Mara kwa mara nimekuwa nakushirikisha nguvu ya neno HAPANA. Umuhimu wa kutumia neno hili ili kuweza kupiga hatua kwenye maisha yako. Hili ni neno ambalo litakupa uhuru mkubwa sana kwenye maisha yako. Unapokuwa na uhaba wa muda, neno hapana ni rafiki sana kwako. Unapaswa kusema hapana kwenye vitu visivyo muhimu ili kuweka muda wako kwenye vile ambavyo ni muhimu zaidi.
Lakini kuna wakati ambapo neno hapana linaweza lisiwe na msaada kwako, na hapo unapaswa kutumia neno NDIYO mara nyingi uwezavyo.
Unapokuwa kwenye hali ya sonona, ni wakati wa kusema ndiyo kwa kila kitu. Kwa sababu sonona ina tabia ya kukutenga na maisha kwa ujumla, kujiona hufai na huna thamani. Huu ndiyo wakati wa kupingana na hali hiyo kwa kusema NDIYO kwa maisha.
Sema ndiyo kwa kufanya chochote hata kama siyo kikubwa au siyo muhimu, kwa sababu sonona inachochewa zaidi na kukosa kitu cha kufanya. Unapokuwa huna cha kufanya na unaingia kwenye hali ya sonona, sema ndiyo kwa chochote kinachokuja mbele yako.
Endelea kusema ndiyo kwa kila kitu mpaka pale muda unapokuwa adimu kwako na unahitaji kusema hapana ili kuweka vipaumbele kwenye maisha yako.
Unapokuwa huna cha kufanya au hujisikii kufanya chochote na ukaendelea kutumia neno hapana ni sawa na kumwaga mafuta ya taa kwenye moto ukitaka kuuzima, kinachotokea ni kuuchochea zaidi.
Sema ndiyo pale unapokuwa kwenye hali ya sonona na ndiyo itakuinua tena mpaka utakapoweza kusema hapana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,