Ndugu,
Mtoto anapozaliwa, mzazi anakuwa na furaha kubwa. Ndugu, jamaa na marafiki, hukusanyika kumpokea na kumpatia zawadi.

Baada ya siku chache, mzazi humpeleka mwanaye kliniki ili kujua kilo zake.  Ili baadaye iwe rahisi kujua ukuaji mtoto na maendeleo yake.

Inapotokea mama akaenda kliniki na kukuta kilo za mwanaye haziongezeki, huanza kujiuliza maswali mengi, pengine kumuona mtaalamu wa afya kwa ushauri.

Kitu kinachofanya achukue hatua, ni matokeo ya namba halisi baada ya kipimo kufanyika kuhusu kilo za mtoto wake.

Kadhalika kwenye mauzo ndivyo ilivyo. Masomo mengi ya nyuma tumeona mauzo ni mchezo wa namba, na kama ni namba basi zinahesabika.

Ili kupima ufanisi wako, lazima hesabu ifanyike kujua idadi ya wateja uliowahudumia, kuwauzia kadhalika na maeneno mengine.

Inapotokea mauzo yapo chini, lazima urejee kwenye yale uliyofanya. Kama ni makosa, labda kukosea oda, mzigo au kitu kingine, jua yamechangia mauzo kuwa chini.

Namna nzuri kuyapandisha mauzo yako ni kuongeza umakini, kuwahudumia vizuri wateja wako. Maana kwenye huduma, kosa unalofanya mbele ya mteja ndiyo kumbukumbu unayomuachia.

Hiki ni kitu unachopaswa kujua. Ikiwa utafanya makosa na kuyachukulia poa yatakuletea shida zaidi mbeleni, maana yanahesabika mbele ya mteja.

Unapogundua kuna makosa yamefanyika katika uhudumiaji, usisubiri mpaka wengine wafanye marekebisho kwa ajili yako

Ni suala linalopaswa kufanyiwa kazi mara moja na kutolipa nafasi ya kurudiwa. Rejea msemo wa usipoziba ufa utajenga ukuta.

Hatua za kuchukua leo;

Moja; Jifanyie tathimini juu ya yale unayofanya

Mbili; Kubali kukosea, kisha jisahihishe.

Kumbuka; Kosa dogo linapofanyika, hupaswi kuanza kutafakari juu ya kutafuta suluhu. Bali hapo hapo unapaswa kuchukua hatua mara moja. Maana likikaa litazalisha tatizo au kosa lingine kubwa yake.

Je, ni kosa lipi ulifanya mbele ya mteja na kukosa mauzo?
Shirikisha hapa, tujifunze na sisi.

Imeandaliwa Lackius Robert

Mkufunzi Msaidizi CHUO CHA MAUZO na Mwandishi.

0767702659 / mkufunzi@mauzo.tz

Karibu tujifunze zaidi