“Above all, keep a close watch on this—that you are never so tied to your former acquaintances and friends that you are pulled down to their level. If you don’t, you’ll be ruined. . . . You must choose whether to be loved by these friends and remain the same person, or to become a better person at the cost of those friends . . . if you try to have it both ways you will neither make progress nor keep what you once had.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 4.2.1; 4–5
Ni jambo la kushukuru sana kwa sisi kuiona siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Siyo kwa ujanja wala nguvu zetu tumepata nafasi hii, ila kwa upendeleo mkubwa, kwa sababu bado tuna mchango mkubwa wa kutoa hapa duniani.
Njia pekee ya kushukuru kwa nafasi hii tuliyopata leo ni kuitumia vizuri siku ya leo, kufanya yale yaliyo bora na kuweka juhudi kubwa sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; KUWAPOTEZA MARAFIKI AU KUJIPOTEZA MWENYEWE…
Kwenye haya maisha, unaweza ukawa na keki, au ukaila, lakini huwezi kula keki yako halafu ukaendelea kubaki nayo.
Hii ina maana kwamba, kuna kitu unapaswa kupoteza ili kupata unachotaka, ubaki na keki lakini usile, au ule na usibaki na keki.
Hili linakwenda mpaka kwa wale watu wetu wa karibu, marafiki zetu.
Hawa wanaweza kuwa kikwazo kikubwa au hamasa ya kufanikiwa.
Kama marafiki zako wanapiga hatua kufanikiwa, na wewe utasukumwa kupiga hatua kufanikiwa.
Lakini kama marafiki zako wamekata tamaa na wanaona hawawezi kufanikiwa, watakurudisha nyuma na wewe, hata uwe na hamasa kiasi gani, hutaweza kufanikiwa.
Lakini watu wengi wamekuwa hawapendi kuwapoteza marafiki zao, hasa wale wamekuwa nao kwa muda mrefu.
Hivyo wanajidanganya urafiki utaendelea na mafanikio watayafikia.
Hicho kitu hakipo.
Kauli nyingi sana zilishatolewa kwenye hili;
wewe ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka – Jim Rhon
ndege wanaofanana huruka pamoja – Wahenga
nioneshe marafiki zako na nitakuambia tabia zako – Goethe
Kauli zote hizi zinaonesha nguvu ya marafiki kwenye kufanikiwa au kushindwa kwetu.
Sasa fanya maamuzi leo na uache kujidanganya,
Amua kuwapoteza marafiki ambao hawaelekei kwenye mafanikio, ili wewe uweze kufanikiwa.
Au amua kuwakumbatia marafiki hao, lakini ujue kabisa hutafanikiwa.
Kumbuka ni kimoja pekee unaweza kuchagua, usijidanganye unachagua vyote.
Unawapoteza marafiki ufanikiwe, au unajipoteza wewe ili ubaki na marafiki ulionao.
Na kumbuka ukiwapoteza marafiki ulionao siyo kwamba utabaki bila ya marafiki, bali utatoa nafasi kwa marafiki wapya, wanaoelekea kwenye mafanikio kama wewe.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchagua kimoja, kati ya mafanikio yako au marafiki uliokwishawazoea.
#KupataNiKupoteza, #KuwaMakiniNaMarafiki, #ChaguaKwaUsahihi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha