Mpendwa rafiki yangu,

Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, tunaalikwa kuwapokea watoto kadiri Mungu anavyotujalia. Hatutakiwi kuwabagua kadiri ya uimara au udhaifu wao. Tuwapokee jinsi walivyo na kuwapa matunzo bora.

Zama zimebadilika sana, malezi ya watoto ya karne ishirini na moja  ni kazi sana kama zilivyo kazi nyingine. Kizazi cha karne ishirini na moja ni kizazi chenye bahati sana lakini ni kizazi ambacho kimekosa ulinzi kutoka kwa wazazi wao. Kila siku dunia inakuwa bora lakini katika eneo la malezi utandawazi unawaharibu watoto wengi na kelele za dunia.

Watoto karne hii,wamekuwa ni watumwa wa mitandao ya kijamii wanafuatilia mambo ambayo hayaendani na umri wao. Dunia imeachia kila kitu wazi hivyo usipokuwa makini na kumlea mtoto vizuri katika njia ipasayo lazima atapotea.

Kitu ambacho watoto wengi wamekikosa katika karne hii ni ulinzi kutoka kwa wazazi wao. Watoto wengi wa sasa hawana ulinzi kutoka kwa wazazi wao.

malezi bora
silhouette of parents and their children on the beach

Watoto wamekosa ulinzi wa kiroho. Kama wazazi hawajakua kiroho mtoto ni ngumu kupata ulinzi wa kiroho. Watoto wamekuwa wanayumbishwa hawajui hata falsafa gani ya dini waweze kuifuata wanakuwa wapo tu hawajui wapi pa kwenda.

Watoto wanakosa ulinzi wa kiakili. Siyo wazazi waote zama hizi wanaokaa chini na kuwafundisha watoto wao. Hapa mzazi unakumbusha kusoma na mwanao. Hatuwezi kujua uwezo wa watoto wetu kama hatupati muda wa kusoma nao na kuwafundisha. Wanakosa muongozo hivyo wanakuwa wanajiendea kama vile watoto wa nyoka yaani akizaliwa atajijua mwenyewe.

SOMA; Jinsi Wazazi Wanavyochangia Kuwaharibu Watoto Wao Kiakili

Ili mtoto wako awe bora, unatakiwa kumfundisha ubora wa hali juu. Mfundishe mtoto ulinzi wa kifedha yaani ajue misingi ya fedha ili anapokuwa mkubwa anakuwa yuko vizuri eneo hili.

Mfundishe mtoto kazi. Watoto wengi wa siku hizi hawezi kazi. Sasa wazazi wanawawekea watoto hata wakubwa ambao wanaweza kujitegemea wasaidizi. Unakuta watoto ambao wanapaswa kujifanyia kazi zao wanafanyiwa hii inapelekea hata kushindwa kufanya vizuri katika maisha yao ya ndoa. Wanakuwa hata hawajui kupika wala kufua nguo zao.

Hatua ya kuchukua leo; mpe ulinzi mtoto wako. Mpe ulinzi katika maeneo yote ya kiroho, kimwili na kiakili.

Kwahiyo, watoto wengi wanakuwa hawana ulinzi. Wanafanyiwa vitu vya ajabu, wengine wanakuwa hawana hata raha ya kuishi. Hivyo kila mzazi anatakiwa kumfuatilia mtoto wake kwa nje na kwa ndani. Usipomfuatilia dunia inamwadhibu vibaya baadaye, utakaposhindwa kumpa malezi mazuri. Mzazi anajisahau mpaka anakuja kushtuka mtoto ameharibika,wape ulinzi watoto ni jukumu lako.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana