Waswahili wanasema usione vyaelea, jua vimeundwa. Chochote ambacho unaona kimekua, jua kuna kazi kubwa imefanyika nyuma yake. Unapoona wafanyabiashara wakubwa wamefika pale walipo, hawakuamka asubuhi na kujikuta walipo, bali walianzia chini, wakaweka juhudi mpaka kufika pale walipofika sasa.

Hivi ndivyo mgahawa mkubwa duniani wa kuuza vyakula vya haraka Mc Donald’s ulivyoweza kukua na kusambaa dunia nzima. Ulianza na wazo la mtu mmoja, ambaye kwa kuweka juhudi na kuishi misingi fulani, aliweza kukuza mgahawa huu kutoka mmoja mpaka kufikia migahawa zaidi ya laki moja kwenye zaidi ya nchi 100 duniani.

Paul Facella mshauri wa mambo ya biashara na mtu aliyefanya kazi kwenye mgahawa wa McDonald’s kwa zaidi ya miaka 20 amefanya utafiti kupitia uzoefu wake na uzoefu wa wengine kujua nini kimesababisha mgahawa huo kukua.

Katika utafiti wake, Paul amekuja na misingi saba ambayo mgahawa huu umejengwa juu yake na kuuwezesha kukua. Kupitia kitabu chake hichi, ametushirikisha misingi hii na kwa mifano jinsi imesaidia mgahawa huu kukua.

everything-i-know-about-business-i-learned-at-mcdonalds

Kwa kuanza, mgahawa wa McDonald’s unaendeshwa kwa mfumo wa Franchise, ambapo wao kama McDonald’s wanaweza kumpa mtu leseni ya kuendesha mgahawa wao na kuusimamia bila ya wao kuhusika moja kwa moja. Wanachofanya ni kufuatilia na kujua kama mtu anafuta misingi na viwango ambavyo vimewekwa. Kushindwa kufuata misingi na viwango, kunamfanya mtu anyang’anywe leseni ya kuendesha mgahawa wa McDonald’s.

McDonald’s ni mgahawa wa kwanza kuendeshwa kwa mfumo huu hivyo kama isingekuwa na misingi imara ambayo inasimamia, usingeweza kupata mafanikio uliopata sasa. Pamoja na changamoto mbalimbali ambazo mgahawa huu umepitia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1955, bado unabaki kuwa mgahawa wenye mafanikio makubwa.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi ambayo tutajifunza misingi saba ya mafanikio ya mgahawa wa McDonald’s ambayo pia tunaweza kuitumia kwenye mafanikio ya biashara zetu na hata mafanikio yetu binafsi.

MSINGI WA KWANZA; UAMINIFU NA UADILIFU.

Uaminifu na uadilifu ni msingi muhimu sana wa mafanikio kwenye biashara na maisha kwa ujumla. Ukiangalia biashara zote zilizofanikiwa na kudumu kwenye mafanikio kwa muda mrefu, utaona uadilifu na uaminifu kama msingi muhimu. Wapo wafanyabiashara wanaotumia njia zisizo za uaminifu, wanapata mafanikio lakini hayadumu kwa muda mrefu.

 1. Mawakala wafaidike kabla ya kampuni.

Ray Krock mwanzilishi wa McDonald’s aliweka uaminifu na uadilifu kama msingi muhimu wa mgahawa alioanzisha. Na katika kuishi msingi huu, Ray alisema mawakala lazima wafaidike kabla kampuni mama haijafaidika. Alifanya kila linalowezekana kuhakikisha kila anayepata leseni ya kuendesha mgahawa wa McDonald’s anapata faida hata kama kampuni haipati faida. Hili liliwafanya mawakala kuiamini kampuni na kuweka juhudi ili kufanikiwa, kitu ambacho kilinufaisha kampuni zaidi.

 1. Makubaliano ya mdomo.

Kwa ukubwa wa kampuni ya McDonland’s na jinsi inavyojihusisha na watu wengi, ingetegemewa kila jambo linalofanywa lifanywe kwa mikataba inayohusisha wanasheria. Lakini kampuni hii iliendeshwa kwa mikataba ya makubaliano ya mdomo. Yaani ahadi ilitolewa kwa mdomo na kila mtu aliishi. Wasambazaji wa malighafi mbalimbali kwenye kampuni hii wengi hawakuwahi kuwa na mikataba ya kisheria, bali walikubaliana kwa mdomo na kampuni ilitunza na kutekeleza ilichoahidi. Hii ilifanya wanaojihusisha na kampuni kuiamini na kufanya nayo kazi zaidi.

 1. Uaminifu na uadilifu haufundishwi.

Katika kuhakikisha kampuni inapata wafanyakazi na mawakala ambao ni waaminifu na waadilifu, uongozi ulijua kwamba unaweza kufundisha viwango na misingi mingine, lakini siyo uaminifu na uadilifu. Hivyo ilihakikisha inafanya uchunguzi kujua watu kabla hawajawaajiri au kuwapa leseni ya kuwa wakala. Uaminifu na uadilifu ni vitu ambavyo ni tabia na vinaanzia ndani ya mtu mwenyewe, huwezi kufundisha wala kuvilazimisha kwa mkataba wa kisheria. Kama mtu siyo mwaminifu, atapata njia ya kutekeleza hilo hata umpe mkataba mkali kiasi gani.

 1. Uaminifu na uadilifu ni kuishi na siyo kusema.

Katika kuhakikisha watu wanaelewa umuhimu wa msingi wa uaminifu na uadilifu, viongozi wa McDonald’s waliishi msingi huu kwenye kila wanachofanya. Hawakuwa wakiongea ili watu wasikie, badala yake waliishi kwa matendo na watu walijionea wenyewe. Hivyo kama unataka watu wajue umuhimu wa uaminifu na uadilifu kwa chochote unachofanya, ishi msingi huo.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Psychology Of Selling (Jinsi Ya Kuuza Zaidi, Kwa Urahisi Na Haraka Kuliko Unavyodhani.)

MSINGI WA PILI; MAHUSIANO.

Mahusiano ni msingi muhimu sana kwenye mafanikio ya kila kitu kwenye maisha. Hakuna kitu chochote hapa duniani ambacho mtu unaweza kufanya mwenyewe. Unahitaji msaada na ushirikiano wa watu wengine. Hivyo unavyoweza kujenga mahusiano mazuri ndivyo unavyowavutia watu wengi zaidi kushirikiana na wewe.

 1. Uhusiano wa kiti cha miguu mitatu.

McDonald’s imejengwa kwenye msingi wa mahusiano ya kiti cha miguu mitatu. Mguu wa kwanza ni wafanyakazi wa kampuni, mguu wa pili ni wasambazaji wa malighafi zinazotumika na mgahawa na mguu wa tatu ni mawakala wa mgahawa. Kama unavyojua, kiti cha miguu mitatu hakitakuwa na maana kama mguu mmoja utakosekana. McDonald’s imekuwa ikitunza na kukuza mahusiano baina ya mihimili hiyo mitatu ya mafanikio yake.

 1. Mahusiano zaidi ya biashara.

Japokuwa McDonald’s ilikuwa biashara, mahusiano yaliyojengwa baina ya watu yalikuwa zaidi ya biashara, watu walichukuliana kama ndugu na hata kuweza kusaidia kwenye mambo nje ya biashara. Wafanyakazi walithaminiwa sana na mawakala walisaidiwa hata pale ambapo kampuni ilikuwa haipati faida. Kwa njia hii watu walijitoa zaidi na kuiwezesha kampuni kukua zaidi.

 1. Hakuna kuitana bosi.

Kwenye kila taasisi kubwa, kuna madaraja mbalimbali ya wafanyakazi, hivyo kwenye kila daraja kunakuwa na mabosi, yaani wasimamizi ambao wanakuwa na watu chini yao. Kwenye kampuni ya McDonald’s kumekuwepo na madaraja hayo, lakini yamekuwa hayatumiki kwenye mawasiliano ya siku kwa siku. Kumekuwa hakuna utaratibu wa kuitana bosi, kila mtu amekuwa akiitwa kwa jina lake la kwanza. Badala ya kuitwa Bwana Makirita, unaitwa tu Amani na kila mtu hata mfanyakazi wa chini kabisa, alikuwa huru kumwita meneja kwa jina lake la kwanza. Hii ilifanya watu wajisikie wapo nyumbani na kuongeza ushirikiano zaidi.

 1. Umenta unasaidia kuboresha mahusiano.

Moja ya vitu vilivyoboresha mahusiano kwenye kampuni ya McDonald ni umenta. Ambapo kila mfanyakazi alikuwa na mtu wa karibu kwake, ambaye alikuwa akimsaidia kukua zaidi kwenye kampuni. Mtu huyo alikuwa na uzoefu zaidi na alikuwa kama rafiki kwake ambaye anaweza kwenda kwake akiwa na uhitaji wowote na akapata msaada mzuri.

 1. Urafiki na kazi vinaweza kwenda pamoja.

Viongozi wengi wamekuwa wakiamini kwamba urafiki na kazi haviwezi kwenda pamoja. Kwamba ukishakuwa na urafiki na wale unaowasimamia, watakuzoea na mwishowe watakuwa hawafuati kile unachowaelekeza. Lakini kwenye kampuni ya McDonald’s urafiki na kazi vimekuwa vinakwenda pamoja na kusaidia kampuni kukua. Kila mtu akishajua majukumu yake na jinsi ya kuyatekeleza, urafiki unasaidia kukosoana na kusahihishana bila ya kuogopana.

MSINGI WA TATU; VIWANGO, KAMWE USITOSHEKE.

Kwenye hii dunia, usipojiwekea viwango kwenye jambo lolote unalofanya, hutaweza kupiga hatua na hata ukipiga, utaanguka haraka sana. Tumekuwa tunaona watu wanaanza biashara zao, wanaanzia chini, wanakazana, wanapata mafanikio, baadaye wanajihusisha na mambo yasiyo sahihi na kupelekea biashara zao kuanguka. Viwango ni muhimu sana, kwa sababu vitakuzuia kuingia kwenye maeneo ambayo siyo sahihi kwako. Wanasema hakuna kitu kinalevya kama mafanikio, sasa kama utafanikiwa ukiwa huna viwango, mafanikio yatakuwa sumu kubwa kwako.

 1. Ubora, huduma na usafi.

Viwango ambavyo vimekuwa vinatumika katika kuendesha migahawa ya McDonald’s ni ubora wa chakula, huduma bora kwa wateja na usafi wa migahawa. Kila eneo ambalo utakutana na mgahawa wa McDonald’s unaweza kulipima hilo wewe mwenyewe, kwa sababu ni viwango ambavyo wamekuwa wanavifanyia kazi kila siku.

 1. Kamwe usitosheke.

Pamoja na mafanikio makubwa ambayo kampuni ya McDonald’s imekuwa inapata, bado imekuwa inapiga hatua zaidi na zaidi kwa sababu msingi wake mkuu ni huu, KAMWE USITOSHEKE. Hata ufanikiwe kiasi gani, kumbuka bado kuna nafasi ya kuwa bora zaidi. Hivyo kampuni imekuwa ikiangalia maeneo zaidi ya kufungua migahawa, njia bora zaidi za kupunguza gharama, njia bora za kuongeza faida, kuongeza bidhaa, kuongeza wateja na kadhalika. Dhana hii ya kutotosheka inafanya watu wasifanye mambo kwa mazoea.

 1. Endeshwa na matokeo.

Kampuni ya McDonald’s imekuwa inaendeshwa na kitu kimoja, matokeo, na siyo tu matokeo ya kawaida, bali matokeo bora. Hivyo kila wakati kitu kinachopimwa ni matokeo ambayo yanapatikana. Kama kitu kinafanyika na matokeo siyo bora, basi inaangaliwa njia ya kuboresha zaidi. Kwa kuangalia matokeo ambayo yanapatikana, inakuwa rahisi kuona njia za kupiga hatua zaidi.

 1. Viwango kwa mawakala.

Kampuni ya McDonald’s, licha ya kuwaruhusu mawakala wake kujiendesha wao wenyewe, inaendelea kusimamia vile viwango ambayo imejiwekea ambavyo ni ubora, huduma na usafi. Kampuni imekuwa ikifanya uchunguzi wa kushtukiza kwa mawakala wake na kama wakala atakutwa hajafikisha viwango vinavyotakiwa, alifungiwa mara moja na kunyang’anywa leseni. Ukali huu wa kusimamia viwango umewafanya mawakala wengi kuwa makini na kusimamia viwango wanavyopewa.

 1. Sema hapana kama viwango havifikiwi, hata kama unakosa faida kubwa.

Kitu kimoja kimewahi kuwashangaza watu wengi kwenye kampuni ya McDonald, pale aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo, Fred Turner alipokataa dili kubwa la kuweka mgahawa wa McDonald’s kwenye vituo vyote vya jeshi. Lilikuwa dili lenye faida kubwa sana, lakini yeye alisema hapana pale alipoona viwango walivyojiwekea visingeweza kufikiwa. Hii inatuonesha umuhimu wa kusimamia viwango hata kama tunapoteza fedha.

SOMA; Uchambuzi Wa Kitabu; The Most Successful Small Business In The World (Kanuni Kumi Za Kuwa Na Biashara Ndogo Yenye Mafanikio Makubwa.)

MSINGI WA NNE; ONGOZA KWA MFANO.

Ni rahisi sana kutoa maagizo ya watu wanapaswa kufanya nini. Lakini watu ni rahisi kusahau kile wanachoambiwa, ukitaka watu wafanye kitu kweli, basi ishi kile unachohubiri. Kile ambacho unataka watu wafanye, anza kukifanya wewe.

 1. Mkurugenzi anafanya usafi kwenye mgahawa.

Mwanzilishi na mkurugenzi wa McDonald’s alikuwa akisifika kwa kukutwa akifanya usafi kwenye mgahawa wa McDonald’s. Hata kama alikuwa anapita tu na kukuta kuna uchafu ambao haujaondolewa, basi hakuongea na yeyote, bali alifanya usafi eneo ambalo halikuwa safi. Hii iliwafanya walio chini yake kujituma mno kuhakikisha migahawa inakuwa safi kabisa. Hii iliwafanya watu kuhakikisha kila eneo ni safi, na pia iliwajengea watu tabia ya kuchukua hatua bila ya kusubiri mwenye jukumu alifanye.

 1. Waajiriwa na viongozi watarajiwa wanafundishwa kwa kufanya kazi pamoja.

Kwenye kampuni ya McDonald’s waajiriwa wapya na wale wanaoandaliwa kuwa viongozi wa baadaye, wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja na wale wenye uzoefu na hata viongozi wakubwa. Hili linawafanya kujifunza kwa matendo na kujifunza haraka badala tu ya kupewa maelekezo. Kwa kipindi kirefu, kampuni ya McDonald’s imekuwa na sera ya kutokuwa na milango ya ofisi, kiasi kwamba kila kitu kipo wazi na kila mtu anaweza kumwona mtu yeyote bila ya kuhitaji kuomba ruhusa.

 1. Ukweli upo kwa wateja.

Kampuni ya McDonald’s imekuwa na msimamo mmoja kwamba ukitaka ukweli wowote kuhusu biashara basi angalia wateja wanavyohudumiwa na wanavyochukulia huduma wanazopata. Hivyo mameneja wote wamekuwa hawakai ofisini, badala yake kuwa ndani ya mgahawa, kuangalia namna huduma zinavyotolewa kwa wateja. Hii inawasaidia kujua kila kinachoendelea na kuweza kuchukua hatua pale mambo yanapokuwa hayaendi vizuri.

MSINGI WA TANO; UDHUBUTU, SEMA KAMA ILIVYO.

Kitu kimoja ambacho kinawafanya wengi waone ukweli ni mgumu ni namna ambavyo ukweli unaumiza. Watu wanapenda ukweli, lakini pale ukweli unapowaumia wao au wengine, wengi huuepuka. Moja ya misingi ya mafanikio kwenye kazi na hata biashara ni udhubutu, wa kusema na kufanya kile kilicho sahihi, bila ya kuogopa hata kama kinaumiza.

 1. Hakuna cha bure, kufanikiwa au kushindwa.

Ipo gharama ya kulipa ili ufanikiwe, na pia ipo gharama ya kulipa ili ushindwe. McDonald’s imekua inaendeshwa kwa msingi huo kwamba kushindwa na kushinda kote kuna gharama, lazima uchague unalipa gharama ipi na uilipe kwa ujasiri bila ya kuogopa. Hivyo kama unataka kufanikiwa, lazima uwe tayari kulipa gharama, na gharama huwa inaumiza. Kuna hatari za kuingia ili kuweza kufikia makubwa, lazima uwe tayari kulipa hatari hizo.

 1. Kubali pale unapokosea.

Katika taasisi nyingi, na hata maisha ya kawaida, wale ambao wanashika nafasi za uongozi, hawakubali kukiri kwamba wamekosea, hata pale inapokuwa wazi kwamba wamekosea, huishia kunyamaza na kubadili mambo kimya kimya. McDonald’s imejengwa kwenye msingi wa kiongozi na yeyote kukubali pale anapokosea na kuchukua hatua sahihi. Kwa njia hii, viongozi wanaheshimiwa zaidi na kuonekana kuwa sehemu ya timu nzima inayofanya kazi.

SOMA; Mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu 85 INSPIRING WAYS TO MARKET YOUR SMALL BUSINESS. (Njia 85 za kutangaza biashara yako)

MSINGI WA SITA; MAWASILIANO.

Changamoto zote kubwa kwenye maisha, ukichimba mzizi wake unaanzia kwenye mawasiliano. Iwe ni mahusiano ambayo yamevunjika, angalia vizuri na utakuta kuna mahali mawasiliano haya kwenda vizuri. Iwe ni biashara inakosa wateja, ukiangalia utakuta wateja hawana taarifa sahihi za biashara hiyo. Hivyo kama unataka mafanikio kwenye maisha, unahitaji kuimarisha sana mawasiliano yako na wengine, hakikisha kile unachotaka wengine wakijue, wanakijua kwa usahihi.

 1. Kila kampuni ina hadithi yake.

Kila kampuni ina hadithi yake, hivyo viongozi wa McDonald’s wamekuwa wakiamini kwenye nguvu ya hadithi hizi na kutoa njia za kuweza kusambaza hadithi hizo. Iwe ni kwenye mikutano, taarifa kwa uma na hata njia nyingine za mawasiliano, hadithi ya kampuni inapaswa kuwa sahihi na watu kuielewa. Hadithi ya kampuni inahusisha kile ambacho kampuni inaamini na kusimamia. Hivyo mtu anaposikia jina la kampuni au kuona nembo yake, moja kwa moja kwenye akili yake anakumbuka kile kampuni inasimamia.

 1. Usiposema wewe, watasema wengine na kwa ubaya.

Kila siku tumekuwa tunasikia habari mbaya na hasi kuhusu makampuni na taasisi kubwa. Mara nyingi habari hizi huwa siyo kweli, na kama ni kweli basi zinakuwa zimeongezwa chumvi sana, kwa sababu vyombo vya habari vinapenda habari za kusisimua. Sasa ili kuzuia kampuni au taasisi isidhurike na habari hizo mbaya, inapaswa kuwa mbele kueleza habari zake nzuri kwa kila njia inayoweza kutumia. Iwe ni kwa utoaji wa elimu, udhamini wa shughuli mbalimbali za kijamii, kampuni inahitaji kuhusishwa na mambo mazuri.

 1. Kila mtu anapaswa kusikilizwa.

Mawasiliano siyo tu kutoa taarifa au maagizo na watu wakayafuata. Bali mawasiliano ni kitu kinachohusisha pande mbili. Hivyo ili mawasiliano yakamilike, uongozi lazima umsikilize kila mtu ana lipi la kusema. Uongozi unapaswa kumsikiliza mtu, hata kama anachosema kinaonekana hakina maana. Hiyo inawajengea watu imani kwamba wanasikilizwa na michango yao inathaminiwa.

MSINGI WA SABA; KUTAMBUA NA KUTHAMINI.

Hakuna kampuni au taasisi ambayo imeweza kukuzwa na mtu mmoja. Chochote ambacho unaona kimekua, basi jua kuna watu wengi ambao wameweka machozi, jasho na hata damu zao. Wapo watu walioteseka hasa, wapo watu waliojitoa kwa juhudi zao zote kuhakikisha kitu kinakua. Hawa ni watu ambao wanapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa, kwa kufanya hivyo wanahamasika zaidi na wengine wanahamasika kuchukua hatua.

 1. Zawadi kwa wanaojitoa na kuleta matokeo mazuri.

Kampuni ya McDonald’s imekuwa inasifika kwa mpango wake wa zawadi kwa wafanyakazi na mawakala wanaofanya vizuri. Kwa mfano watu wote ambao wanapata uongozi kwenye kampuni hiyo, lazima wawe wameanzia hatua ya chini kabisa kwenye kampuni hiyo na kupanda ngazi kadiri wanavyoweka juhudi zaidi. Hata ambao wamepata kuwa mameneja na wakurugenzi, walianzia ngazi ya chini kabisa ya kufanya usafi na kuhudumia wateja. Kwa wale waliopo chini kuona wenzao wanapanda juu, wanapata hamasa ya kuweka juhudi zaidi ili nao wapande juu zaidi.

 1. Huhitaji gharama kubwa kuwatambua na kuwathamini watu kwa michango yao.

Watu wengi hufikiri ili uwatambue watu na kuthamini michango yao basi unahitaji uwe na fedha nyingi za kuwaongezea mshahara, kuwapa marupurupu na hata kuwapa zawadi mbalimbali. Lakini hilo siyo kweli. Kampuni ya McDonalds imekuwa inatumia njia nyingi ambazo hata hazina gharama. Mfano kumsifia mtu mbele ya wengine, kuwa na ubao wenye majina ya wanaofanya vizuri, kuwa na kitabu cha mwaka ambacho kinaorodhesha wale waliofanya vizuri, kupewa siku ya kupumzika yenye malipo baada ya mtu kujitoa sana. Zote hizo ni njia ambazo zinamfanya mtu aone mchango wake unatambuliwa na hazina gharama yoyote.

 1. Hisa ni njia yenye nguvu ya kutambua mchango wa watu.

Kampuni ya McDonald’s ndiyo kampuni ya kwanza kutoa zawadi ya umiliki wa hisa kwa wafanyakazi wake, hasa wale waliokaa muda mrefu na walioonesha kujituma zaidi. Hii iliwafanya wajione wao ni sehemu ya kampuni, kwa kumiliki hisa wanakuwa tu siyo wanafanya kazi kwenye kampuni, bali wanamiliki kampuni hiyo pia. Hilo linawafanya wajitume zaidi kwa kuwa wanajua ni kitu chao.

Hii ndiyo misingi saba muhimu ambayo imeiwezesha kampuni ya McDonald’s kuwa na mafanikio makubwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50. Angalia jinsi gani unaweza kutumia misingi hiyo kwenye kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla. Chochote unachofanya, kifanye kwa juhudi, kuwa mwaminifu na mwadilifu, kuwa jasiri kusimamia unachoamini, tengeneza mahusiano mazuri na wengine, boresha mawasiliano yako na usisahau kuwatambua na kuwathamini wale wanaokusaidia kupiga hatua zaidi.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

KIPATO KWA BLOG