu, tusizidishe ugumu wake kwa kuchagua upande ambao siyo sahihi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchagua upande sahihi na kuusimamia ili uwe na maisha bora.
#ChaguaUpande, #FikiriKwaAkiliYako, #SimamaNaFalsafa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha