Kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo uchumi unavyozidi kuwa mgumu duniani kote. Hii ni kwa sababu maendeleo ya sayansi na teknolojia yanakuja na vifaa ambavyo vinarahisisha sana kazi na hivyo watu wachache zaidi kuhitajika kwenye kazi yoyote ile.

Kwa mfano kompyuta moja inaweza kuchukua kazi za watu watano, ikaendeshwa na mtu mmoja na ikafanya kazi kubwa. Pia programu mbalimbali za kompyuta, zinarahisisha sana kazi. Mfano programu ya kutunza kumbukumbu za fedha za biashara, inaweza kupunguza nafasi za watu wanaohitajika kukusanya na kutunza kumbukumbu hizo.

Kama

Kutokana na mabadiliko haya, kile kilichotufikisha hapa hakitakufikisha kule unakokwenda. Yale mazoea ya kusoma, upate cheti na cheti kikusaidie kupata kazi yameshapitwa na wakati.

Sasa hivi kitakachokupa fedha na hata mafanikio ni uwezo ulionao ambao unautumia kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Kuna aina mbili za uwezo ambazo zinalipa sana kwenye zama tulizopo na hata tunazoendea. Uwezo ambao hauwezi kuchukuliwa na kompyuta wala program ya aina yoyote ile. Hata maroboti yanayoweza kufanya kazi kwa umakini na muda mrefu kuliko binadamu yeyote, hayana uwezo huo unaohitajika.

Hivyo ni wajibu wako kujua uwezo huo wa aina mbili na jinsi ya kuutumia ili kuweza kufanikiwa.

Aina ya kwanza ni uwezo wa kutatua matatizo magumu.

Kompyuta na hata program za kompyuta zinaweza kutatua tatizo lolote lile, kama tu tayari zimeshapewa suluhisho. Yaani zinatatua matatizo kwa kutumia kumbukumbu. Lakini pale tatizo linapokuwa jipya kabisa, ni mtu pekee anayeweza kutatua, na siyo kila mtu, bali mtu anayetumia akili yake vizuri.

Hivyo mara zote jenga akili yako kwenye uwezo wa kutatua matatizo magumu na ambayo hayajazoeleka. Acha kompyuta na wengine wasiotaka kufanikiwa watatue matatizo yaliyozoeleka, wewe tatua magumu na onesha njia. Utahitajika kila mahali.

SOMA; UKURASA WA 975; Unamwangalia Nani?

Aina ya pili ni uwezo wa kuzalisha matokeo bora kwa kasi na viwango.

Watu hawana muda, watu wanataka kitu na wanakitaka sasa, watu wanataka ubora wa hali ya juu, wakiukosa hawasubiri hata dakika moja, wanaondoka. Hivyo ukiwa na uwezo wa kuzalisha matokeo bora kabisa kwa kasi na viwango vya hali ya juu, hutakosa wanaotaka huduma au bidhaa zako. Mara zote utahitajika maana dunia inazidi kwenda kasi.

Jijengee uwezo huu wa aina mbili kwenye eneo ambalo umechagua kwenye maisha yako, kuwa tayari kutatua matatizo magumu, na zalisha matokeo bora kabisa kwa kasi na viwango vya hali ya juu. Dunia itajua uwepo wako hata kama utakuwa kwenye pori la aina gani.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog