Rafiki yangu mpendwa,
Wahenga walisema, usihesabu vifaranga kabla mayai hayajaanguliwa. Hii ni kauli iliyobeba ushauri mkubwa sana wa maisha ambao wengi tumekuwa hatuuzingatii.
Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto ambapo tunapena hatua za kuchukua ili kuweza kutoka pale ambapo tumekwama na kupiga hatua zaidi.
Leo tunakwenda kushauriana kuacha kuweka kwenye mahesabu yako fedha ambayo ipo kwenye mfuko wa mtu mwingine.
Msomaji mwenzetu Paschal alikuwa na haya ya kutuandikia katika kuomba ushauri kwenye eneo hili;
“Changamoto niliyo nayo ni kwamba nimekuwa nategemea sana pesa ambayo nilimkopesha mtu toka mwaka 2017 mwezi wa saba nianzishe biashara lakini sasa huyo mtu sioni mwelekeo wa kunipa hiyo pesa kulingana na makubaliano yetu. Sasa nakuwa nikingoja anipe ndio nipate hela hiyo ya mtaji lakini sioni mwelekeo yaani kama ananipa hiyo hela na mimi naona kama muda unaenda kuanzisha biashara yangu na hapa sasa sina hela ya kuniwezesha kuanzisha biashara yangu. Je nifanyeje jamani naomba ushauri tafadhali.” – Paschal J.
Ndugu Paschal, mtu pekee anayekuzuia wewe usianze biashara ni wewe mwenyewe na wala siyo huyo uliyemkopesha fedha ambaye anakuzungusha katika kukulipa.
Nasema wewe ndiye unayejizuia kuanza biashara na kujiwekea kikwazo kwa sababu umeweka mategemeo yako yote kwenye kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako.
Siku zote kwenye maisha hupaswi kuwa na chaguo moja pekee, kutegemea kitu kimoja ni utumwa, hasa pale kitu hicho kinapokuwa nje ya uwezo wako.
Mfano wewe kwa karibu miaka miwili sasa umekuwa unategemea fedha hiyo uliyomkopesha mtu mwingine, vipi kama hatakulipa kwa miaka mitano? Je utaendelea kusubiri?
Ushauri wangu kwako ni huu, usiweke mategemeo yako ya mtaji kwenye fedha hiyo tu. Jiulize ulipataje hiyo fedha mpaka ukaweza kumkopesha mtu mwingine. Kisha tumia njia hizo kupata fedha nyingine kwa ajili ya kuanza biashara yako. Kama ulijiwekea akiba anza tena kuweka akiba sasa kwa lengo la kupata mtaji wa kuanza biashara.
Ondoa mategemeo yako yote kwenye kulipwa fedha hizo unazodai, na hata kama mtu atakuahidi kesho anakulipa fedha unayomdai, bado hupaswi kuweka mategemeo yako yote kwenye ahadi kama hiyo. Watu wamekuwa wanapenda kuahidi vitu lakini utekelezaji mgumu.
Kamwe usiweke kwenye mahesabu yako fedha ambayo ipo kwenye mfuko wa mtu mwingine. Weka kwenye mahesabu fedha ambayo tayari umeishika kwenye mikono yako. Ukipiga hesabu za kifedha kwa ahadi za watu wengine, utaishia kujikwamisha halafu uwalaumu watu wengine.
Somo jingine kubwa sana unalopaswa kuondoka nalo hapa ni kuacha tabia ya kuwakopesha watu. Kama biashara yako siyo ukopeshaji wa fedha, basi epuka sana kuwakopesha watu wengine fedha. Waachie kazi hiyo wakopeshaji, ambao wanazo njia za kuwabana watu wawalipe. Lakini wewe ambaye huna njia ya kumbana mtu akulipe, kaa mbali na kitu hicho.
SOMA; USHAURI; Hatua Za Kuchukua Pale Watu Uliowakopesha Fedha Hawataki Kukulipa.
Kama kuna mtu ana uhitaji na ipo ndani yako kuweza kumsaidia fanya hivyo, kwa kumsaidia na siyo kumkopesha fedha. Kumbuka mpaka mtu anaingia kwenye changamoto inayomlazimisha kukopa fedha, ana matatizo kwenye eneo la fedha, hana nidhamu ya kutosha. Hivyo unapomkopesha fedha zako, ambazo una mipango nazo, unakaribisha matatizo yake kwenye maisha yako.
Iwe kuna mtu unamdai, au ameahidi kukupa fedha fulani, kamwe usiweke mipango yako yote kwenye ahadi kama hiyo. Badala yake endelea na juhudi nyingine za kukuwezesha kupata kile unachotaka. Ukishaziweka fedha kwenye mikono yako ndiyo unaweza kuzipangia mipango na kuzitumia, lakini kwa ahadi pekee, utajikwamisha.
Usikae zaidi ya mwaka mzima hujaanza biashara kwa sababu unasubiri mtu uliyemkopesha fedha au aliyekuahidi fedha ndiyo uweze kuanza. Badala yake tumia njia mbadala za kukuwezesha kupata mtaji wa kuanza biashara yako.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog